Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imetumia jumla ya Shillingi Billioni 24 katika utekelezaji afua za Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Hayo yamebainika mkoani Morogoro katika kikao kilichowakutanisha Kamati tendaji ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mpango huo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sayi Magessa amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imetekeleza programu mbalimbali zinazosaidia katika kutekeleza afua za Mpango huo.
Magessa amesema kuwa Utekelezaji wa Mpango huo umelenga pia kuimarisha hali ya uchumi wa kaya kwa kutoa fursa na kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali ya jamii kuanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya kujipatia kipato.
Ameongeza kuwa Mwaka 2019/20 Serikali imetekeleza Mpango huo katika masuala ya kuimarisha mazingira ya kufanya biashara nchini, Mpango wa kunusuru Kaya Maskini – TASAF na Upatikanaji wa Mikopo kwa Wajasiriamali ambapo ni nyezo muhimu katika kuhakikisha jamii inapata ustawi wake.
“Niseme tu kuna mafanikio mengi sana yametokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, tumefanikiwa kwa mwaka 2019/2020 kufikia malengo tuliyojiwekea” alisema
Akifungua kikao kazi hicho Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema Serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Dkt. Jingu ameeleza kuwa utatuzi wa migogoro ya ndoa umesaidia sana katika kuhakikisha jamii inakuwa katika mazingira salama hasa katika malezi na makuzi ya watoto na familia kwa ujumla.
Dkt, Jingu ameongeza kuwa Serikali katika kuhakikisha mtoto anapata malezi bora hasa ya wazazi wote kwa mwaka 2019/2020 ilipokea mashauri elfu 38 ya ndoa na jumla ya mashauri elfu 19 yamesuluhishwa na kuwezesha familia kuishi katika amani na watoto kupata malezi bora.
“Familia ndio msingi wa malezi kwa watoto wetu katika hili Serikali tumetekeleza Mpango huu kwa kuhakikisha watoto wanapata malezi katika familia zao” alisema
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha watoto wanapata ustawi wao Serikali imeweza kuwaunganisha watoto 1600 katika familia zao kuwarudisha katika shule na kuwapatia huduma za afya jumla ya watoto.
Dkt. Jingu amesema kuwa jukumu kuu la kikao hicho ni kupitia na kujadili taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ya mwaka 2019/20 na kuweka mikakati itakayowezesha kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa mwaka 2020/21.
“Tunajua Lengo kuu la Mpango wetu ni kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii zetu hivyo ni muhimu kwa wadau na wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kuhakikisha tunaondokana na vitendo vya ukatili dhidi ya makundi haya” alisema
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Save the Children Jesca Ndana amesema Shirika hilo limeshirikiana na Serikali katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hasa katika kutoa elimu na kuhakikisha wanawezesha watoto, wazazi na walimu kuwa na uelewa wa kuzuia vitendo ya ukatili dhidi yao.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Legal Services Facility (LSF) Ramadhani Masele amesema kuwa Shirika hilo limeendelea kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi ikiwemo kuwahamsisha kufahamu haki zao na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanaposhuhudia au kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na wajumbe wa Sekretarieti ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika kikao kilichofanyika mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sayi Magessa akieleza mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa mwaka 2019/20 katika kikao kilichofanyika mjini Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kutoka Wizara, Taasisi, Wakala za Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakifuatilia hoja mbalimblia zilizokuwa zikitolewa katika kikao kilichofanyika mjini Morogoro.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (kushoto) akimsikiliza Mwakilishi wa Shirika la Legal Services Facility (LSF) Ramadhani Masele (kulia) wakati waijadiliana jambo mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati tendaji ya ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika mjini Morogoro.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment