DK.JOHN MAGUFULI AAHIDI KUKAMILISHA BARABARA YA LAMI KUTOKA UVINZA HADI MALAGARASI, AMPIGIA SIMU WAZIRI JAFO | Tarimo Blog

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Uvinza


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wanatarajia kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Uvinza hadi Malagarasi mkoani Kigoma yenye urefu wa zaidi ya kilometa 151.

Ametoa ahadi hiyo leo Septemba 20,mwaka 2020 akiwa njiani akitoa Kigoma Mjini akielekea mkoani Tabora ambapo akiwa na akizungumza na wananchi wa Uvinza , Dk.Magufuli amesema fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo tayari zipo, hivyo wataanza kuitengeneza barabara hiyo.

"Tumetengeneza huko kote pamebakia hapa, hatuwezi kupaacha, hii barabara fedha zipo , sizungumzi kwasababu ya kampeni , msema kweli mpenzi wa Mungu , fedha zipo.Ndio maana nimepita hapa sio kwa helkopta bali kwa gari nione changamoto ya barabara hii,"amesema Dk.Magufuli.

Ameongeza barabara hiyo inatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu , na kwamba watatangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.

Wakati huo huo Dk.Magufuli amezungumzia ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 10 ambayo itajengwa katikati ya Mji wa Uvinza ambapo ametumia nafasi hiyo kumpigia simu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo kwa ajili ya kupeleka fedha Sh.bilioni tano ili kuanza ujenzi wa barabara hiyo na fedha hizo ziwe zimefika kuanzia wiki ijayo.

Pia Dk.Magufuli amezungumzia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Nsibwa hadi Kaya kilometa 237 pamoja na madaraja."Tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Changu hadi Kazilambwa, tumeipangia katika bajeti hii."

Akizungumzia nishati ya umeme, Dk.Magufuli amesema Uvinza imechelewa sana kwani katika vijiji 61 , ni vijiji 17 tu ndio vimefikiwa na umeme."Suala la umeme Uvinza hatujafanya vizuri sana , naomba mnipe kura tukafanye ya ukweli , kwa nchi nzima kwa mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 2018, leo hii tuna vijiji 9700 , vimebaki vijiji 2500 vikiwemo na vya hapa Uvinza,"amesema.

Amesisitiza kuwa atawabana vizuri watu wake akiwemo Waziri wa Nishati ambaye anaamini anasikia changamoto hizo, na kumtaka asikilize na kuanza kutekeleza kwani bado ni Waziri wa Nishati."Waziri Ndalichako, nataka ukamueleze Waziri Kalemani kwamba suala la umeme Uvinza sijalifurahia, kwa hivi vijiji 61 nitavibeba.Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya simamieni hili,"amesema.

Dk.Magufuli amesema ni lazima suala hilo lazima alibebe mwenyewe kwani Uvinza kuna kiwanda cha Chumvi ambacho kinatakiwa kutangazwa ili kuuza chumvi hadi nchi za Burundi , DRC na Uganda.Kwa kufanya hivyo kutasaidia pia vijana kupata ajira."Waziri wa Viwanda abebe kama changamoto kubwa."

Hata hivyo amesema kuwa kuhusu kukatika kwa umeme kwa Wilaya ya Uvinza ni changamoto ya muda mrefu lakini kupitia mradi mkubwa wa umeme katika bwawa la Julius Nyerere ambalo litazalisha umeme megwati 2,115 zitatumika katika gridi ya Taifa na hivyo kuunganisha Uvinza Mkoa wa Kigoma na Kagera.

"Naomba mniamini ndugu zangu katika hili, hii ya kuunganisha katika gridi ya taifa , ambapo kwa mwaka itatumika Sh.bilioni 2.18 na hadi kukamilika kwa mradi huo jumla ya Sh.bilioni 26.16. ili tutae tatizo hilo,",amesema Dk.Magufuli.

Kuhusu sekta, Dk.Magufuli amesema ujenzi wa miundombinu ya afya imejengwa katika maeneo mbalimbali ya Uvinza, ikiwemo pamoja na kuongeza bajeti ya dawa ambayo imesaidia kuboresha huduma za afya , maabara, nyumba za watumishi.Wakati katika elimu nako kuna jitihada ambazo zimefanyika huku akifafanua jumla ya Sh.bilioni 5.04 zimetumika kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya Uvinza.

Pia amesema wamepeleka Sh.bilioni 7.63 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo ambayo imetoa fursa ya elimu kwa watoto wa Uvinza.Kuhusu maji amesema miradi yenye thamani ya Sh.bilioni 11.06 imetekelezwa katika Wilaya ya Uvinza na mingine inaendelea kutekelezwa."Tunaomba mtupe tena nafasi ya kuongoza nchi ili tuendelee kutekeleza miradi ambayo tumeianza" .

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2