Wakuu wa Mikoa Kanda ya Ziwa wavutiwa na Huduma za NBC Maonesho ya Dhahabu na Teknolojia Geita. | Tarimo Blog

   Wakuu wa mikoa ya Mwanza na Geita  wamewaomba  wadau wa sekta ya madini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanautumia ipasavyo ushiriki wa taasisi za fedha ikiwemo Benki ya NBC kwenye  maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayoendelea mkoni Geita ili  waweze kujijengea uelewa wa kutosha katika masuala ya kifedha na mitaji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel walitoa wito huo mwishoni mwa wiki walipotembelea mabanda ya washiriki wa maonesho pamoja na kuongea na wananchi waliotembelea maonesho hayo ya siku kumi yanayofanyika kwenye viwanja vya Bombambili, Mkoani Geita.

“Kupitia maonesho haya habari njema imekuwa ni ushiriki mzuri wa taasisi za fedha ikiwemo Benki ya NBC ambao pamoja na kudhamini maonesho haya pia wanaendesha mafunzo kwa wajasiriamali na wachimbaji wadogo. Hii ni hatua kubwa na wito wangu kwa wadau wa sekta ya madini kuhakikisha wanatumia vema fursa hii kujijengea uwezo wa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kwa viwango bora,’’ alisema Bw Mongella.

Bw Mongella aliongeza kuwa kupitia maonesho hayo taasisi mbalimbali za kifedha zimeweza kutangaza huduma mbalimbali ikiwemo mikopo mahususi kwa ajili ya wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wakubwa na wadogo pamoja na wajasiriamali huku akitolea mfano mafunzo yanayotolewa na Benki ya NBC na wadau wengine kuwa yatawasaidia kujenga uelewa wa kutosha hususani katika masuala ya kifedha na uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini kisasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel alisema kupitia maonesho hayo, mkoa huo unatarajia mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana na mageuzi makubwa ya uendeshaji wa shughuli za kiuchimbaji na biashara yanayotarajiwa kufuatia mafunzo yanayoendelea kufanywa na taasisi mbalimbali kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali.

“Ndio maana tunashukuru sana taasisi za fedha hususani benki ya NBC ambayo ndio wadhamini wakuu kwenye mafunzo haya kwa kuwa chachu ya mabadiliko tunayoyatarajia. Pia, ushiriki wa taasisi nyingine kwenye mafunzo haya ikiwemo  TANTRADE, Tume ya Madini, TRA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, NSSF, GST, SIDO, NEMC, TBS, OSHA na NEEC unatuhakikishia mabadiliko tunayoyatarajia,’’ alisema Mhandi Gabriel

Akifafanua kuhusu huduma  na ushiriki wa benki ya NBC kwenye maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo Cha Mahusiano na Serikali kutoka benki hiyo, Bw William Kallaghe alisema mbali na mafunzo hayo benki hiyo inaendesha huduma nyingine ikiwemo kliniki ya biashara kwa ajili ya wajasiriamali mbalimbali ili waweze kunufaika na mnyororo wa biashara katika sekta ya madini.

“Ni wingi wa huduma maalumu kwa wadau mbalimbali ndio unaosababisha benki ya NBC tuweze kushiriki kwenye maonesho ya wadau tofauti tofauti yakiwemo maonesho haya ya dhahabu na teknolojia. Kwa upande wa sekta ya madini  tunazo bidhaa au huduma maalumu kwa ajili yao ikiwemo Klabu ya Biashara, internet Banking na mikopo isiyo na dhamana inayolenga kuwajengea uwezo wa kifedha wanapoendesha shughuli zao.’’ Alibainisha Bw Kallaghe.

Aliongeza kuwa ili huduma za kifedha ziweze kuleta tija kwa wadau hao wa sekta ya madini, benki hiyo imeona ipo haja ya kutoa mafunzo hayo yatakayowasaidia washiriki kuzitambua fursa za kibiashara ambazo wanaweza kunufaika nazo sambamba na mafunzo ya uchimbaji wa kisasa.

 Meneja Mahusiano Serikalini wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) William Kallaghe (Kushoto) akiwatambulisha baadhi ya maofisa wa benki hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (wapili kushoto) wakati mkuu wa mkoa huyo alipotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya Dhahabu na Teknolojia vya Bombambili mkoani Geita. 

 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (katikati) akisaini kitabu cha wageni cha Benki ya NBC alipotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya Dhahabu na Teknolojia vya Bombambili mkoani Geita. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (Kulia) na  Meneja Mahusiano Serikalini Benki ya NBC Bw William Kallaghe (Kushoto)

 Meneja Mahusiano Serikalini Benki ya NBC Bw William Kallaghe (Kushoto) akielezea kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki mahususi kwa ajili ya wadau wa sekta ya madini nchini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (katikati) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (Kulia)  wakati viongozi hao walipotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya Dhahabu na Teknolojia vya Bombambili mkoani Geita. Wanaoshuhudia ni baadhi ya maofisa wa benki hiyo.


 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (wa tatu kushoto)akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya Dhahabu na Teknolojia yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita. Anaeshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (wa pili kushoto) pamoja na baadhi ya maofisa wa benki ya NBC.

 Meneja Mahusiano Serikalini Benki ya NBC Bw Taifa William Kallaghe (Kushoto) akielezea kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo mahususi kwa ajili ya wadau wa sekta ya madini nchini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (katikati) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (Kulia)  wakati viongozi hao walipotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya Dhahabu na Teknolojia vya Bombambili mkoani Geita. Wanaoshuhudia ni baadhi ya maofisa wa benki hiyo.

 Baadhi ya maofisa wa benki ya NBC wakitoa huduma kwa wateja na washiriki mbalimbali wa maonesho ya Dhahabu na Teknolojia yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2