DK.JOHN MAGUFULI ASEMA TANZANIA SIO MASIKINI, UONGOZI HAUJARIBIWI | Tarimo Blog




Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Geita

WAKATI Mgombea urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli akiendelea kukukutana na maelfu ya Watanzania katika mikoa mbalimbali nchini akiwa katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu ametumia nafasi hiyo kueleza Tanzania ni nchi tajiri , sio masikini kwani inakila kitu na wanaoiita ni masikini waache.

Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Geita, Dk.Magufuli amefafanua "Tanzania ni tajiri, huwezi kuwa masikini wakati tuna madini, huwezi kuwa masikini wakati tuna maziwa yamekuzunguka, huwezi kuwa masikini wakati hata Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu uko kwetu, hata mti mrefu kuliko yote uko Tanzania.

"Tunachotakiwa ni kuzitumia rasilimali zetu tulizonazo vizuri, tuanze kusema sisi ni matajiri, sisi sio masikini maana ulimi huumba.Bajeti ya maendeleo imeongezeka kutoka asilimnia 25 hadi 40, na hivyo hata bajeti ya miradi imeongezeka.Miradi mikubwa inaendelea kujengwa, tumenunua ndege 11 na tutanunua nyingine, ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea. haya mafanikio ni kwasababu mlituamini,hivyo lazima tufanye kazi,"amesema Dk.Magufuli.

Amefafanua kazi kubwa ambayo inafanyika ya kuleta maendeleo ni kutaka kuithibitishia Dunia Tanzania imengia kwa kasi katika kuleta uchumi. "Tumetoka kuwa nchi masikini hadi yenye uchumi wa kati. Kama tumeikuta nchi inaitwa masikini na leo imeingia uchumi wa kati huu ndio wakati wa kutupa kura.

"Mbinu za kufika huko tunazo, mbinu za kubana mafisadi tunazo, uongozi sio wa kujaribu, uongozi haujaribiwi, ni bora ujaribu gongo, unaweza kujaribu kupanda mlima ukikhindwa unarudi nyuma, kujaribu uongozi madhara yake ni makubwa, kuna nchi mpaka leo zinapigana, wananchi wanakimbia, ziko nchi hata za kabila moja wanapigana,"amesema Dk.Magufuli.

Wakati huo huo Dk.Magufuli amezungumzia kuhusu uhuru wa Watanzania katika kufanya ibada na kumuabudu Mungu, hivyo makanisa na misikiti yote ruksa wakati kuna baadhi ya nchi hata uhuru wa kuabudu haupo."Mnakumbuka hata wakati wa Corona walifunga misikiti na makanisa, sisi tukasema hapana lazima tuendelee kumuomba Mungu kwani kwenye Mungu hakuna kinachoshindana.

"Corona ilikwenda kwa wengine huko, tumshangilie Mungu kwa kupiga miluzi, Mungu hoyee, hayo ndio maajabu ya Mungu katika nchi yetu.Ndio faida ya kumtanguliza Mungu, watu wengine waje wajifunze Tanzania jinsi tulivyofanikiwa katika Corona.Tuliambiwa tufunge midomo yetu, tuliambiwa tusitoke nje sasa tungefanya shughuli zetu saa ngapi, madhara yalikuwa makubwa.Inawezekana watu wameshasahau na hawaoni.

Pia Dk.Magufuli ameelezea kuhusu wabunge wa vyama vya upinzani ambavyo wamekuwa na tabia ya kutoka bungeni , hivyo ameomba wananchi kuchagua wabunge wa CCM ambao ndio hukaa bungeni kwa ajili ya kupitisha bajeti za maendeleo ya Watanzania.

"Hii miradi inayoendelea sasa ilipitishwa na wabunge wa CCM.Hata hii bajeti ya Uchaguzi Mkuu imepitishwa na wabunge wa CCM , ni bajeti ya kwetu kwa asilimia 100, msijaribu uongozi. Hawa wagombea ubunge wa CCM nawafahamu, wamechujwa kweli kweli.

"Wakati nakwenda kuzindua Bunge wapinzani walitoka, lakini mishahara wamepokea kwa miaka yote mitano, posho na marupurupu wamechukua kwa miaka mitano.Sio kwamba nawasema ila nataka wananchi mchambue ninyi wenyewe,"amesema Dk.Magufuli.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2