DK.MAGUFULI ATAJA MABILIONI YA FEDHA YALIYOTUMIKA KUPELEKA MAENDELEO KAGERA, AGUSIA KUKATIKA KWA UMEME | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe, Michuzi TV -Kagera

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na Mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa tiketi ya Chama hicho Dk.John Magufuli ameeleza kwa kina maendeleo ambayo yamefanyika katika Mkoa wa Kagera huku akitumia nafasi hiyo kuzungumzia mkakati uliopo katika nishati ya umeme ambao umekuwa ukikatika mara kwa mara katika mkoa huo.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Kagera leo Septemba 16, mwaka 2020 wakati wa mkutano wake wa kampeni ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kuwa Rais kwa miaka mingine mitano, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano kazi kubwa imefanyika katika kuboresha sekta ya nishati ya umeme.

"Vijiji vyenye umeme vimeongezeka kutoka 168 mwaka 2015 hadi kufikia vijiji 541 na Kagera kuna vijiji 664, hivyo vimebaki vijiji 123 kupata umeme.Mkitupa miaka mingine mitano, ile miaka ya mwanzo ile mitatu vijiji ambavyo vimebakia vyote vitakuwa na umeme.

"Tanzania tutakua na umeme wa kutosha na hasa baada ya kukamilika bwawa la Julius Nyerere ambalo litakuwa linalisha megawati 2115 .Nafahamu Kagera kuna tatizo la umeme kukatika, unaangalia TV umeme unakatika, nataka niwaambie Kagera na naahidi tutakapounganisha umeme wa gridi ya Taifa hili suala halitakuwepo tena,

"Kuna miradi mingi ya umeme ambayo ipo katika maeneo mbalimbali ukiwemo mradi wa maji Rusumo ambao unaendelea kutengenezwa ambao utazalisha megewati 80.Bado kuna miradi mingine ya Kinyerezi ii, na Kinyerezi i .Pia tutatumia umeme wa gesi.Kwa hiyo nataka kuwakikishia ndugu zangu tutakuwa na umeme megawati 5000.

"Kwa hiyo suala la umeme litakuwa la uhakika , hatutegemea tena umeme wa nchi jirani hapa Kagera.Tunaamini tukiwa na umeme wa kutosha suala la umeme kukatika viwandani litakuwa historia, "amesema Dk.Magufuli.

Kuhusu sekta ya afya, Dk.Magufuli amesema katika Mkoa wa Kagera zimejengwa hospitali nne za Wilaya ambavyo vimejengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 5.9, idadi ya vituo vya upasuaji na sasa viko 21, zahanati 10 na nyingine 16 zinamalizika wakati kwenye bajeti ya dawa kwa Mkoa wa Kagera imeongezeka kutoka Sh.bilioni 2.3 hadi Sh.bilioni 8.6 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.Magari ya kubeba wagonjwa yamenunuliwa 10 na hayo ni baadhi tu yaliyofanyika kwa miaka mitano

Kwa upande wa maji, Dk.Magufuli amesema kuna mabilioni ya fedha yametumika katika kufanikisha miradi ya maji ikiwemo miradi 154 imetekelezwa pamoja na miradi ya maji yenye thamani ya Sh. bilioni 5071.Wakati Sh.bilioni 59 ya maji katika maeneo ya mjini ukiwemo mradi wa maji Bukoba mjini ambao utagharimu bilioni Sh.52.

Wakati huo huo amezungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga ambalo nalo linakwenda kufungua fursa ya kiuchumi."Bomba litapita hapa Kagera na mikoa mingine saba. Faida ambayo itakuwa inapatikana Tanzania asilimia 60 na Uganda asilimia 40, ni kitu kikubwa sana, hili bomba lingeweza kupita kwingine, tulipambana sana kulipitisha hapa,"amesema Dk.Magufuli.
 
Mgombea Urais kupitia Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia maelfu ya Wananchi wa mkoa wa Kagera katika mkutano wa Kampeni za CCM uliofanyika katika viwanja vya Gymkhana Bukoba mkoani Kagera leo tarehe 16 Septemba, 2020
Sehemu ya Wananchi wa mkoa wa Kagera waliokusanyika katika Viwanja vya Gymkhana kumsikiliza Mgombea Urais kupitia Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Septemba, 2020

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2