***************************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
HALMASHAURI ya Mji Kibaha ,Pwani unatarajia kukamilisha ujenzi mkubwa wa machinjio ya kisasa eneo la Mtakuja lenye ukubwa wa ekari 27, kata ya Pangani utakaogharimu zaidi ya sh.bilioni 2,9.
Kukamilika kwa ujenzi huo utawezesha kuboresha afya za wananchi walaji wa kitoweo cha nyama kitakachoandaliwa kwenye mazingira bora mkoa wa Pwani na Mkoa jirani wa Dar-es-Salaam.
Meneja wa TARURA, Halmashari ya Mji Kibaha Mhandisi Bupe Anjetile amebainisha kuwa ujenzi ulianza rasmi tarehe 22 Aprili, 2019 na kukamilika Mwezi Novemba 27, 2019 na sasa upo kwenye matazamio ya miezi 12, itakayokamilika tarehe 24 Novemba, 2020.
Mhandisi Bupe alisema, ujenzi ulifanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya mwanzo iligharimu kiasi cha Tsh.804,309,600.00 huku awamu ya pili ikitumia kiasi cha tsh.1,993,004,027.30 pamoja na gharama za ununuzi na ufungaji wa mitambo ya uchinjaji huku Tsh.140,000,000.00 zikilipwa kwa wahandisi washauri.
“Kandarasi ya Ujenzi huu inafanywa kupitia kampuni ya M/S Petra Construction ya Jijini Dar-es-Salaam kwa kushirikiana na Kampuni za M/s B.J Amuli Architects partnership, Mbega and associates na MAS-Q Associates kama kampuni za ushauri ambazo ni kampuni za wazawa zote za jijini Dar-es-Salaam” alifaffanua Bupe.
Nae mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Jenifa Omolo aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuiwezesha Kibaha kuwa miongoni mwa Miji 18 inayofadhiriwa na mpango wa uendelezaji miji-ULGSP .
Alieleza lengo la mradi huu ni kuboresha huduma za uchinjaji ili kupata kitoweo bora na salama kitakachoandaliwa kwenye mazingira mazuri ili kuimarisha sekta ya mifugo, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuleta tija kwa wafugaji na kuinua uchumi wa Kibaha.
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Charles Makanya Marwa alisema kuwa,licha ya kuboresha kitoweo kwa walaji pia utaongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo, kama ngozi, Damu, Pembe na Samadi ambayo itakusanywa na kutolewa bure kwa wananchi wa maeneo ya jirani .
Marwa aliongeza kuwa pia utakua miongozi mwa vyanzo vikubwa vya mapato kwani utakapoanza kufanya kazi utakuwa na uwezo wa kuchinja Ng’ombe kuanzia 200 na wanyama jamii ya Mbuzi 250 kwa wakati mmoja .
“Halmashauri itapata wastani wa Tsh.1,650,000.00 kwa siku kama gharama za uchinjaji kwani kila Ng’ombe hulipiwa tsh.5000.00 huku mbuzi ama Kondoo alilipiwa tsh.2,500.00 kama gharama za uchinjaji.”;
Ujenzi huo umefikia asilimia 95 huku asilimia 5 iliyobaki itakamilika baada ya kufunga mitambo ya kuchinjia.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment