Na. Farida Ramadhani na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma
Serikali imezitaka Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinapata kibali cha Waziri wa Fedha na Mipango kabla ya kuanzisha mfumo wowote wa kielektroniki wa usimamizi wa fedha za umma kama ilivyoelekezwa katika Waraka wa Hazina.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James wakati wa hafla ya kupokea ripoti ya tathmini ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma.
Bw. James alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango ndio yenye mamlaka ya kutoa muongozo wa uanzishwaji wa mifumo ya usimamizi wa fedha za umma na kutoa angalizo kuwa wote watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Nawasisitiza Maafisa Masuuli wote kuhakikisha mnapata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya kufanya ununuzi, uundaji, usimikaji na utumiaji wa mfumo wowote wa kielektroniki wa usimamizi wa fedha za umma katika mafungu au Taasisi zenu kama ilivyoelekezwa katika Waraka huo”, alisisitiza Bw. James.
Alisema kuwa Serikali hufanya jitihada mbalimbali katika kuboresha na kuanzisha mifumo mbalimbali ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato na kusimamia matumizi ya Fedha za Umma.
Alisema mpaka sasa Serikali imeshabuni na kutengeneza mifumo mikubwa ya kielektroniki minne ambayo ni Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG), Mfumo wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi na Malipo ya Serikali (MUSE), Mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo (NPMIS) na Mfumo wa Usimamizi wa Misamaha ya Kodi.
Bw. James alibainisha kuwa Mfumo wa MUSE unawezesha Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri zote, Wakala na Taasisi zingine za Serikali kusimamia na kudhibiti mapato, malipo ya matumizi ya kawaida nakulipa malipo kwa njia ya kiektroniki kupitia Benki Kuu na Benki za Biashara.
Akizungumzia Mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo (NPMIS), Katibu Mkuu huyo alisema mfumo huo ulianzishwa ili kuiwezesha Serikali na wadau wengine kupata taarifa sahihi za miradi ya maendeleo kwa wakati.
Alisema kuwa kila Taasisi inayotaka kutekeleza mradi wowote wa maendeleo ni lazima ahakikishe kuwa inatumia mfumo katika kufanya maombi na utekelezaji wa mradi. Hakuna malipo au mgao wa pesa za maendeleo zitalipwa nje ya mfumo. Nazitaka taasisi zote zenye miradi inayotegemea pesa kutoka Serikalini kuhakikisha miradi yote iko kwenye kanzidata hii ya miradi”, alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema Mfumo wa GePG ulianzishwa kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za ukusanyaji mapato ikiwemo ugumu wa kupata taarifa ya makusanyo yanayofanyika kwa wakati huo huo, gharama kubwa za miamala inayohusu makusanyo ya Fedha za Umma, utaratibu usio rafiki kwa Mlipaji wa huduma za umma na machaguo machache ya njia za kulipia (Benki, Mitandao ya simu za mkononi au Mawakala).
Alisema pia Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Serikalini umeanzishwa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo Serikalini katika zoezi zima la usimamizi na utoaji wa misamaha ya kodi ya ongezeko la thamani Serikalini ikiwemo Wizara/Taasisi/Halmashauri kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango baadhi ya orodha za vifaa visivyokidhi vigezo vya kupata msamaha wa VAT.
Kwa upande wake Mtafiti aliyefanya tathmini ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanya wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Joel Mtebe, alisema kuwa, alifanya utafiti katika taasisi za Serikali 271 kwenye mikoa 11 na kubaini kuwa mfumo umerahisisha ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali kwa asilimia 87 kutokana na wananchi kutokwenda moja kwa moja katika ofisi kulipia huduma.
Naye Mhasibu Mkuu wa Serikali, Francis Mwakapalila, alisema kuwa Mifumo ya Fedha iliyoanzishwa na Serikali ukiwemo Mfumo wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi na Malipo ya Serikali (MUSE), umeokoa takribani Shilingi bilioni tano zilizokuwa zikitumika kununua leseni za mifumo iliyokuwa ikitengenezwa nje ya nchi.
Kwa upande wa wanufaika wa mifumo hiyo akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Willium Erio, alisemakuwa Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG), umesaidia kuongeza mapato kutoka Sh. bilioni 994 kwa miaka miwili iliyopita hadi takribani Sh. trilioni 1.1 kwa sasa.
Alisema kuwa ongezeko la mapato hayo umetokana na mifumo kuondoa mianya ya mapato kuvuja na kupungua kwa gharama za miamala.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James akizungumza wakati wa halfa ya kupokea ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, ambapo amewaagiza Afisa Masuhuli wote nchini kutotengeneza mifumo yoyote bila kupata kibali kutoka wizara hiyo, jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James (wapili kushoto), wakifatilia uwasilishwaji wa ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James akimsikiliza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede baada ya kumaliza halfa ya upokeaji ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, jijini Dodoma.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Francis Mwakapalila, akizungumza wakati wa halfa ya kupokea ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Wiliam Erio akizungumza wakati wa halfa ya kupokea ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Kifedha, Bw. John Suasi akiteta jambo, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Alfred Dede (kushoto) na Dkt. John Kalugendo baada ya halfa ya kupokea ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James (katikati), ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Menejimenti ya wizara hiyo baada ya halfa ya kupokea ripoti ya tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, jijini Dodoma.
(Picha na WFM – Dodoma).
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment