Na Ramadhani Ali – Maelezo
Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amewashauri Maimamu na Makhatibu wa Misikiti pamoja na Walimu wa Vyuo vya Qur ani kuhubiri amani wakati nchi inaelekea kwenye Uchaguzi mkuu mwezi Octoba.
Sheikh Khalid ametoa ushauri huo katika uzinduzi wa ugawaji mas-hafu kwenye vyuo vya Qur-an vya Wilaya zote za Zanzibar yaliyotolewa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiislamu ya Al Salaam ikishirikiana na Ofisi ya Mufiti wa Zanzibar. hafla iliyofanyika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya Magharibi ‘A’ Kianga.
Amesema wananchi wanahitaji amani hivyo mahubiri yatakayotolewa na Mashekhe na Maimamu wa misikiti yaelekezwe katika kuimarisha umoja, amani na utulivu.
Alikumbusha kuwa Dini ya Kiislamu haishawishi fujo bali inahimiza amani na ushirikiano hivyo aliwataka viongozi hao kuelekeza mahubiri yao kama dini inavyoelekeza.
“Usalama na amani ndio mtaji wetu, bila ya amani hakuna maisha nani ataweza kutoka kutafuta mahitaji ya familia yake wakati nchi inafujo,” aliuliza Katibu wa Mufti.
Aliwaeleza walimu wa vyuo vya Qur an kwa upande wao kuacha tabia ya kuwaingiza wanafunzi wao kwenye misimamo ya kisiasa kwani kufanya hivyo ni kuwapeleka katika matatizo bila ya muda wao kufika.
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A“ Maalim Abeid Juma Ali ambae alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo aliwanasihi viongozi wa dini kuendelee kutoa mahubiri yanayoelekezea jamii katika ustawi mzuri wa maisha yao.
Aliweka wazi kuwa Wilaya yake haitmvumilia kiongozi yoyote wa dini atakaeanzisha mahubiri ya kushawishi waumini wao kuvunja sheria za nchi.
Maali Abeid aliishukuru Serikali ya Kuweit kwa misaada mbali mbali inayotowa kwa Jumuiya ya Kiislamu ya Al Salaam ambayo imeanza kuwasaidia wananchi wa Zanzibar.
Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya ya Al Salaam katika hafla hiyo iliyofanyika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi “A”, Mwenyekiti wa Jumuiya Sheikh Khamis Masoud alisema wamekusudia kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu na Jengo la Dakhalia kwa ajili ya waislamu wa kike.
Jumuiya hiyo imeanza kusambaza zaidi ya mas-hafu 336, 000 iliyotolewa msaada na Serikali ya Kuweit kwa ajili ya vyuo vya Wilaya zote za Zanzibar na wameanza na Wilaya ya Magharibi A.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Al-salaam Sheikh Khamis Massoud Omar akitoa historia ya Jumuiya yao kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa Mas-hafu katika Wilaya za Zanzibar ulioanza Wilaya ya Magharibi A hafla iliyofanyika Ofisi ya Halmashauri magharibi A Kianga.
Muhadhir maarufu wa dini ya Kiislamu Shekh. Othman Maalim akitoa mawaidha juu ya fadhila za kuhifadhi Quran Tukufu katika uzinduzi wa ugawaji wa Mas-hafu iliyotolewa na Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Salaam.
Baadhi ya Wanajumuiya, Mashekhe na Walimu wa Qur an wa Wilaya ya Magharibi A wakisikiliza nasaha za Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya Maghari A Maalim Abeid Juma Ali (hayupo pichana) alizozitoa wakati wa zinduzi wa ugawaji wa Mas-hafu katika Wilaya yake.
Katibu wa Mufti Khalid Ali Mfaume akimkabidhi misahafu Mkuu wa Wilaya Magharibi A katika uzinduzi wa ugawaji Mas-hafu kwa Wilaya zote za Zanzibar hafla iliyofanyika Halmashauri magharibi A.
Mkuu wa Wilaya Magharibi A Maalim Abeid Juma Ali (katikati) katika picha ya pamoja na masheha na viongozi wa Jumuiya ya Al-Salaam. Picha na Makame Mshenga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment