KESI YA UCHOCHEZI YA MGOMBEA URAIS CHADEMA YAZIDI KUPIGWA KALENDA | Tarimo Blog

KESI ya chochezi inayowakabili mgombea wa Urais nchini, Tundu Lissu na wenzake watatu iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa imeendelea kusogea mbele kwa kushindwa kuendelea kusikilizwa kwa sababu mshitakiwa huyo yupo kwenye kampeni za  kugombea urais.

Mapema leo Septemba 14, 2020 Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa lakini mshitakiwa Lissu na Jabir Idrisa hawapo mahakamani.

Hata hivyo, Mdhamini wa Lissu aliyefika mahakamani hapo Robert Katula alidai amewasiliana na watu wa karibu na mshitakiwa na kuelezwa kuwa yupo kwenye kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Simba  ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 15, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea  kusikilizwa.

Mbali na Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni , Wahariri wa gazeti la Mawio,Simon Mkina, Jabir Idrisa pamoja na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Katika kesi hiyo, Lissu na wenzake  wanakabiliwa na mashitaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa, Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washitakiwa Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia, Januari 14, 2016 washtakiwa hao walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshitakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Aidha, washtakiwa hao wanadaiwa kuwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu  kitendo wanachodaiwa kufanya bila ya kuwa na mamlaka yoyote.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2