MFUMO MPYA WA HCMIS KUHIFADHI TAARIFA MUHIMU ZA KIUTUMISHI NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MADAI YA MALIMBIKIZO YA MISHAHARA | Tarimo Blog

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo hayo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.



Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Wilaya ya Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS mara baada ya Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael kufungua Mafunzo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango akitoa neno la utangulizi kuhusiana na mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS yaliyofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. FrancisMichael kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma leo.

*********************************

Na James Mwanamyoto- Dodoma

Tarehe 14 Septemba, 2020



Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) uliotengenezwa na wataalam wa ndani una uwezo wa kuhifadhi taarifa muhimu za Watumishi wa Umma tangu kuajiriwa kwao na utatatua changamoto nyingi za kiutumishi ikiwamo ya madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.

Dkt. Michael amesema Mfumo huo pamoja na kujumuisha taarifa zote muhimu zinazohusu maendeleo ya Mtumishi wa Umma tangu aajiriwe hadi anapofikia ukomo wa ajira yake, pia unajumuisha taratibu zote muhimu za kiutendaji katika Utumishi wa Umma.

“Tofauti na Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa, Mfumo huu mpya unahifadhi taarifa za Miundo ya Taasisi za Umma, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, Miundo ya Mishahara ya Watumishi, Ikama na Bajeti, taarifa za Ajira za Watumishi na matukio yote yanayowahusu, malipo ya mishahara yao, makato ya marupurupu yao kwa kila mwezi na upandishwaji vyeo,” Dkt. Michael amefafanua.

Dkt. Michael ameainisha kuwa, Mfumo mpya utaondoa changamoto ya madai ya malimbikizo ya mshahara ya muda mrefu pindi Mtumishi anapopandishwa cheo, kwani mara baada ya kupanda cheo, taarifa zake zitabadilishwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupata mshahara mpya.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa, Mfumo huo uliotengenezwa na wataalam wa ndani wa Serikali, unaakisi mahitaji ya ndani ya Serikali, utaimarisha usalama wa taarifa na nyaraka pamoja na kupunguza gharama za matengenezo na ulipiaji leseni ambapo Serikali ilikuwa ikitumia dola 217,000 kwa mwaka ambazo hivi sasa zitatumika katika miradi ya maendeleo nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Wilaya ya Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, ameipongeza Serikali kutengeneza Mfumo kwa kutumia wataalam wa ndani, kitendo kinachoashiria nchi yetu imeanza kujitegemea kwenye eneo la mifumo.

Bw. Kilaja ameahidi kuyafanyia kazi mafunzo watakayoyapata ili watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi waweze kuutumia mfumo vizuri kama Serikali ilivyokusudia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango amesema, Mafunzo yatakayotolewa kwa kundi la kwanza la Maafisa Utumishi na Utawala, yamepewa muda mrefu wa wiki mbili kwani ndio walengwa wakuu na watumiaji wa mfumo, muda huo utawawezesha kufahamu vizuri namna mfumo unavyofanya kazi.

Bw, Kiwango ameongeza kuwa, Mfumo mpya ambao utatumika badala ya Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa, umeshafanyiwa majaribio, na Serikali imejiridhisha kwamba uko tayari kwa ajili ya kuanza kufanya kazi rasmi na utakuwa bora zaidi ya unaotumika sasa.

Maandalizi ya Mfumo Mpya wa HCMIS ulianza mwaka 2018 kwa kukusanya mahitaji ya wadau kutoka kwenye taasisi mbalimbali za Serikali, usanifu na ujenzi wa Mfumo ulianza mwaka 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2020.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2