DK.JOHN MAGUFULI ASEMA LAZIMA TANZANIA IJITEGEMEE KIUCHUMI, SIO KUSUBIRI WAFADHILI | Tarimo Blog


Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Chato

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na Mwenyekiti wa Chama hicho Dk.John Magufuli amesisitiza kuna kila sababu ya Tanzania kuwa na uchumi wa kujitegemea ambao hautegemei fedha za wafadhili katika kufanya maendeleo yake.

Dk.Magufuli amesema hayo leo Septemba 14,2020 akiwa katika Viwanja vya Mazaina wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita alipokuwa akiomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kwa nafasi ya urais kwa kipindi cha miaka mitano mingine.

Amefafanua kuwa wapo watu ambao mawazo yao siku zote yamekuwa ni kusubiri fedha kutoka kwa wafadhili na kuhoji kwani hao wafadhili hawataki kuishi huko kwao.

"Wafadhili wakuletee wewe, ukichukua fedha ya wafadhili wewe utalipa mara mbili yake, atakwambia anakuletea ufadhili halafu wanakuletea masharti mengi,"alisema Dk.Magufuli.

Dk.Magufuli amesema kabla ya kuwa Rais amefanya kazi katika wizara tofauti tofauti ikiwemo Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kwamba anajua maana ya ufadhili.

"Anayetegemea cha ndugu hufa masikini na ukiona wanakuganda ujue wanataka kukunyonya.Hata nchi za Ulaya zimefanya maendeleo kwa kutumia fedha zao wenyewe,"amesema.

Pia amesema vitabu vya dini navyo vimeandika kuhusu kodi na ndio maana wanasema ya Kaisari muachie Kaisari."Mtu anasimama mashavu yamemvimba anasema akichaguliwa atafuta kodi.Mwingine anazungumzia masuala ya ya kula ubwabwa wakati hata nyumbani kwake haumtoshi, na wengi wanasema wanakula bata wakati hata vitabu vya dini vinasema asiyefanya kazi na asile".

Amesema ni vema watu wakaambiwa ukweli kwani kipindi hiki cha kampeni kuna mengi yatasikika yakisemwa lakini kikubwa ni sera za wagombea na kisha kufanya maamuzi sahihi.

Wakati huo huo amesema uongozi ni kujitoa sadaka na yeye ameamua kujitoa sadaka kwa Watanzania, licha ya kuwa ni kazi ngumu lakini anaiweza , hivyo anaomba tena kwa miaka mitano.

Hata hivyo amewataka wananchi wasifanye majaribio kwa kuweka watu wengine kwenye uongozi kwani hadi sasa katika hao wanaogombea urais hakuna mmoja anayeweza kufanya kazi ambayo ameifanya hata robo.

Wakati huo huo Dk.Magufuli amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakisema nchi yetu haina mahusiano mazuri ya kimataifa ambapo amehoji kwani mahusiano ya kimataifa lazima mtu uende Ulaya.

"Nimekuwa Mwenyekiti wa SADC wanakuchaguaje kuwa Mwenyekiti kama huna mahusiano nao, katika kipindi cha miaka mitano tumefungua balozi nane.Wanaweza kuja kuchukua hati ya utambulisho kama huna uhusiano nao, na juzi nimepokea hati ya Balozi wa Marekani,"amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza mahusiano sio kwenda Ulaya peke yake na kwamba nataka kuwa na uhusiano na Watanzania ambao wamemchagua na kumuweka madarakani."Najua nina deni kubwa kwao, hata sasa nina mualiko wa kwenda Umoja wa Mataifa lakini siendi , nitamtuma balozi aliyeko huko, aende."
 Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Tawala na Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amejawa furaha na bashashaakiondoka katika viwanja vya Mazaina mjini Chato mkoa wa Geita baadaya kuhutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi kwenye mkutano wake wa
hadhara wa kampeni leo Septemba 14, 2020.
 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2