Mkurugenzi Mtendaji akutana na Wakuu wa Taasisi za Serikali jijini Dodoma | Tarimo Blog

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi  amefanya kikao na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Serikali Jijini Dodoma ili kuandaa mpango wa kuibua fursa za uwekezaji zinazotokana na kuwepo wa mradi wa Reli ya kisasa (Standard Gauge Railway – SGR). 


Kikao hicho kilihudhuria na Wakuu wa Taasisi za Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu (LATRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na wawakilishi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Kazi alisema, “kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji Na. 26 ya Mwaka 1997, miongoni mwa majukumu ya TIC ni kuibua, kuhamasisha na kunadi fursa za uwekekezaji nchini”. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania alieleza kuwa, ujio wa Reli ya SGR unaambatana na fursa nyingine za uwekezaji kwa sekta mbalimbali ambazo zinahusishwa na Wadau wengi hivyo, kikao kilihitaji kuwepo na uelewa wa pamoja kati ya TIC na Taasisi zinazohusika moja kwa moja na uwekezaji katika mradi wa SGR kabla ya kuitisha Kikao cha wadau mbalimbali na Serikali watakaohusika na kuibua fursa za uwekezaji zinazoambatana na mradi wa SGR. 


“Kusudi la reli hii ni zaidi ya usafirishaji (kubeba abiria na mizigo), ndio maana Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimeona ni vema kuibua fursa au shughuli za kiuchumi zinazotakiwa kufanyika katika maeneo ya pembezoni mwa reli, ili kuleta ufanisi na tija kwa  reli, nchi na jamii iliyopo pembezoni mwa reli hii. Uwepo wa Reli hii ni mojawapo ya maboresho ya mazingira ya uwekezaji kwenye miundombinu yanayofanywa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli” Alisema Dkt Kazi.

 

Mmoja wa wakuu wa Taasisi walioshirikinkatika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Ndg. Masanja Kadogosa alisema “tunawapongeza Kituo Cha Uwekezaji Tanzania kwa jitihada za kuratibu mpango huo na sisi kama Shirika la reli Tanzania tupo tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya kuhakikisha reli hii inaleta manufaa zaidi kwa jamii iliyopo pembezoni mwa reli ya SGR”. 


Vilevile, pamoja na mambo mengine, Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt Edwin Mhede alisema “mpango huu ushirikishe sekta binafsi na wadau wengi zaidi upande wa serikali na kila Taasisi itakayohusika ipewe jukumu lake na kutekeleza kwa wakati na upande wa serikali tuwe tayari kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania ili kufanikisha mpango huu mzuri wenye nia ya kuifanya reli yetu isiishie kubeba mizigo na abiria tu, bali iende sambamba na faida nyingine za kiuchumi, uwekezaji pamoja na elimu kwa mlipa kodi ili tuweze kukusanya mapato ya serikali bila kuwaletea usumbufu wawekezaji”.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2