MWANASIASA ANAPOIBUKA NA HOJA YA SERIKALI ZA MAJIMBO | Tarimo Blog

 

Na Sultan Kipingo.

Katika siku za karibuni, mwanasiasa mmoja ameibuka tena na hoja ya serikali za majimbo. 

Kwa mtazamo wangu, muundo wa serikali za majimbo si suluhisho la matatizo ya watanzania. Kwa lugha nyingine, maendeleo ya Watanzania na Waafrika yataletwa na mikakati mahususi ya kimaendeleo, na si ubadilishwaji wa miundo ya serikali.

Kwa ufafanuzi, tuanze na yafuatayo:

1.       Iwapo katika ulimwengu wa sasa, nchi zote zina miundo sawa ya uongozi;

2.       sababu zilipelekwa nchi tofauti duniani kuwa na miundo tofauti ya kiutawala/serikali; na

3.       iwapo kuna uhusiano kati ya miundo ya serikali/kiutawala (ufalme/serikali za kitaifa/serikali za majimbo) na  na hali ya maendeleo ya wananchi (huduma bura za afya, elimu, maji, mausha bora, amani n.k.)

Kwanza kabisa, ukweli ni kwamba katika ulimwengu wa sasa, nchi tofauti zina miundo tofauti ya serikali/kiutawala. kama aina fulani ya muundo wa serikali (mathalan muundo wa serikali za majimbo) ungekuwa ni suluhisho la matatizo ya wananchi na kiutawala, basi dunia nzima ingefuata mfumo huo!

Kutokana na ukweli kwamba nchi tofauti duniani zina mifumo tofauti ya serikali/kiutawala, ni vema kusisitiza kwamba uamuzi juu ya muundo wa serikali/kiutawala siyo suala la kufanyia maamuzi katika majukwaa ya kampeni. Hivyo basi, ni vyema kufahamu sababu zilizopelekea nchi tofauti duniani kuwa na miundo tofauti ya kiutawala/serikali. Na ukweli ni kwamba,

Kwa kuwa suala husika ni serikali za majimbo, nitajikita katika mifano inayoonyesha kwamba kila nchi ina historia yake, na kwa sababu hiyo, muundo wa serikali si suala la kuiga eti kwa sababu wengine wanafanya

Mara nyingi, wanaoongelea serikali za majimbo hutolea mifano nchi za Ujerumani, Marekani na Uswisi, japo Nigeria, Ethiopia, Russia, Venezuela, Pakistan na Somalia pia zina muundo wa serikali za majimbo (pitia katiba za nchi husika). Kwa kufupisha mjadala, tuangalie nchi za Ujerumani na Marekani , ambazo hutolewa mifano zaidi katika mijadala inayohusu serikali za majimbo.

Nchini  Ujerumani , kwa ufupi sana, historia ya majimbo ya Ujerumani inarudi nyuma hadi enzi za utawala wa Kirumi, kufuatia makubaliano ya amani ya ,Westphalia na katiba ya Dola ya Ujerumani kutoka 1871. Majimbo ya awali yalikuwa yakitawaliwa na wafalme (labda kwa mlinganisho, tungeweza kuwalinganisha na watemi, machifu, au watawala wengine wa kiafrika kabla ya ukoloni).

Kwa upande wa Marekani , kwa historia, tena kwa kifupi sana, majimbo 13 ya awali yalipatikana mnamo Julai 1776 wakati wa vita vya Mapinduzi vya Amerika, kama warithi wa Makoloni kumi na tatu, baada ya kukubaliana na Azimio la Lee na kutia saini Azimio la Uhuru la Merika. Kwa maana hiyo, kabla ya uhuru wa Marekani, majimbo husika hapo awali yalikuwa makoloni (kama vile ambavyo Tanganyika, Rwanda na Burundi kwa pamoja (kabla ya vita ya kwanza ya dunia) zilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani kama Deutsch-Ostafrika.

Kwa mifano hii, kama wanaoongelea mfumo wa majimbo wanaiangalia marekani, basi mlinganisho mzuri ungekuwa lile wazo la Gadaffi la kuwa na United States of Afrika , na si kuigawa Tanzania katika vipande vya majimbo. Kwa wanaoangalia mfumo wa majimbo kwa kuiangalia Ujerumani, hali ya sasa ya Tanzania hairuhusu kutengeneza majimbo kwa uzingatia historia ya watawala waliopita.

Uhalisia ni kwamba, si kweli kwamba kila palipokuwa na muundo wa majimbo, basi mambo yalienda sawa. Ipo mifano ya kutosha ya kuthibitisha kwamba hakuna uhusiano kati ya miundo ya serikali/kiutawala (ufalme/serikali za kitaifa/serikali za majimbo) kwa upande mmoja, na  na hali ya maendeleo ya wananchi (huduma bura za afya, elimu, maji, mausha bora, amani n.k.) kwa upande mwingine.

Si kweli kabisa kwamba nchi zote zenye mfumo wa serikali za majimbo au shirikisho zimefanikiwa kutatua matatizo ya wananchi wao kama vile rushwa, umasikini, ukosefu wa ajira na kadhalika. Hii inadhihirisha kwamba matatizo kama rushwa, maradhi, umasikini, ukosefu wa ajira n.k. hayaondolewi na mfumo wa majimbo, mfumo wa jamuhuri au mfumo wa kifalme, bali huondolewa na mipango thabiti ya maendeleo. 


Ndiyo maana, bado matatizo ya umasikini, rushwa, ukabila na udini yapo katika nchi kama Nigeria na Ethiopia, ambazo nazo zina mfumo wa majimbo. Bado pia nchi kama Russia, Venezuela, Pakistan na Somalia (ambazo nazo zina mfumo wa serikali za majimbo) zina matatizo lukuki ambayo baadhi ya wanasiasa wa Tanzania wanaotetea mfumo wa majimbo wanataka kutuaminisha kwamba hayajitokezi katika mfumo huo.

Maendeleo hayachagui mfumo wa serikali, bali huwafuata wanaoainisha kwa ufasaha namna bora ya kutatua changamoto za wananchi. Wakati huohuo, japo zipo nchi kadhaa zisizo na mfumo wa majimbo na zina maendeleo makubwa. Mifano ya nchi hizo ni kama Korea ya Kusini, Finland, Iceland, Singapore na China, japo kwa ufupi.

Hoja ya kwamba tuwe na mfumo wa serikali za majimbo labda tu kwa sababu Ujerumani au Marekani wana serikali za majimbo, haina tofauti na hoja ya kwamba tuwe na mfumo wa kifalme kwa sababu Brunei, Qatar na Kuwait kuna tawala za kifalme na maendeleo makubwa ya kiuchumi. 


Hivyo ni vyema kutofautisha baina ya “siasa za maendeleo” na “siasa za muundo wa kiutawala”. Siasa za maendeleo hujibu swali “ni namna gani kila mwananchi atapata haisha bora, huduma ya maji safi au elimu bora, ”? wakati siasa za muundo wa kiutawala zinajibu swali “Je, nchi yetu iwe katika mfumo wa majimbo / kifalme / kitaifa au la?” Umasikini au utajiri hauna uhusiano wowote na mfumo wa majimbo, kifalme, kitaifa au la.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2