Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MSIMAMIZI wa uchaguzi wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi amewataka wananchi waliojiandikisha kupiga kura kusikiliza Sera za wagombea wanaojinadi hivi sasa na kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Myenzi akizungumza jana amesema wananchi hao wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili wakapige kura siku ya jumatano ya Octoba 28 mwaka huu ili kuwachagua wagombea wanaowapenda wao.
Amesema hivi sasa wagombea wengi wanazungumza sera zao kupitia ilani za uchaguzi hivyo wananchi wajitokeze kwenye mikutano ya hadhara ili kuwasikiliza.
"Siku ya kupiga kura mjitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwachagua wagombea mnaowataka ninyi wenyewe katika ngazi ya urais, ubunge na madiwani," amesema Myenzi.
Hata hivyo, amewataka wananchi wa Simanjiro kuchuja ahadi za wagombea ili kutowachagua wale ambao wanawaahidi mambo ambayo hawawezi kuyatekeleza.
Amesema wao kama wasimamizi wa uchaguzi wa eneo hilo wamejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika bila vikwazo vyovyote.
Mkazi wa kata ya Endiamtu, Sokota Mbuya amesema kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zimeanza na wagombea wa nafasi mbalimbali wameanza kujitokeza kumwaga sera zao.
"Hivi sasa wananchi wana uelewa wa kutosha tofauti na awali hivyo watawachagua wagombea ambao watafanikisha maendeleo na siyo maneno matupu," amesema Mbuya.
Mkazi wa kata ya Mirerani Adam Woiso amesema wananchi wanapaswa kuchuja sera za wagombea kupitia ilani ili wafanye uamuzi sahihi wa kupiga kura siku itakapofika.
Woiso amesema anatambua kuwa wananchi wa Mirerani hawatafanya makosa kwa kuwachagua viongozi ambao hawajaacha alama ya maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi akizungumza na wananchi wa Kata ya Terrat.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment