Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Chato
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano Serikali ya Awamu ya Tano imejenga miundombinu mbalimbali katika sekta ya afya nchini na mpango ulipo sasa ni kuwa na bima ya afya kwa Watanzania wote milioni 62.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita wakati wa mkutano wa kampeni za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kwa nafasi ya urais, Dk.Magufuli amesema katika kuimarisha sekta ya afya jumla ya zahanati 1200 kwa nchi nzima.
Pia tayari vimejengwa vituo vya afya 487 , hospitali za wilaya 98, hospitali za mikoa 10, hospitali za rufaa tatu na zingine zinakuja, hayo yote ni mafanikio.
Amesema katika miaka mitano bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Sh.bilioni 31, hadi Sh,bilioni 270 kwa mwaka.
"Haya sio mambo ya kupuuzwa hata kidogo kwani hata usambazaji dawa kupitia maduka ya MSD yameongezeka,tumefanya hivyo ili kujenga muelekeo mpya wa nchi.Ukitaka kujenga uchumi wowote wa nchi lazima ujenge uchumi wa watu wenye afya njema, huwezi kujenga uchumi wa wananchi wako ambao ni wagonjwa ambao wakienda kutibiwa hawapati dawa,"amesema.
Aidha amesema katika kipindi cha miaka mitano walihakikisha wazee na watoto wanapata matibabu bure na kwa mkakati wa Serikali katika miaka mitano inayokuja watanzania wote wawe na bima ya afya na itakapofika mwishoni mwa mwaka huu Watanzania wa Bara na Visiwani watakuwa wamefikia milioni 62.
"Tuliamua kujikita katika fedha za makusanyo tunayoyapata kwa ajili ya kufanya uwekezaji wa kutosha katika eneo la afya.Tayari tumejenga vituo vingi vya afya na haya ni mafanikio,"amesema na kuongeza hayo yote yanayoendelea kufanyika ni kuitengeneza nchi kuwa ya kisasa, hivyo tupeni tena miaka mitano kuendelea kuleta maendeleo ya Watanzania,"amesema
Akizungumzia hali ya usalama nchini amesema wakati anaingia madarakani wilayani Kibiti kulikuliwa na mauaji na askari polisi 12 waliuawa kwa kupigwa risasi,hivyo walisimama imara kuimarisha ulinzi na usalama.
"Zamani ukitaka kusafiri lazima usindikizwe na Polisi nikasema hapana, majambazi hawawezi kutawala katika nchi hii, navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia hali ya ulinzi nchini kwetu,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza nchi ikikosa usalama hakuna kinachoweza kufanyika.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment