POLISI RUVUMA YAFANYA MAZOEZI YA NGUVU KUJIAANDAA KUKABILINANA NA WAHARIFU WAKATI WA UCHAGUZI MKUU | Tarimo Blog

 Askari wa kikosi cha kuzuia ghasia(FFU)mkoani Ruvuma wakifanya mazoezi maalum wa kukimbia kuzunguka mitaa mbalimbali katika Manispaa ya Songea ikiwa ni kujiweka tayari kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
 Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Kamishina msaidizi Simon Maigwa katikati akifanya mazoezi na baadhi ya askari na maafisa wa Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia jana ikiwa ni kwa ajili ya kujiweka tayari kukabiliana na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi mkuu.


Baadhi ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU mkoani Ruvuma wakiwa katika gari la washawasha baada ya kumaliza mazoezi ya kukimbia umbali wa km 50 kuzunguka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Songea jana ikiwa ni maandalizi ya kukabilianana matukio yoyote ya uharifu katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.Picha na Muhidin Amri.

========= =========  ========  =========

Na Muhidin Amri,Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma,katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali  inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuri, limekamata jumla ya silaha 131 kati ya hizo  SMG 4,Short Gun 12,Gobole 64 na Bastola 3 na Riffle 44.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma kamishina msaidizi wa Polisi  Simon Maigwa amesema hayo jana ofisini kwake mjini Songea, ambapo pia  alitaja silaha nyingine zilizokamatwa ni pamoja na SAR 2,MMG 1 risasi 157 na watuhumiwa 158 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Aidha kamanda Maigwa amesema,mbali na silaha hizo wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya Heroine yenye uzito wa km 1 na gram 787.15 na watuhumiwa 6 wamekamatwa.Pia wamefanikiwa kukamata  bangi kilo 1,675 na gram 279.231,hekari 181 na miche 62,220 ziliteketezwa na watuhumiwa 796 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kamanda Maigwa alitaja mafanikio mengine ni  kukamatwa kwa nyara  mbalimbali za Serikali ikiwemo meno ya Tembo 92,vipande vya nyama ya Tembo 103,mikia 4,mkonga 1 na miguu 2 ya Tembo,nyama  na meno ya kiboko pamoja nyara nyingine za Serikali ambapo jumla ya watuhumiwa 330 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika hatua nyingine,  Kamanda Maigwa amewahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu  kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu.

Alisema, wanaendelea  kufanya mazoezi ili kuwaandaa askari na maafisa wake kuwa na utayari wa kukabiliana na watu au vyama vitakavyotaka kuvuruga uchaguzi mkuu na kuwaonya wale wenye dhamira mbaya kutojaribu  kwa namna yoyote kuvuruga uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.

Alisema  mbali na kuwaandaa askari na maafisa wake,  jeshi hilo limeandaa  vifaa vya kutosha  ikiwemo magari ili kudhibiti vitendo na matukio yoyote yanayoweza kuvuruga uchaguzi huo na kuwataka wananchi kushiriki uchaguzi mkuu kwa Amani na utulivu.

Pia Kamanda Maigwa alisema,  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama  na wadau wa uchaguzi mkoani Ruvuma linaendelea kutola elimu sambamba na kuratibu mabaraza ya Amani ambayo yanajumuisha wagombea,viongozi wa Dini na makundi mbalimbali.

Kamanda Maigwa, amewataka wananchi  katika wilaya zote tano za mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni kwa kusikiliza sera za wagombea na vyama vyao ili wawe na maamuzi sahihi siku ya kupiga kura na kuwachagua viongozi  bora watakao waongoza katika kipindi cha muda wa miaka mitano.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2