Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo ambayo imelenga kusikiliza maoni ya walipakodi, kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati, kusikiliza changamoto walizonazo na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi. Kampeni hiyo itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020. Kushoto ni Meneja wa TRA Mkoa wa Tabora Thomas Masese na kulia ni Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakimuelimisha mfanyabishara wa maeneo ya soko kuu mkoani Tabora wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. Kampeni hiyo itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020.
Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora
NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati ametoa wito kwa wafanyabiashara,wananchi kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu na faini ambayo wanaweza kutozwa kwa wale wanaochelewa.
Alitoa kauli hiyo leo kwenye kikao cha waandishi wa habari na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati akizungumzia kampeni inayoendelea mkoani hapa ya elimu kwa mlipakodi inayojulikana kama mlango kwa mlango.
Dkt. Sengati alisema kuwa kodi ndio inayoiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii ikiwemo kujenga vituo vya afya na kuboresha barabara na madaraja, utoaji elimu bure ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya watumishi wa umma.
Aliwataka wafanyabiashara mkoani Tabora kutoa ushirikiano kwa Maafisa wa TRA watakaopita katika shughuli zao za biashara wakifanya zoezi hilo la kutoa elimu ya kodi.
“Ninawaasa wafanyabiashara na walipakodi wote mkoani hapa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TRA na watumie elimu hiyo kama fursa ya kupata uelewa na kutoa maoni yao kwa ajili ya maboresho ya Sheria za Kodi”, alisema Dkt. Sengati.
Alisema kuwa Mamlaka ya Mapato imeamua kutoa elimu hiyo ili walipakodi wapende kulipa kodi kwa hiari na isionekane wanashinikizwa bali waone ni haki yao kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote ambao watakutwa wakiuza bidhaa zao bila kutoa stakabadhi zinazotolewa kwa njia ya mashine za kieletroniki (EFD).
Naye Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Makao Makuu Diana Masalla alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kusikiliza maoni ya walipakodi kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA na kuongeza walipakodi wapya.
Alisema kuwa wakati wa utoaji elimu hiyo watawakumbusha wananchi kulipa kodi stahiki na kwa wakati, kusikiliza kero na changamoto walizonazo na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi.
Masalla alitaja maeneo ambayo wanakusudia kutembelea katika zoezi hilo la utoaji elimu kwa wafanyabiashara kuwa ni ni pamoja na soko kuu la Manispaa ya Tabora, Nzega mjini Igunga, Choma, Nkinga na Simbo.
Alisema lengo ni kuwafikia wafanyabiashara 3,500 katika kipindi cha wiki moja watakayokuwa wakitoa elimu ya mlipakodi mkoani Tabora.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Makao Makuu Dar es Salaam wakishirikiana na Maafisa wa TRA wa Mkoa wa Tabora wameanza kampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyopewa jina la ‘’Mlango kwa mlango’’.
Kwa Mkoa wa Tabora, Kampeni hiyo imeanza tarehe 14 na itamalizika tarehe 19 Septemba, 2020.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment