Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu, Emmy Hudson akitoa huduma kwa mmoja ya wananchi waliotembelea banda la RITA kupitia jukwaa la 'One Stop Jawabu' lililoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke na kufanyika kwa siku saba katika viwanja Mbagala Zakheem jijini Dar es Salaam.
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) imesajili wananchi 12000 na kuwapa vyeti vya kuzaliwa wananchi 2000 waliojitokeza katika jukwaa la 'One Stop Jawabu' lililoratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Joseph Magufuli la kuwataka wasaidizi wake na taasisi za Umma kutatua kero na changamoto za wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kilele cha jukwaa hilo Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu kutoka RITA, Bi. Emmy Hudson amesema, Wametoa huduma hiyo tangu tarehe 14 mwezi huu na wamefanikiwa kusajili wananchi kumi na mbili elfu na kati ya hao wananchi elfu mbili wamekabidhiwa vyeti vyao vya kuzaliwa.
"Leo ni siku ya mwisho kwa wakazi wa Mbagala Zakheem, kuanzia tarehe 22 tutakuwa katika viwanja vya MwembeYanga Temeke, niwatake wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapate vyeti ya kuzaliwa wasisubiri matukio ndio waanze kufuatilia vyeti hivi ambavyo kwa sasa vinatumika katika huduma mbalimbali ikiwemo kuomba pasi za kusafiria, vitambulisho vya Taifa, kuomba mkopo kwa wanafunzi vya elimu ya juu na huduma za afya" ameeleza.
Pia amesema kuwa, RITA pamoja na taasisi nyingine zimewafuata wananchi ili kutatua changamoto zao, na hiyo ni pamoja na kuwapunguzia gharama wanazotumia katika kufuata huduma hizo.
"Tumesogea katika maeneo ya wananchi ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, zipo taasisi nyingi hapa...Niwatake wananchi wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata elimu na huduma mbalimbali za kijamii" ameeleza.
Vilevile amemshukuru Mkuu w Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe kwa kuratibu mpango huo ambao umeonesha matokeo chanya ambapo kwa muda wa wiki moja pekee wananchi wamepata huduma, elimu pamoja na utatuzi wa changamoto zao.
Jukwaa hilo limehusisha taasisi mbalimbali za Umma zikiwemo RITA, NIDA, TANESCO, BRELA, TRA, LATRA na DAWASA na kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 28 taasisi hizo zitasogeza huduma zao katika viwanja vya MwembeYanga Wilaya ya Temeke.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment