Na Mwandishi wetu
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), imetolea ufafanuzi wa taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya Kijamii juu ya usalama na ubora wa dawa za sindano zenye kiambata hai chenye jina la 'Remdesivir' zinazotumika kutibu ugonjwa wa COVID-19.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMDA kwa vyombo vya Habari mapema leo 18, Septemba imeeleza kuwa hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikihusisha dawa hizo zenye kiambata hai zinajulikana kwa majina ya kibiashara (brand names) kama Covifor.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Covifor inayotengenezwa na kampuni yenye jina Hetero Labs Ltd iliyoko nchini India na Jubi-R inayotengenezwa na Jubilant Generics Ltd, India.
"Dawa hizi za sindano zimefungashwa (packed) kwenye vifungashio ambavyo lebo zake zinaonesha haziruhusiwi kusambazwa kwenye nchi za Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya (Not for distribution in US, Canada and EU).
Maandishi haya kwenye lebo za dawa hizi yameleta taharuki na wasiwasi kwamba inawezekana dawa zinazosambazwa maeneo mengine ya dunia si salama au ni duni (sub-standard) na hazifai kwa matumizi ya binadamu.
TMDA inapenda kutoa ufafanuzi kwamba uandishi wa maneno hayo kwenye lebo za dawa hizo ni wa kawaida kwenye sekta ya dawa na lengo lake ni kuzuia usambazaji wa dawa kwenye nchi ambazo mtengenezaji au mgunduzi wa kwanza (innovator company) hajaruhusu kutokana na kuweka haki miliki (patent) ya dawa yake." Ilieleza taarifa hiyo ya TMDA.
Taarifa hiyo pia ilibainisha kuwq, Dawa hiyo ya Redemsivir imegunduliwa kwa mara ya kwanza na kampuni yenye jina Gilead Ltd iliyoko nchini Marekani na imesajiliwa kwa dharura na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Chakula ya nchini Marekani (US-FDA) kwa ajili ya kutibu COVID-19 (Emergency Use Authorization – EUA).
"Utaratibu huu unatumiwa na US-FDA kwa ajili ya kuidhinisha dawa ambazo tafiti zake (clinical trials) hazijakamilika ipasavyo kabla ya kuruhusiwa rasmi kutumika kwa binadamu ili kuweza kutibu au kuzuia magonjwa yanayoambukiza kwa kasi na kusababisha vifo ikiwa hamna dawa nyingine kama ilivyo kwa magonjwa ya COVID-19, Ebola na mengine.
Kwa mantiki hii, dawa zilizotajwa hapo juu zimetengenezwa na makampuni hayo mawili ya India baada ya kupewa kibali maalum na kampuni ya Gilead Ltd kwa ajili ya kutengeneza dawa za genesi (generic medicines) ili ziweze kutumika kwenye nchi nyingine 127 duniani kwa mujibu wa makubaliano tofauti na nchi za Marekani, Canada na EU" Ilifafanua taarifa hiyo.
Ambapo pia imebainisha kuwa, baada ya haki miliki kuisha muda wake ambao mara nyingi ni kati ya miaka 10 hadi 20 kutegemeana na sheria za haki miliki (Intellectual Property Rights) za nchi husika, makampuni mengine yataanza kutengeneza dawa hii kwa ajili ya kutibu COVID-19.
"Pamoja na ufafanuzi huu, dawa hizo zenye majina Covifor na Jubi-R bado hazijasajiliwa na TMDA kwa ajili ya matumizi hapa nchini.
Hata hivyo kwa taarifa zaidi, wananchi wanaweza wasiliana na TMDA kupitia Ofisi za Makao Makuu au Ofisi za Kanda zilizoko Dodoma, Mwanza, Tabora, Mbeya, Arusha, Mtwara na Dar es Salaam" Ilimalizia taarifa hiyo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment