Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kuimarisha Maadili na Usaidizi kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi (WoLaoTa), Samwel Olesaitabau Lukumay , akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu Uchaguzi Mkuu.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
TAASISI ya Kuimarisha Maadili na Usaidizi kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi (WoLaoTa) imeiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki kwa vyama vyote ili nchi yetu ivuke salama katika Uchaguzi Mkuu utakao fanyika Octoba 28 mwaka huu.
Ombi hilo limetolewa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Samwel Olesaitabau Lukumay wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu Uchaguzi Mkuu.
"NEC kama mlivyofanya kwa chaguzi zilizopita fanyeni hivyo katika uchaguzi huu ili nchi yetu ivuke salama japo hapatakosekana lawama hasa kwa washindwa vitu ambavyo vipo hasa kwenye chaguzi za wale wanaodaiwa kujua demokrasia zaidi." alisema Lukumay.
Alisema nchi nyingi duniani na hasa zile za kiafrika, zimeingia kwenye migogoro hadi watu wao kumwaga damu kwa ajili uchochezi uliyotengenezwa na baadhi ya vyombo vya habari ambapo anaviomba vyombo hivyo hapa nchini kuhakikisha katika kipindi hiki cha kampeni za kuomba kura wagombea na baada ya kutangazwa matokeo vinatenda haki ili kuepusha nchi yetu kuingia kwenye changamoto hiyo na kuwataka watanzania wote tuwe na kauli moja ya kwamba,”AMANI yetu ni zaidi ya siasa”
Lukumay akizungumzia taasisi hiyo alisema inayo nafasi kubwa katika kuimarisha uchumi na hata kuleta mabadiliko chanya katika maandeleo ya nchi yetu kwa kusisitiza kupatikana viongozi wenye ueledi wa kutosha kwenye maeneo mbalimbali ya huduma na inaamini kwamba, wengi wa viongozi wanatokanana vyama vya siasa.
Mtendaji Mkuu huyo wa Taasisi hiyo alitumia nafasi hiyo kwa kuwapongeza wote waliopitishwa na vyama vyao kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo za ugombea Urais kuwa wamepewa thamana hiyo ili kwamba, ushindi wa mmoja wao unakuwa ni ushindi wa watanzania wote, bila kujali itikadi za vyama vyao.
Alisema anauhakika kila lililofanywa na chama cha siasa ni chaguo sahihi na bila shaka wapiga kura wa ngazi mbalimbali watazingatia uadilifu wa kila mgombea ambaye haleti mashaka machoni au masikioni mwa watanzania walio wengi.
" Naamini bila chembe ya shaka, watanzania wataendelea kutuchagulia rais asiye na makandokando na mwenye kuaminisha umma kwamba yeye atakuwa rais wa watu wote na sio rais wa chama fulani.
Niwaombe tena watanzania watuchagulie rais mwenye uchungu na umaskini wetu, mwenye kuchukia rushwa kwa vitendo na asiye kuwa na woga kwa Mabeberu, na asiyeyumba katika maamuzi yake.
Niendelee kuwaomba watanzania watuchagulie wagombea wenye sifa na wenye nia thabiti ya kuleta maendeleo katika nchi yetu na chonde chonde waachane na wagombea wenye kutoa rushwa ili wachaguliwe." alisema Lukumay.
Aidha Lukumay alisema wagombea wa aina hiyo hawana nia yoyote nzuri kwetu sisi watanzania, na hivyo waepukwe na kuogopwa kama ugonjwa wa COVID 19.
" Niwaombe tena watanzania watuchagulie rais mwenye uchungu na umaskini wetu, mwenye kuchukia rushwa kwa vitendo na asiye kuwa na woga kwa Mabeberu, na asiye yumba katika maamuzi yake.
Tupeni viongozi wenye uchungu na umaskini wetu, wenye uchungu na wizi wa rasilimali zetu kama nchi, wenye maadili mazuri na wenye nia ya kuimarisha na kuendeleza mazuri yaliyokwishaanzishwa.
Niwaombe watanzania na hasa vijana wa nchi hii, kuachana na siasa za kishabiki kwani hayata tuletea mafanikio kamwe ndugu zangu watanzania, nakumbukeni kwamba, kura yako moja itatusaidia kutuletea maendeleo ya kweli kwa miaka mitano, lakini tukicheza na hiyo kura moja itatutesa kwa miaka mitano ijayo.
Najua kwa vyovyote kuna watakao au waliotumia fedha na kupenya na kwakuwa hakuna binadamu asiyependa fedha niwaombe kwa anayekuja/aliyekuja kwa gia ya kutoa rushwa pokeeni lakini maamuzi yetu yawe “Tanzania Kwanza”kwenye sanduku la kura.
Niwaombe tena wagombea wote waachane na kampeni za kuchafuana na badala yake kila mmoja atangaze sera ya chama chake kwa ustaarabu ili kuwapa nafasi wapiga kura wao nafasi ya kuchagua chama sahihi cha kuwaongoza watanzania kupitia viongozi waadilifu kwa miaka mitano". alisema Lukumay.
Lukumay alitoa mwito kwa vyama na mashabiki wao ili kuepuka mtifuano na vyombo vya usalama vya nchi na kuwa haitapendeza na wala haina baraka toka kwa Mungu damu ya watanzania ikimwagika kwa ajili tu ya uongozi.
Alisema wote tuamini na kujua kwamba mara nyingi kuna maisha pia baada ya uchaguzi na hivyo hakuna sababu ya kufarakana katika kipindi ambacho kinapita.
"Kama nilivyotangulia kusema, nirudie tena na tena kwamba, wagombea wote ni vyema wakafuata taratibu na maadili ya uchaguzi ambayo walikubaliana kabla ya kampeni kuanza na kamwe wagombea wasiwe ndiyo chanzo cha fujo kwa kuwachokoza vyombo vya usalama ili mwisho wa siku uchaguzi wetu uishe kwa amani. Niwaombe nao vyombo vya usalama kutoegemea upande wowote katika kampeni zinazoendelea na badala yake waonyeshe ukomavu wao kwa kusimamia sheria, kanuni na hata taratibu zote zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi." alisema Lukumay.
Katika hatua nyingine Lukumay ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha haipendelei upande wowote katika kuwabaini watoa au wapokea rushwa kwenye mchakato huu na wakifanya hivyo watakuwa wameepusha kupata Serikali ya wala rushwa.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment