BAKWATA MWANZA, WAMILIKI SHULE ZA KIISLAMU WASAKA MWAROBAINI WA KUKABILI MAJANGA YA MOTO | Tarimo Blog




Mwenyekiti wa Halmshauri Kuu ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza, Shaaban
Moshi, akitoa taarifa ya ukaguzi wa shule za Kiislamu kwa wamiliki wa
shule hizo (hawapo pichani), ukaguzi huo ulifanyika kwenye shule hizo
kubaini changamoto za majanga ya moto na kielimu.

Alhaji Sheikh Hasani Kabeke, wa nne kushoto akifafanua jambo
kuhusina na taarifa ya ukaguzi wa shule za Kiislamu kuhusu majanga ya
moto wakati wa mkutano na wamiliki wa shule hizo uliofanyika Bakwata
mkoani humu .
Wamiliki na waendeshaji wa shule za Kiislamu wakishiriki kuomba dua
baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi ya Bakwata jana zokuhusiana na
majanga ya moto kwenye shule hizo.



NA Baltazar Mashaka, Mwanza

MWAROBAINI wa kukabiliana na majanga na ajali za moto kwenye shule za
Kiislamu umepatikana baada ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) Mkoa wa Mwanza na wamiliki wa shule hizo kukubaliana kuweka
mikakati ya pamoja.

Katika mkutano huo wamiliki wa shule hizo wameiomba serikali kusamehe kodi kwenye vifaa vya kubaini viashiria vya moto, kuzima na kudhibiti majanga ya moto yanapotokea kwenye shule zao.

Uamuzi huo ulifikiwa  baada ya kupokea taarifa ya uongozi wa
BAKWATA ya ukaguzi wa miundombinu ya shule zinazomilikiwa na taasisi
za kiislamu ili kubaini kasoro ama mapungufu kwenye shule hizo
kutokana na kukumbwa na matukio ya majanga ya moto.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA, Shaaban Moshi amesema shule walizotembelea nyingi hazina vifaa vya kubaini viashiria vya moto na
vya kuzima moto na zenye vifaa havikidhi na hakuna vituo vya
kujiokolea, milango ya kuingia na kutoka mabwenini na miundombinu ya
umeme si rafiki inapotokea ajali ya moto ama dharura.

Kwa muktadha huo wamiliki na waendeshaji wa shule hizo wametakiwa
kuboresha miundombinu hiyo lakini pia kupata mafunzo ya kukabiliana na
majanga ya moto yanapotokea.

Aidha  Mkurugenzi wa Islamic Development Founadation (IDF) Juma Chia
amesema silaha pekee ya kukabiliana na majanga ya moto shuleni,
wamiliki na BAKWATA wakutane ili kuweka mikakati thabiti ya kumaliza
tatizo hilo na liundwe jukwaa la wamiliki wa shule za Kiislamu na
wadau wa elimu ambalo litasaidia kukabiliana na majanga hayo na
changamoto za elimu.

“Zipo ajali za moto za hujuma na zingine za uzembe wa kibinadamu,kama
shule yaliyo ndani ni wajibu wetu tuyafanye kwa kuweka vifaa vya
kubaini na kuzima moto, pia ushirikiano wa wataalamu wa Jeshi la
Zimamoto....pia TANESCO watoe elimu kwa walinzi, wanafunzi,walimu na
walezi ili wapate maarifa ya kutambua viashiria vya moto
shuleni,”amesema Nchia.

Pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA) Amina Masenza,ameshauri ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa majanga ya moto ufanyike ukaguzi wa mifumo ya nyaya za umeme kuona kama imeathiriwa pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi.

Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Thaqaafa, Idrisa Haeshi ameshauri kila
shule ianishiwe mapungufu yaliyopo kwenye miundombinu ya
majengo,mifumo ya nishati ya umeme,vifaa na kupewa muda wa kuboresha
ili kuepuka athari za majanga ya moto.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa wa Bodi ya Shule ya Muntazir, Yahya
Lushaka, amesema sababu za kubuka kwa majanga ya moto hazijapatikana kwa usahihi ingawa ajali zingine ni hujuma hivyo zifanyike jitihada za
kudhibiti hali hiyo huku taasisi husika zikijenga uwezo wa kukabiliana
na majanga ya moto shuleni.

Akizungumza baada ya taarifa na kupokea mapendekezo ya wadau hao,
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hasani Kabeke alisema,licha ya
mapungufu wamebaini watumishi wa mamlaka za elimu wanatumia lugha
isiyofaa na kuchelewa kutoa vibali vya uanzishaji wa mabweni na bodi
za shule.

Amesema jambo hilo linahusu mustakabali wa maisha ya Waislamu na watoto
wao hivyo ni muhimu kujenga mshikamano kwa shule za Kiislamu kuondoa
mambo yasiyofaa na wakishikamana watapiga hatua kwa kasi kubwa.

“Tunafurahi baada ya ukaguzi uliofanywa na BAKWATA baadhi ya shule
zimeboresha miundombinu yenye kasoro, hivyo tuendelee kuwa na subira
na watulivu wakati na baada ya majanga ya moto ili kutoa fursa kwa
serikali na vyombo vyake kuchunguza ili mwishowe tupate taarifa sahihi
ya vyanzo vya kadhia hiyo,”amesema Sheikh Kabeke.

Amesisitiza wamiliki kuhakikisha kasoro zilizobainika wazifanyie kazi
haraka ili kunusuru maisha ya watoto na majanga ya moto ambapo BAKWATA
itakuwa ikifanya ukaguzi mara mbili kwa mwaka kwenye taasisi hizo za
elimu zinazomilikiwa na Waislamu.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2