WANANCHI WAZUA GUMZO MAKABURINI, WATAKA UFAFANUZI WA KIFO CHA MAREHEMU | Tarimo Blog

Gideon Stiven Mwautenzi msemaji wa familia akieleza sababu zilizopelekea kifo cha kijana wao Kelvin Fute mara baada ya waombolezaji kuomba sababu za kifo chake.
Insp.Oraity Shomari Muwakilishi wa jeshi la polisi akitoa ufafanuzi kidogo juu ya kifo cha mtuhumiwa waliokuwa wakimshikilia huku akiwaomba wananchi kushirikana katika mazishi ya kijana huyo.

Mmoja wa makamanda kutoka jeshi la polisi mkoa wa Njombe akishiriki kusindikiza mwili wa marehemu Kelvin Fute katika nyumba yake ya milele mara baada ya waombolezaji kuomba washirikiane kutokana taarifa za kifo chake akiwa mikononi mwao.

Wanafamilia na ndugu wa marehemu Kelvin Fute wakiwa nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Njombe hapo jana walipofika wakati wakitoa lawama za kijana wao kufariki akiwa ameshikiliwa na jeshi la polisi.



Na Amiri Kilagalila, Njombe

WAKAZI wa kata ya Mji Mwema katika Halmashauri ya mji wa Njombe,wameibua gumzo Makaburini wakihitaji taarifa ya kifo cha kijana Kelvin Fute (34) mkazi wa kata hiyo aliyekutwa na kifo cha utata wakati akiwa mikononi mwa jeshi la polisi.

Waombolezaji waliofika katika mazishi eneo la Hagafilo walitaka ufafanuzi wa kifo cha kijana huyo ambaye alikuwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuuza msitu usio kuwa mali yake huku wakitaka polisi kushiriki zoezi la kusindikiza kaburini mwili wa kijana huyo.

Kutokana na hali hiyo msemaji wa familia bwana Gideon Stiven Mwautenzi amefafanua sababu za kifo cha kijana wao Kelvin Fute kuwa ni kutokana na mbinu za jeshi la polisi zilizokuwa zikitumiwa na jeshi la polisi katika mahojiano kwa kuwa walibaini katika mwili wa marehemu kuwa na majeraha.

“Mpaka kufikia hapa tumekaa na mkuu wa Wilaya tukiwa na wanafamilia wasiopungua arobaini na kuongea kwa kina baada ya kukubaliana mambo mengi tulikwenda Mochwari kutambua mwili wa marehemu,tulichokiona tulimwambia daktari andika amuawa maana yake alichomwa mgongoni na umeme na alivunjwa mguu”amesema Gideon Stiven Mwautenzi

Mwautenzi aliongeza kuwa “Nilipokuwa kwa mkuu wa wilaya nilisema mdogo wangu sikatai kwenye mambo haya ambayo anahisiwa ninamtambua na ninamjua vilivyo lakini kosa ni kumchukua bila kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa,amekufa bila kutoa taarifa na mmeshinda naye kama masaa 24 hili jambo kama mimi mwanafamilia halikai kabisa akilini mwangu”alisema msemaji wa familia

Kwa upande muwakilishi wa jeshi la polisi Insp.Oraity Shomari,amesema kwa kuwa tayari suala la kifo hicho limefika ngazi ya juu hawezi kuzungumza mambo mengi huku akiomba wananchi waweze kushirikiana katika mazishi hayo.

“Kwa hiyo sisi tumekuja kushiriki katika hili suala la msiba na siwezi kuongeza mambo mengi zaidi,ninaomba tumzike salama na kama kuna mambo mengine ya kisheria yapo yanaendelea.”amesema Insp.Oraity Shomari

Kutokana na ufafanuzi huo ndipo waombolezaji wakaweza kushirikiana na jeshi la polisi katika mazishi ya kijana huyo.

Michael Lugome  mchungaji wa kanisa la Anglican aliyeongoza ibada ya mazishi,ametoa wito kwa vijana na jamii kubadilisha mienendo katika maisha yao huku akiomba jeshi la polisi na viongozi wa serikali kuendelea kuongoza kwa kufuata jamii kwa kufuata sheria hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi ili kulinda amani.

“Yupo ambaye amepewa kazi ya hukumu,ninaomba vyombo vya sheria viweke utaratibu mzuri kuleta amani katika nchi yetu,tuna jambo la uchaguzi mbele yetu tusingependa kusikia kuna watu wanaleta shida na migongano tunaomba sana tusaidiane kutafuta amani,na vijana tunaomba hebu turekebishe hayo mapito yenu.”amesema Michael Lugome.

Marehemu Kelvin Fute mjasiriamali wa mtaa wa Lunyanywi alifariki mnamo tarehe 2 Oktoba 2020 akiwa mikononi mwa jeshi la polisi huku akiwa ameacha mke na watoto wawili. Hata hivyo jeshi la polisi limeshirikiana na waombolezaji katika mazishi ya kijana huyo ikiwa ni pamoja na gharama zinazohusu msiba huo.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2