Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Save The Children limeungana na ulimwengu katika kuadhimisha siku ya Mtoto wa kike ulimwenguni kwa kuwakutanisha watoto wa kike pamoja na wanawake waliofanikiwa katika fani mbalimbali na kujadili changamoto zinazowakabili sambamba na kuzipatia suluhu, huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikielekezwa kwa jamii, Serikali na wadau mbalimbali kushiriki katika kulinda haki za Mtoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Meneja wa Uchechemuzi na Kampeni, Nuria Mshare amesema kuwa maadhimisho hayo yanayokwenda na kauli mbiu ya "Tumuwezeshe Mtoto wa Kike Kujenga Taifa Taifa lenye Usawa" yameenda sambamba na kuhamasisha jamii, Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wa kike wanapata mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na lishe bora ili kujenga taifa bora lenye jamii shupavu.
"Maadhimisho haya yanaenda sambamba na uzinduzi wa ripoti ya kimataifa ya Save The Children inayohudumia nchi 120 duniani na mambo yatakayojadiliwa na kufanyiwa kazi ni pamoja na malengo ya mkutano wa Beijing ambao umeweka mwelekeo wa hatua za usawa wa kijinsia.'' Amesema.
Amesema kuwa ripoti hiyo inaonesha masuala ya ndoa za utotoni katika ukanda wa jangwa la sahara yameongezeka mara mbili zaidi.
"Jukumu la kutokomeza masuala ya ndoa na mimba za utotoni ni la kwetu sote ikihusisha jamii, Serikali na wadau mbalimbali na kubwa zaidi ni kumshirikisha mtoto wa kike katika kufanya maamuzi na sauti zao kusikilizwa" amesema Nuria.
Pia Meneja wa mradi wa Ulinzi kwa mtoto, Haki na Utawala kutoka Save The Children Jesca Ndana, amesema maadhimisho ya siku ya Mtoto wa KIKE ulimwenguni mwaka huu yamekuja na mapendekezo kutoka kwa watoto hao waliohitaji kukaa na wanawake waliofanikiwa ili waweze kujifunza, kuhamasika na kubadilishana uzoefu ili waweze kuyafikia malengo.
"Watoto wa kike waliokutanika hapa watapata nafasi ya kukutana na wanasheria, madaktari, wahandisi na marubani ambao watawaongoza katika maadili katika kufanikisha ndoto zao" amesema.
Pia amesema kuwa katika maadhimisho hayo wataangalia makundi yote ya watoto wakike waliopata elimu na wale wasiopata elimu.
"Elimu ni haki ya msingi kwa watoto wa kike katika kuleta matokeo chanya katika jamii, na ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki hii ya msingi bila changamoto zozote" amesema.
Akiwawakilisha watoto wa kike waliohudhuria maadhimisho hayo Sarafina Frank kutoka shule ya Sekondari Mikocheni, ameiomba Serikali kutambua umuhimu wa mtoto wa kike kwa kuwapa vipaumbele ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu mashuleni ili waweze kufurahia masomo yao.
Pia ameishukuru Save the Children kwa kuwakutanisha watoto kutoka sehemu mbalimbali na kupata wasaa mzuri wakubadilishana mawazo pamoja na kujadili na kupeana mbinu za kutatua changamoto zinazowakabili.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment