Na Said Mwishehe,Michuzi TV
NGOJA nianze na maelezo mafupi sana, tena mafupi haswaaa. Mwanasiasa Zitto Kabwe wakati akiwa kijijini Lupaso mkoani Lindi katika maziko ya Mzee Benjamin Mkapa, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu Tanzania, alisema maneno mabaya dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msingi wa maneno yake ni kuwa nyumbani au kijijini kwa Mzee Mkapa hakuna mvuto, hakuna maendeleo hakuna hata kiwanja cha ndege cha kueleweka na zaidi ya yote hakuna barabara ya lami.
Wapo waliomjibu na wapo waliompuuza, kwa sababu Zitto huyo huyo akishirikiana na wanasiasa wenzake akiwemo Tundu Lissu wamekuwa wakiwaambia Watanzania kuwa Rais Dk. John Magufuli anajipendelea yeye kwa kujenga uwanja wa ndege wa Chato wenye hadhi ya kimataifa.
Hata sasa haijulikani tatizo liko wapi kwa kuwa inafahamika kiwanja cha ndege si kitu cha mtu binafsi wala cha ukoo, laiti angetaka kuwa na kiwanja binafsi basi asingethubutu kukifanya cha kimataifa.
Aidha, kama hiyo haitoshi kuna jambo la ubaguzi wa kikanda na kikabila linajidhihirisha kwa kuwa Chato au Mkoa wa Geita nako kuna Watanzania ambao wanayo haki ya kuwa na kiwanja cha ndege tena kwa kipindi hiki ambacho Serikali imeamua kuwa macho na rasilimali za umma ikiwemo dhahabu.
Vilevile, viwanja vya ndege havikuanza kujengwa Chato pekee vipo katika maeneo mengi ya nchi ikiwemo Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Kagera, Dodoma, Dar es Salaam, Songwe na kwengine kwingi huku kuna maeneo ya kimkakati vipo viwanja vinakarabatiwa na vingine vitajengwa vipya au kuboreshwa.Hata Mkoani Singida Dk.John Magufuli ameahidi kutajengwa uwanja wa ndege , achilia mbali kuboresha viwanja vya Mpanda, Tabora, Mtwara, Musoma na Shinyanga.
Msingi wa hoja yangu hapo juu ni kutaka kuwaeleza Watazania uhalali wa kujengwa kiwanja cha Chato, bila kuingiza ubinafsi wa mtu mmoja mmoja kunasibisha kiwanja hicho na urais wa Dk. John Magufuli.
Ikumbukwe kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa kiwanja hiki ulikuwepo tangu Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete, ambapo kulitakiwa kufunguliwa kwa ushoroba wa utalii Kanda ya Ziwa.
Kuzinduliwa na kutangazwa kwa hifadhi mpya za Burigi-Chato, Ibanda, Rumanyika na Karagwe ambapo mchakato umeshakamilika kwa awamu ya kwanza ili kuwezesha watalii kutua katika Uwanja wa Chato moja kwa moja bila kupitia Dar es Salaam wala Kilimanjaro.
Pili utalii na uwepo wa Kisiwa cha Rubondo katika Ziwa Victoria kunaleta watalii wengi watakaofanya utalii wa uvuvi na kupumzika kwenye visiwa mbalimbali ikiwemo Ukerewe.Nafahamu katika kipindi hiki cha kampeni wapotoshaji ukweli wamekuwa wengi.
Chakushukuru Watanzania wengi wanajua nchi yao inaelekea wapi na nini ambacho Serikali inafanya.Tunaitaka Tanzania mpya, Tanzania yenye kueleweka, Tanzania ambayo ifike wakati dunia ione tumeamua na tunasonga mbele.Tuachane na wanasiasa uchwara wanaoangalia maslahi yao na matumbo yao.Acha niendelee na hoja yangu kuhusu Uwanjwa Ndege wa Chato.
Iko hivi kama hiyo haitoshi, umuhimu wa Uwanja wa ndege wa Chato unaonekana katika masuala ya kitaalamu ya anga kuwa ni uwanja mbadala wa ndege wa Mwanza, ambapo ndege za kimataifa zinapopata hitilafu na kushindwa kutua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza, hawatalazimika kutua Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam au Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) wala kulazimika kwenda nchi jirani ya Uganda katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe.
Suala la tatu kwanini naamini Uwanja wa Ndege wa Chato una faida kwa Watanzania, ni namna ambavyo Dk. Magufuli amerudisha heshima ya wachimbaji wa dhahabu hasa wachimbaji wadogo pamoja na kufungua masoko ya dhahabu katika Kanda ya Ziwa likiwemo soko kubwa la dhahabu la Geita.
Hiki kinaweza kuwa kivutio kwa wafanyabiashara wa dhahabu kutoka nje kuja kununua au kuuza bidhaa hiyo bila kulazimika kupitia mikoa mingine.
Ikumbukwe kwa Tanzania na pengine ukanda huu wa Maziwa makuu ukiondoa Afrika Kusini, ardhi ya Geita ina utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu kuliko mahali pengine popote.
Kwa hiyo hakuna dhambi kuwa na uwanja wa ndege Chato, lazima kuwe na shukurani kwa wananchi wa Chato ambao wanatoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa ili baada ya miaka 30 ijayo, watu kama kina Zitto na Lissu wasihoji kwanini Chato hakukujengwa Uwanja mkubwa wa Ndege.
Wakati mwingine Watanzania tuwe wakweli tuache kumsema vibaya Rais kwa kuwa amefanya mambo mengi ya miundombinu hasa kuimarisha sekta ya anga kwenye mikoa mbali mbali nchi nzima, tujikite kwenye hoja za msingi badala ya kuleta ubaguzi wa kikabila na kikanda.
Naeleza hivyo kutokana na kuwa asilimia kubwa ya watu wanaobeza jitihada hizo ndio hao hao wanaotumia viwanja hivyo kwenda maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi.
Tuchukulie mfano hawa wanasiasa wawili Zitto na Lissu, kwenye mipango ya serikali katika mikoa wanayotoka yaani Kigoma kwa Zitto na Singida kwa Lissu kuna mikakati ya kujengwa na kupanua viwanja vya ndege, lakini hakuna mahali popote wanapopaza sauti ya kulalamika kwanini kwenye mikoa yao kuna viwanja vya ndege.
Naomba nitumie muda wako kidogo kufafanua jambo kidogo, Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano imefanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege.Naomba nitaje kiwanja kimoja baada ya kingine, mahali kilipo na fedha ambayo Serikali ya Rais Magufuli imetumia.
Serikali ya Awamu ya Tano imekamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere ambapo hapo umefanyika utekelezaji wa jengo jipya la abiria ambapo jumla ya Sh.722,458,081,255,75 zimetumika.
Katika Kiwanja cha Ndege ya Kimataifa Kilimanjaro(KIA), Serikali imekamilisha upanuzi wa jengo jipya na ukarabati wa maegesho ya ndege umekamilika .Taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi mshauri kwa ajili ya usanifu wa ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege na viungio zinaendelea ambapo jumla ya Sh.104,387,176.714.24 zimetengwa.
Katika Kiwanja cha Ndege Mwanza na Kiwanja cha ndege Tabora awamu ya kwanza na ya pili ujenzi wa maegesho ya ndege, jengo la mizigo, jengo la kuongozea ndege, kituo cha umeme, maegesho ya magari ,kusimika taa za kuongozea ndege na mfumo wa kuondoa maji ya mvua. Pia ukarabati wa barabara za kutua na kurukia ndege , usimikaji wa taa na mifumo ya kuongoza ndege, hapo Serikali imeweka jumla ya Sh.87,433,285,756.45.
Serikali ya Awamu ya Tano katika kiwanja cha ndege Dodoma imefanya ukarabati wa barabara ya kurukia na kutua ndege, viungio na usimikwaji wa taa za kuongozea ndege, jumla ya Sh.12,954,035,283,44 kimetengwa. Wakati kiwanja cha ndege Songwe utwaaji ardhi kwa wananchi walioathirika na upanuzi wa uwanja wa ndege, ujenzi wa jengo jipya la abiria na kumalizia ujenzi wa maegesho ya ndege kiasi cha Sh.14,870,482,418.86 kimetengwa hapo.
Kiwanja cha ndege cha Bukoba umefanyika utekelezaji wa ujenzi wa jengo la abiria, upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege , ujenzi wa barabara ya viungo, ujenzi wa maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami na ujenzi wa uzio wa usalama na hapo Serikali imetenga Sh.31,900,000,000.00.
Kwa upande wa Uwanja wa Ndege wa Geita umefanyika utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya kurukia na kutua ndege,ujenzi wa barabara za viungo na ujenzi wa maegesho ya ndege ambapo kiasi cha jumla ya Sh.43,239,201,402.00 kimetumika.
Pia kuna kiwanja cha ndege cha Mtwara kazi ambazo zinaendelea ni ukarabati na upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege , ujenzi wa maegesho ya ndege na barabara za viungo, usimikaji taa za kuongoza ndege na ujenzi wa barabara za kuingilia kiwanjani na hapo jumla ya Sh.8,175,679,798.64 zimetumika.
Kuna kiwanja cha ndege Shinyanga fidia imelipwa kwa waliopisha eneo la mradi, mkataba wa kazi za ujenzi na ukarabati umeshasainiwa , utekelezaji unaendelea mwaka 2020/2021 ambapo kiasi cha jumla ya Sh.478,664,489.00 kimepangwa. Katika Kiwanja cha ndege Sumbawanga fidia imeshalipwa kwa wanaopisha mradi eneo la mradi, mkataba wa kazi ya ujenzi na ukarabati umeshasainiwa na utekelezaji unaendelea na hapo Serikali imetenga jumla ya Sh.3,723,940,659.00.
Katika kiwnja cha ndege Kigoma (awamu ya pili, Serikali imeshalipa fidia kwa wanaopisha eneo la mradi, taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi zinaendelea.Kazi iliyopangwa ni ni ujenzi wa barabara za kuruka na kutua ndege , ujenzi wa maegesho ya ndege na barabara za viungo , ujenzi wa jengo la abiria na jengo la kuongozea ndege pamoja na ujenzi wa maegesho ya magari , kiasi cha jumla ya Sh.215,105,663.00 kimetengwa na Serikali.Kumbuka Kigoma ndiko ambako Zitto anatoka na Dk.Magufuli ameamua kuuboresha uwanja huo.Hapo Zitto yuko kimya.
Uwanja wa ndege wa Msalato hapo kuna usanifu wa kina na kuanza maandalizi ya ujenzi , kulipa fidia kwa mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi ambapo jumla ya Sh.3,285,076,635.72 zitatumika.Pia kuna Kiwanja cha Ndege cha Lindi ambapo hapo taratibu za manunuzi ya mkandarasi zimekamilika, ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege , maegesho ya ndege na barabara za viungo kwa kiwango cha lami.
Katika jitihada hizo za Serikali kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege haikuishia hapo kuna kiwanja cha ndege cha Songea ambapo kazi zinazoendelea ni upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, ujenzi wa maegesho ya ndege na barabara za viungo kwa kiwango cha lami pamoja na usimikaji wa taa za kuongozea ndege na hapo jumla ya Sh.5,429,144,136.66 zitatumika.
Kuna kiwanja cha Ndege Musoma , katika uwanja huo taratibu za zinaendelea kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ukarabati na upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, ujenzi wa maegesho ya ndege pamoja na barabara ya viungo kwa kiwango cha lami.
Pia kuna kiwanja cha ndege cha Iringa ambapo taratibu zinaendelea kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ukarabati na uboreshaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege, ujenzi wa maegesho ya ndege na barabara za viungo.
Kwa ujumla Serikali katika kipindi cha miaka mitano katika viwanja hivyo jumla ya fedha ambazo zimetumika na zinaendelea kutumika ni jumla ya Sh.1,066.073,574,212.76.Hakika hizo ni fedha nyingi ambazo Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli imeamua kuzitumia kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa viwanja vyetu vya ndege.
Kwa aina ya wanasiasa wetu hasa wale wa upinzani na wasioitakia mema nchi yetu kazi yao ni kubeza tu na si kubeza mbaya zaidi wamekuwa wapotoshaji wakubwa licha ya kwamba wanajua ukweli na umuhimu wa viwanja hivyo.
Baada ya kuamua kutaja viwanja hivyo na kiasi cha fedha ambacho Serikali imepanga kutumia au imeshaanza kukitumia kufanikisha ujenzi wa viwanja hivyo , nirudie tena sioni dhambi ya aina yoyote kujengwa kwa kiwanja cha ndege mkoani Geita.Kama ambavyo vinajengwa viwanja vya ndege au kuboreshwa kwa viwanja katika mikoa mingine ndio dhana hiyo hiyo ambayo imetumika kwa Geita.
Wanasiasa hasa wale wenye tabia ya kupotosha na kupindisha ukweli kuhusu uwanja wa ndege wa Geita ni vema mkawa wa kweli.Uwanja wa ndege wa Chato ni muhimu na ninyi mnaopotosha mnajua ukweli.Tuache kutafuta kura kwa Watanzania kwa kuwaambia uongo.Watanzania wanaelewa na wanajua umuhimu wa viwanja vya ndege.
Wanajua umuhimu wa kiwanja cha ndege Geita ambacho kipo wilayani Chato.Kina faida kibiashara hasa biashara ya madini ya dhahabu lakini pia kina faida kubwa katika eneo la utalii kama ambavyo nimesema hapo awali.
Kwanini naamini Uwanja wa Ndege Chato umejengwa sehemu sahihi?Hayo ambayo nimeeleza hapo juu ni sehemu ya sababu tena za msingi tu.Tanzania ni yetu sote, ni ya kila mtanzania, hakuna mwenye hati miliki nayo, narudia tena Tanzania ni ya Watanzania, itajengwa na Watanzania na hakuna sababu ya kukaa kimya dhidi ya watu ambao hawaitakii mema nchi yetu.
Naamini Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea na mipango yake ya kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.Halafu nilikuwa sijaweka bayana , katika utalii wa uwanja huo wa Chato mkoani Geita umekuja wakati muafaka kama ambavyo nimeeleza pale mwanzoni.
Takwimu za mwaka 2018/2019 za watalii zinaonesha Kisiwa cha Saa nane watalii kutoka nje walikuwa 609, watalii wa ndani na wa nje wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki walikuwa 14,676 na mapato ambayo yamepatikana kutokana na idadi hiyo ya watalii ni 188,141,691.
Wakati katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo idadi ya watalii ambao wametembelea katika kipindi hicho watalii wa nje ni 467, watalii wa ndani ni 808 na kufanya kuwa na jumla ya watalii 1,275 na kiasi cha mapato ambayo yamepatikana ni 376,209,637.
Maeneo hayo ya utalii ambayo nimeyataja yapo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako ndiko uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita upo.Narudia tena hakuna dhambi yoyote ambayo imefanywa na Serikali kwasababu tu imejenga uwanja wa ndege Geita.
Tunapaswa kufahamu kipindi hiki cha kampeni mengi yatasikika, mengi yatazungumzwa lakini jukumu letu Watanzania kusikiliza,kisha kuchuja na kuchanganua lipi la kuwekwa kichwani na lipi la kupuuza.
Hili la wanaopotosha kuhusu uwanja wa ndege Chato ni wa kuwapuuza na kutosikiliza wanayotamka mana ni upotoshaji wa hali ya juu.Narudia kwa kusema wanapotosha kuhusu uwanja wa ndege Chato ni wa kupuuzwa.
Na Mungu alivyo wa ajabu uwanja huo tayari umeshaleta neema kwa Watanzania, wote tunakumbuka makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga nchini Tanzania hadi nchini Uganda yamefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Chato.Tanzania tutavuna mabilioni ya fedha katika bomba hilo.
Rais Magufuli kwa niaba ya wengine nikuombe endelea kuchapa kazi, endelea kuijenga nchi yetu ya Tanzania.Sina shaka na uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, utashinda , utashinda kwa kishindo na wala usipate tabu na hao ambao wamekuwa wakitumia kipindi hiki cha kampeni kupotosha na kuwagawa Watanzania.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment