MIRADI mikubwa mitatu ya maji katika kata ya Kakola Wilayani Kahama imepatiwa sh. bilioni 18.4 ili kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Kakola, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga mapema hapo jana.
“Serikali ilileta sh. bilioni 18.4 za maji lakini najua kwamba hazitoshi. Kwa hiyo, Serikali yenu itaendelea kuboresha mradi huu wa Kakola kwa sababu hapa Kakola ni mji unaokua kwa kasi,” amesema.
“Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya miradi mikubwa ya Nduku-Busangi na kufanya ukarabati na upanuzi kwenye mradi wa maji Kakola na kwenye mradi wa Msalala ambako Serikali inatekeleza kwa kushirikiana na mgodi wa Bulyanhulu.”
Aliitaja miradi mingine kuwa ni miradi ya maji katika vijiji vya Mwanzimba, Igombe, Mwakuzuka, Izuga, Mhama na Chela ambako sh. bilioni 2.1 zimetolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miradi hiyo.
Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Shinyanga kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli aliwanadi pia wagombea udiwani wa jimbo la Msalala. Mgombea ubunge wa jimbo la Msalala, Bw. Iddi Kassim Iddi amepita bila kupingwa.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, ambaye alipewa nafasi ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Magufuli alisema wachimbaji wadogo wa mgodi wa Bulyanhulu, mkoani Shinyanga, wamesaidia kuongeza pato la Taifa kupitia Serikali ya CCM.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment