MAVUNDE AAHIDI KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI KATA YA CHAHWA, 'TUTAONGEZA SHULE YA MSINGI' | Tarimo Blog

 


Charles James, Michuzi TV.


ACHA kazi iendelee! Ndiyo kauli aliyoitoa leo Mgombea Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini CCM, Anthony Mavunde katika mkutano wa kampeni kata ya Chahwa ambapo ameahidi kumaliza changamoto ya Maji, Umeme na Miundombinu. 


Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile ambaye pia ameshiriki kampeni hizo ambapo amemuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, Mavunde mwenyewe pamoja na mgombea Udiwani, Sospeter Mazengo.


Akizungumza kwenye mkutano huo, Mavunde ameomba ridhaa kwa wananchi hao ya kuwapa kura za kishindo wagombea wote watatu wa CCM ili kazi iliyokwishaanza ya kuwatumikia iendelee kwa miaka mingine mitano.


Amesema kata ya Chahwa inapakana imepakana na Ikulu ya Chamwino jambo ambalo litaongeza fursa kubwa za kimaendeleo kwa wananchi wa eneo hilo hivyo hawana budi kuchagua viongozi ambao watazungumza lugha moja na Rais Dk John Magufuli.


" Mnauona huo ukuta mweupe jirani yenu wenye urefu wa Km 27? Hiyo ni Ikulu ndio anapoishi Rais Magufuli, nitashangaa sana Rais amewaletea Ikulu jirani ambayo inaongeza thamani ya kata yenu halafu mkachague Diwani wa upinzani.


Chahwa hamkuwahi kuwa na Shule za Sekondari chini yangu na Diwani Mazengo zimejengwa mbili, leo mnataka kuchagua Diwani wa ACT? Mkimchagua mimi sitofanya nae kazi hii ni kata ya Ikulu haiwezi kuongozwa na mpinzani, nendeni Oktoba 28 mkamchague Rais Magufuli, Mimi na kwenye udiwani niletee Mazengo ambaye naongea nae lugha moja," Amesema Mavunde.


Amesema anaomba miaka mingine mitano ili aweze kujenga heshima ya Chahwa na kuifanya iwe na hadhi ya kuwa jirani na Ikulu huku akisema changamoto ya Maji kwenye kata hiyo inaenda kumalizika kwani unaletwa mradi wa Sh Milioni 842 ambao utaenda kumalizika changamoto hiyo kata nzima.


" Najua mna shida ya umeme na nafahamu nguzo zimeishia pale Vikonje, tulishaenda na Diwani wenu kwa Meneja wa Tanesco tumekubaliana baada ya muda siyo mrefu kazi itaanza na mtaona nguzo zikisimama na kata yote ikiwaka umeme, sasa tuchague tena ili tuje kusimamia kazi hiyo," Amesema Mavunde.


Amesema anajua changamoto ya sekta ya elimu ambapo kuna shida ya walimu lakini tayari walishaweka maazimio kwenye baraza la madiwani kuwa Ajira zote mpya zitakazotolewa jijini Dodoma zitaelekezwa nje ya mji ambapo maeneo kama Chahwa ndio yanapewa kipaumbele lakini pia ameahidi kuongeza shule nyingine ya Msingi kwenye kata hiyo.


" Nafahamu pia changamoto ya Barabara inayounganisha Mahoma hadi Chahwa lakini tulishaipeleka Tarura na iko kwenye mpango, na Rais alishafika hapa na akazungumza na nyie kuhusu barabara itakayozunguka Ikulu, sasa mwenye uwezo wa kumkumbusha Dk Magufuli ni mimi, na mwenye uwezo wa kunikumbusha mimi ni Diwani Mazengo, mkimchagua huyo wa ACT atampatia wapi Magufuli? Msifanye makosa Oktoba 28," Amesema Mavunde.

 Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini CCM, Anthony Mavunde akizungumza na wananchi wa Kata ya Chahwa jijini Dodoma alipofika kuomba kura za Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, za kwake kama Mbunge na Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Sospeter Mazengo.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Chahwa CCM jijini Dodoma, Sospeter Mazengo akiomba kura kwa wananchi wa kata yake waliojitokeza kusikiliza Sera za chama hicho kwenye mkutano wa mgombea Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2