Charles James, Michuzi TV.
Mgombea Ubunge Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma kupitia CCM, Deo Ndejembi ameendelea na mikutano yake ya kampeni katika ya Membe ambapo amewaomba wananchi wa kata hiyo kumpa kura nyingi mgombea Urais wa chama hicho, Dk John Magufuli hadi wapinzani wakome kugombea nae.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Ndejembi amesema kwa mambo makubwa aliyofanya Dk Magufuli ndani ya miaka mitano yake ya kwanza ni uthibitisho tosha wa namna gani ni kiongozi aliyeletwa na Mungu kuja kuwatumikia watanzania.
Amesema ukiachana na miradi mikubwa ya kimaendeleo ambayo Dk Magufuli na serikali yake wamefanya, uwezo wake jinsi alivyoiongoza Tanzania kupambana na ugonjwa wa Corona ni uthibitisho wa namna ambavyo amejawa maono katika kuwaongoza wananchi wake.
" Nchi zingine duniani huko zinateseka na Corona, lakini Magufuli alisimama kidete akasema hafungii watu ndani badala yake wajikite katika kumuomba na kumtegemea Mungu, Corona ikaondoka na tunaendelea na shughuli zetu kama kawaida ingawa Nchi za wenzetu bado wanateseka," Amesema Ndejembi.
Kata ya Membe inakua kata ya sita kufikiwa na mgombea huyo ambaye ameahidi wananchi hao kuwa endapo watampa ridhaa ya kuwatumikia kwa miaka mitano basi atahakikisha anamaliza changamoto ya Maji, Umeme na Miundombinu.
" Naombeni mnipe ridhaa nina uzoefu na nguvu ya kuweza kupambana na kumaliza changamoto zilizopo jimboni kwetu na zaidi kata hii ya Membe, najua Changamoto zilizopo kwenye afya, miundombinu, umeme na elimu zote hizo naahidi kuzimaliza," Amesema Ndejembi.
Wananchi wa Kata ya Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma wakimsikiliza Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chamwino, Deo Ndejembi alipofanya mkutano wa kuomba kura za wagombea wa Chama cha Mapinduzi akiwemo mgombea Urais, Dk John Magufuli, Yeye mwenywwe na madiwani wa kata zake.
Mgombea Ubunge Jimbo la Chamwino Wilayani Chamwino akicheza ngoma za asili na wananchi wa Kata ya Membe alipofika kufanya kampeni za kuomba kura kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment