. Katibu Tawala wa Wilaya Bw.Andrea Ng’hwani kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Kondoa akizungumza na wakazi wa kata ya Khondomairo wakati wa uzinduzi wa Mnara wa mawasiliano ya simu ya TTCL Corporation.
Katibu Tawala wa Wilaya Kondoa Bw.Andrea Ng’hwani, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba na Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kondoa Rahiya Nasoro pamoja na viongozi wa Kata wakiwa katika picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano katika kata ya Khondomairo.
Wananchi wa kata ya Khondomairo wakisajili laini za simu za TTCL Corporation katika uzinduzi wa mnara wa mawasiliano.
Wananchi wa kata ya Khondomairo wakisajili laini za simu za TTCL Corporation katika uzinduzi wa mnara wa mawasiliano.
Kikundi cha Ngoma ya Kirangi ikitumbuiza katika hafla ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano ya simu ya TTCL Corporation katika Kata ya Khondomairo, Wilaya ya Kondoa, Dodoma
Katibu Tawala wa Wilaya Bw.Andrea Ng’hwani kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Kondoa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation wakizindua mnara wa mawasiliano katika kata ya Khondomairo, Wilayani Kondoa, Dodoma.
====== ========== ============
Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation yatoa fursa ya wananchi kupata huduma ya mawasiliano ya simu baada ya kuzindua mnara wa mawasiliano katika Kata ya Khondamairo Wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Akizindua mnara huo Katibu Tawala wa Wilaya Bw.Andrea Ng’hwani kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo ameishukuru Shirila la Mawasiliano Tanzania kwa kuondoa changamoto ya muda mrefu ya kata hiyo kukosa huduma ya mawasiliano ya simu.
Katibu Tawala wa Wilaya Bw.Andrea Ng’hwani amesema kuwa uwepo huduma ya mawasiliano itaondoa changamoto iliyokuwa inawakuta wakazi wa kata hiyo ya kukosa huduma ya mawasiliano ya simu kwa muda mrefu, hivyo mawasiliano ya simu yataleta tija kwa wananchi sambamba na kufungua milango ya fursa ya ajira na kujiongezea kipato
“mawasiliano haya tuyatumie katika kukuza ajira katika maeneo ambayo tunaishi, sambamba na kuchangamkia fursa ambazo zinatokana na uwepo wa Mtandao huu. Fursa hizo pamoja na Kusajili laini, fursa ya kuwa wakala wa kuuza VOCHA na uwakala wa T.PESA” amesema Katibu Tawala wa Wilaya
Wananchi wa kata hiyo wameshauriwa kutumia uwepo wa mawasiliano ya simu katika kujenga utamaduni wa kutafuta fursa za maendeleo, ikiwa pamoja na kutafuta masoko ya mazao yao.
Aidha, Bw Ng’hwani amewataka wananchi wa kata hiyo kuhakikisha miundombinu ya mnara huo na miundombinu mingine ya Shirika la Mawasiliano Tanzania inalindwa, na kutaka wananchi na viongozi wa Kata kushirikiana pamoja katika kulinda miundombinu hiyo ya mawasiliano.
“Tutakapohujumu miundombinu hii, maana yake Kata hii itakosa mawasiliano ya simu, hivyo kuathiri shughuli za kijamii na maendeleo katika maeneo yetu” amesema Bw.Andrea Ng’hwani.
Katibu Tawala wa Wilaya ametoa wito kwa wale wote watakaohujumu miundombinu ya mawasiliano wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba amesema Shirika linaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupeleka huduma za mawasiliano ya simu maeneo ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano hasa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mipaka ya nchi yetu.
“Kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) tumefanikisha kupeleka mawasiliano ya simu za mkononi kwenye kata zaidi ya 130 nchi nzima zenye vijiji zaidi ya 506. Huku juhudi zikiendelea kukamilisha minara iliyobakia ili kusogeza huduma ya mawasiliano ya simu karibu na wananchi” ameongeza Waziri Kindamba
Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa wananchi wa kata hiyo ya Khondomairo watapata huduma ya kupiga simu, ujumbe mfupi, intaneti na huduma ya miamala ya kifedha kutuma, kupokea na kutoa pesa, kununua muda wa maongezi, huduma za kibenki, kununua umeme, ving’amuzi nk.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu amesisitiza wananchi na viongozi wa kata hiyo kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inalindwa kwani uharibifu wa aina yoyote ule utakuwa na madhara makubwa kwa wananchi ikiwamo kukosa huduma za mawasiliano.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment