VITENGO VYA HABARI VYATAKIWA KUBAINI KERO ZA JAMII KATIKA SEKTA YA MAJI | Tarimo Blog


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba (Kulia) akimkabidhi nyenzo za kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) Bw. Samora Lyakurwa, ambaye ametakiwa kuanza majukumu yake kwa kuhakikisha mtandao wa huduma ya majisafi unaongezwa ili kufika asilimia 100 ya upatikanaji maji kutoka asilimia 88.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza kabla yahajazindua Bodi ya Wakurugenzi wa BUWASA, ambapo amesisitiza Serikali inajenga miradi mikubwa ya maji nchini, na mamlaka za maji zinatakiwa kufanya kazi ya kuongeza mtandao wa huduma hiyo kwa wananchi wote.


Baadhi ya wataalam wa sekta ya maji waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya BUWASA wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu.

Watumishi wa BUWASA nao wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu. Watumishi hao wametakiwa kuongeza kasi katika utendaji kazi, kuwajibika kwa haraka kwa mrejesho kutoka kwa wadau kuhusu huduma ya maji na kubaini fursa zinazojitokeza za kutoa huduma ya maji kama maeneo ya ujenzi wa viwanda, shule na hospitali.
Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Nadhifa Kemikimba katika picha ya pamoja na uongozi wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Guguti (4 kutoka kulia,) pamoja na viongozi na watendaji wa sekta ya maji nchini.



NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi. Nadhifa Kemikimba amezitaka Bodi za Wakurugenzi za Mamlaka za Maji kuvitumia ipasavyo vitengo vya Habari, Masoko na Huduma kwa Wateja ili kuweza kubaini mahitaji ya jamii na changamoto za kufanyia kazi katika sekta ya maji. 

Mhandisi Kemikimba amesema hayo wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) tarehe 9 Oktoba 2020 mjini Bukoba. Bodi hiyo mpya ni ya nane katika kuiongoza Mamlaka hiyo na imeelekezwa kuanza na kazi ya kuongeza mtandao wa majisafi na kufikisha huduma hiyo katika maeneo ya viwanda na makazi ya wananchi. 

Mhandisi Kemikimba amesema zipo changamoto zinazohusu huduma ya maji katika jamii ambazo lazima zifanyiwe kazi mara moja na sio sawa kusubiri viongozi wa kitaifa au mkoa katika kutafuta utatuzi wake wakati mamlaka za maji zipo. 

“Nazitaka mamlaka zote za maji ziwatumie watumishi katika vitengo vya Habari, Masoko na Huduma kwa Wateja kushiriki na kutumia weledi wao kuwasaidia wananchi kufaidi huduma ya majisafi na salama bila kuwa na kero, wataalam wa sekta ya maji wajikite zaidi katika kutoa huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza jamii." Amesema. 

Ameongeza kuwa, lengo la Serikali katika miradi yote ya maji inayotekelezwa nchi nzima ni kutoa huduma bora kabisa ya maji kwa wananchi wote, wanaoishi mijini na vijijini, na ubora wa maji ni jambo la kuzingatia wakati wote kwa afya za wananchi na wateja wa mamlaka za maji. 

Mhandisi. Kemikimba katika hafla hiyo ya uzinduzi amewaelekeza wataalam wote katika sekta ya maji kutoka Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Bodi za Maji za Mabonde na Maabara za Maji kutekeleza kazi kwa pamoja katika kufanikisha huduma bora ya maji kwa Watanzania. 

Uzinduzi wa bodi ya BUWASA umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya maji kutoka serikalini, sekta binafsi, watumishi wa umma waliopo kazini na waliostaafu, viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa na wawakilishi wa AZAKI.







Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2