ELIMU YA MLIPA KODI NYUMBA KWA NYUMBA, MWAROBAINI MIGOGORO YA ARDHI | Tarimo Blog


Kaimu kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara Leonard Msafiri
akiongea na kikosi kazi maalum cha kutoa elimu ya kodi ya pango la Ardhi
nyumba kwa nyumba kabla ya kuingia mitaani kutekeleza zoezi hilo.

Bibi Nyamate Ligima kiongozi wa kikosi kazi maalum cha kutoa elimu ya kodi
nyumba kwa nyumba akimuelimisha Bwn. Zuberi Miraji, mkazi wa mtaa wa
Negamsi Halmashauri ya Mji wa Babati.

Baadhi ya watoa elimu ya mlipa kodi nyumba kwa nyumba kutoka Wizara ya
Ardhi Makao makuu Dodoma kwa kushirikiana na wataalam kutoka ofisi ya
Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu na Ankara za madeni kwa wananchi wa mtaa wa Ngarenaro Halmashauri ya Babati Mji.


Wataalam kutoka Wizara ya Ardhi makao Makuu Dodoma, Halmashauri ya Mji wa Babati na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu kwa Mkazi wa Mtaa wa Mji Mpya katika utoaji elimu ya kodi nyumba kwa nyumba.


Watendaji wa sekta ya Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi makao Makuu Dodoma,
Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara na Halmashauri ya mji wa Babatiwakipita nyumba hadi nyumba katika mtaa wa Negamsi kutoa elimu ya kodi ya pango la Ardhi.


Mchungaji James Chimbalambala (wa pili kulia) akitoa historia ya kiwanja chake kwa wataalam wa sekta ya Ardhi katika mtaa wa Mji Mpya eneo la Kanisani Halmashauri ya Mji wa Babati, wakati wa utekezaji zoezi la elimu ya kodi ya pango la Ardhi nyumba kwa nyumba.

Wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa
Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu nyumba kwa nyumba katika mtaa wa
Negamsi (kwa masista) Halmashauri ya Mji wa Babati. 



Na Eliafile Solla

SIKU ya elimu ya mlipa kodi ya pango la Ardhi imetajwa kuwa mwarobaini katika utatuzi wa migogoro ra ardhi hasa migogoro inayohusiana na mipaka ya viwanja pamoja na ile ya upimaji juu ya upimaji. 

Hayo yamesemwa na Kaimu kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara  Leonardd Msafiri alipokutana na kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ya pango la Ardhi pamoja na masuala mengine yahusuyo sekta ya Ardhi katika Mkoa wa Manyara.

Akizungumza katika utekelezaji wa zoezi hilo la utoaji elimu ya kodi nyumba kwa nyumba, Msafiri amesema Wizara iligatua madaraka kwa maana ya kusogeza huduma karibu na mteja kutoka kuwa na ofisi za Ardhi za kanda ambazo zilikuwa nane (08) nchi nzima na kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa kwenye kila mkoa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Msafiri amesema kwamba, Wizara imepiga hatua kubwa kuanzisha kampeni ya siku ya elimu ya mlipa kodi kwa sababu utoaji elimu nyumba kwa nyumba unawapa fursa ya kukutana na wateja wao moja kwa moja na  kugundua changamoto nyingi na tofauti tofauti wanazokutana nazo wananchi katika maeneo wanayomiliki.

Pia Mkuu wa kitengo cha kodi kutoka Wizara ya Ardhi Makao makuu Dodoma Bwn Denis Masami alisema, jukumu la msingi la wizara ni kupanga na kupima lakini hakuna upangaji wala upimaji utaokuwa na tija kama wananchi watakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kupimiwa na kupangiwa maeneo yao. 

Masami ameongeza kwamba, elimu inayotolewa sasa nyumba kwa nyumba ni fursa nzuri ya kuboresha kumbukumbu za wamiliki kutokana na uhalisia kwamba Wizara imeboresha taratibu nyingi za utoaji hudumu zikiwemo zile za ukadiriaji kodi ya pango la Ardhi na ulipaji ambapo sasa zinafanyika kielektroniki.

Aidha Zuberi Njola mkazi wa Mtaa wa Negamsi katika Halmashauri ya Mji wa Babati, ambaye alifikiwa na watoa huduma katika mji wake alifurahia sana zoezi hilo na kuiomba Wizara kuwafikia wengi zaidi.

"Huu ni mkakati mzuri, tulio wengi hatuzijui haki zetu za msingi hasa kuhusiana na masuala ya Ardhi. Pia migogoro mingi tunaitengeneza wenyewe kwa sababu hatuna uelewa wa mambo. Kutoa elimu nyumba kwa nyumba kama hivi kunaleta faraja kwetu wananchi, tunaiomba Wizara iendeleze mkakati huu kwani tukishirikiana hakutakuwa na migogoro amesema Zuberi’ 

Siku ya elimu ya mlipa kodi ya Ardhi ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi ambapo kila siku ya Ijumaa watendaji wa sekta ya Ardhi kote nchini hupita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kutoa elimu kwa wamiliki wa Ardhi kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta ya Ardhi.





Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2