Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
WANANCHI wa kata ya Mwandege Mkuranga wameiomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuharakisha mradi wa maji ili waondokane na kero ya muda mrefu.
Aidha pia, Wameipongeza Mamlaka hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kero ya maji ndani ya mji wa Mkuranga inaelekea ukingoni.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi katika kikao cha Kata ya Mwandege, Mtendaji wa Kata hiyo Abas Likonda amesema wananchi wa Mwandege wana kiu kubwa ya kupata maji safi ambapo wameikosa kwa muda mrefu.
Amesema, Kata ya Mwandege eneo kubwa sana halipati maji ya Dawasa na wananchi wamekuwa na shauku ya mradi wa maji kwenye maeneo yao.
Mhandisi wa Mkoa wa Kihuduma Dawasa Mkuranga Richard Katwiga amesema kuna mradi wa maji Mkuranga unaendelea ukiwa katika hatua ya ujenzi wa Tenki la Lita Milion 1.5 utakaosambaza maji kwenye mji huo.
Ameeleza kuwa, mbali na tenki hilo wanajenga tenki lingine Kisarawe 2 lenye ujazo wa Lita Milion 13 ambapo litasambaza maji hadi maeneo mengine ya Mkuranga.
Aidha, Katwiga amesema walipokea baadhi ya miradi kutoka kwa Ruwasa na tayari Dawasa wamefanya usanifu kwa maeneo hayo na wataanza kulaza mtandao mpya wa maji kuelekea maeneo mengine ili kutoa huduma ya maji.
Afisa Mahusiano Dawasa Elizabeth Eusebius amewataka wananchi kushirikiana na Dawasa katika kulinda mbinu ya maji pamoja na kulipa bili za maji kwa wakati ili Mamlaka iendelee kujenga miradi na kuwanufaisha wananchi wengine kupata huduma hiyo.
"Wananchi wamekuwa wana changamoto kubwa ya kutokulipa bili kwa wakati na wengine wakiwa wasumbufu kwenye ulipaji, tunawaomba walipe bili zao ili Dawasa waendelee kujenga miradi mingine kwani ni gharama kubwa sana zinatumika kwenye ujenzi," amesema.
Amefafanua kuwa, kwa sasa wanaendelea na bei ya maji waliyoikuta kwenye miradi waliyokabidhiwa ila miradi mikubwa ya maji itakapokamilika watatoa bei elekezi.
Watendaji wa Mamlaka ya Dawasa Mkoa wa Kihuduma Mkuranga wamekutana na viongozi wa Kata ya Mwandege na Vitongoji vyake na kufanya mkutano wa pamoja kusikiliza kero za wananchi kuhusiana na kero za majina kutolea ufafanuzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na mamlaka hiyo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment