Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaadhimisha wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kusogeza huduma karibu zaidi na wateja katika mitaa, kupitia madawati mbalimbali ya kuhudumia Wateja.
Miongoni mwa ofisini za TANESCO zilizowafuata wateja mtaa kwa mtaa ni ofisi ya TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, ambayo imeweka kambi maeneo mbalimbali ya Kinondoni na viunga vyake, ikiwemo kituo cha Daladala Tegeta Nyuki kwa lengo la kufikisha huduma karibu zaidi na Wateja.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Tegeta, Mhandisi Josephat Joseph amesema kuwa TANESCO inawathamini Wateja wake na inatambua watu wengi wako katika harakati za kujitafutia riziki, hivyo wameamua kuwafuata katika maeneo yao ya kazi na sehemu zenye mikusanyiko ya watu kama ilivyo katika eneo hilo ambalo ni stendi ya mabasi ya daladala.
Aliongeza kuwa pamoja na kutoa huduma TANESCO pia inawapatia elimu kuhusu matumizi bora na salama ya umeme pamoja na kutatua kero mbalimbali za wateja.
"Mfano tumekuja na mita za umeme za zamani na za sasa, ili kuwaeleza wananchi kuwa Kama watakuwa na mita za zamani basi wanapaswa kutoa taarifa ili tuwabadilishie mita hizo pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya mita mpya", alisema Mhandisi Josephat.
Aliongeza kuwa, mita zina muda maalum wa matumizi ambayo ni kati ya miaka 10 hadi 20 muda huo ukipita zinaanza kuleta matatizo ya kiufundi kama vile batan kuacha kubonyezeka, tatizo la mita kuzima na kuwaka, mita kutokupokea token.
Aidha, mmoja wa Wateja waliofika kwenye banda hilo la huduma kwa wateja Bw. Job Mpipa mkazi wa Madale amesema kuwa baada ya kumsikiliza maelezo ya wataalamu wa TANESCO amejifunza namna ya kumuokoa mtu aliyenaswa na umeme na jinsi ya kumuongezea pumzi.
"Ili kumuokoa mtu aliyenaswa katika umeme yakupasa utumie kijiti kikavu, pia huruhusiwi kumpa maji ya kunywa kwa maana anakuwa na kiu ya maji lakini kwa wakati huo haupaswi kumpatia maji ya kunywa." Alisema mteja huyo.
Mwananchi mwingine aliyefika kwenye banda la TANESCO, Bi. Lucia Msahara kutoka Boko Magengeni, alisema yeye amevutiwa na namna ya kutumia umeme, kama vile unapochaji simu na baada ya kujaa, unapoiondoa unapaswa kuzima umeme badala ya kuacha umeme ukiwa umewaka.
"pia nimejifunza kuwa, mtu kama amepigwa na shoti ya umeme usimguse kwa mikono kwani unaweza kujikuta na wewe unaathirika kwa shoti hiyo ya umeme" aliongeza Bi. Lucia
Maadhimisho ya Wiki ya Wateja yanafanyika tarehe 5-9 Octoba, 2020 na ni fursa kwa Taasisi zinazotoa huduma kana TANESCO kuwa karibu zaidi na Wateja wake.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment