*Watanzania washauriwa kuendelea kunawa mikono
MKURUGENZI wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa, asilimia 63.7% ya kaya zote nchini Tanzania zimefanikiwa kuwa na vyoo bora kwa mwaka 2020, kutoka asilimia 59 mwaka 2019, huku lengo likiwa ifikapo mwaka 2030 kila mtu Duniani atumie choo bora.
Dkt. Subi amesema hayo leo, wakati akiongea na Waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma ikiwa ni siku ya matumizi ya choo Duniani na wiki ya usafi wa mazingira Tanzania.
"Kaya zenye vyoo bora zimeongezeka kutoka asilimia 59 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 63.7 mwezi Juni, 2020, huku lengo namba 6.2 la dunia la maendeleo endelevu limeweka bayana kila mtu Duniani anatakiwa kutumia choo bora huku likitanabaisha kuwa kufikia mwaka 2030 hakuna atakayejisaidia hovyo katika mazingira yasiyo rasmi". Amesema Dkt. Subi.
Amesema kuwa, Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Zingatia Mahitaji ya Jinsia kwa Usafi wa Mazingira Endelevu” (Gender Consideration a Pillar for sustainable Sanitation and Hygiene), lengo likiwa ni kuongeza uelewa zaidi juu ya umuhimu wa kujenga na kutumia choo bora pamoja na kuweka mazingira safi wakati wote.
Aidha Dkt. Subi amesema kuwa, Mikoa inayoongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya kaya zenye vyoo bora ni pamoja na Dar es Salaam (95.8%), Iringa (77.5%) na Njombe (74.6%), huku akiweka wazi Mikoa yenye hali duni ni pamoja na Kigoma (49.3%), Lindi (49.2%) na Dodoma (46.1%).
"Mikoa inayoongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya kaya zenye vyoo bora ni Dar es Salaam (95.8%), Iringa (77.5%) na Njombe (74.6%). Mikoa yenye hali duni ni Kigoma (49.3%), Lindi (49.2%) na Dodoma (46.1%)" amesema Dkt. Subi.
Mbali na hayo, Dkt. Subi amehimiza Jamii ihakikishe inajenga na kutumia vyoo bora ili kuepuka kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko na kuwataka kujenga tabia ya kunawa mikono pamoja na kuimarisha usafi wa mazingira ngazi ya kaya.
Hata hivyo, Dkt, Subi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatupa kinyesi cha watoto chooni pamoja na kunawa Mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Pia, Dkt. Subi ametoa wito kwa Taasisi, maeneo ya umma, maeneo ya biashara za vyakula zihakikishe uwepo wa vyoo bora pamoja na sehemu maalum za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwa rika zote, huku akisisitiza kila kaya na maeneo yote yahakikishe yanakuwa na vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment