MAJALIWA AANZA KAZI KWA SPIDI YA HAPA KAZI TUU | Tarimo Blog

*Atembelea miradi mikubwa ya maendeleo, aahidi neema zaidi.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

NI siku mbili tuu zimepita tangu Waziri mkuu Kassim Majaliwa aapishwe rasmi na tayari ameanza kazi kwa Kasi kubwa, na leo Novemba 18 ametembelea na kukagua miradi mikubwa ya kimaendeleo ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha ahadi zote zilizohaidiwa kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inakamilika kwa wakati.

Akiwa katika mradi wa stesheni kubwa ya umeme na Karakana ya kutengeneza mabehewa na vichwa vya treni uliopo Kwala Wilayani Kibaha, Majaliwa amesema kuwa mradi huo wa reli wa kimataifa utakamilika na wananchi watafurahia rasilimali za taifa.

"Nilipokuwa natoka Dodoma nilisimama Morogoro kituo cha kati kuona ujenzi wa phase one, nimeambiwa mwezi wa tatu au wa nne hivi maajabu yataanza, safari za Dar Morogoro zitakuwa fupi zaidi....na Desemba mwaka huu watakamilisha  kupanga mataluma kwa kilomita 50, 60 zilizobaki ili viberenge vianze kupita kutoka Dodoma Morogoro na nitakuwa wa kwanza kupanda." Amesema Majaliwa.

Amesema kuwa ni mara ya tano anatembelea mradi huo kwa nyakati tofauti na maendeleo ni makubwa na ahadi zote zilizohaidiwa zitatekelezwa kwa wakati.

"Nimeridhika na kazi hii, fedha zinazotekeleza mradi huu na hata ule wa umeme wa Mwalimu Nyerere ni zetu pia watanzania wameajirikaa..niwahakikishie na kuwataka watanzania kuendelea kuiamini Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli kwa nguvu mliyoionesha Oktoba 28 katika uchaguzi."

Ameeleza kuwa Shirika la Reli nchini (TRC,) limekua  likifanya kazi kwa weledi kama lilivyoaminiwa na Serikali.

"TRC safi sana, mnafanya kazi nzuri na mradi huu unaotekelezwa na kampuni ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki umeendelea kudumisha mahusiano mema baina yetu."Amesema.

Wakati huo huo Waziri Majaliwa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuharakisha mchakato wa maombi ya ekari 4000 zilizoombwa ili wawekezaji waanze kujenga miundombinu ya kiuchumi ikiwemo hoteli na sehemu za biashara kwa kuwa sehemu hiyo ni kituo kikubwa cha reli hiyo ya kisasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC) Masanja Kadogosa amesema kuwa wataendelea kutekeleza miradi muhimu ya kimaendeleo ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi jirani katika kuhakikisha maendeleo yanawafikiwa zaidi.

Kadogosa amesema miradi yote inayosimamiwa na Shirika hilo itatekelezwa kwa wakati ili wananchi waweze kufaidi matunda ambayo Serikali ya awamu ya tano imekua ikiitekeleza usiku na mchana.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia sehemu ya ujenzi wa mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ambapo alishuhudia tukio la uchepushaji wa maji ya mto Rufiji kwenye handaki ili kupisha ujenzi wa tuta kuu la bwawa la kufua umeme mkoani Pwani, leo Novemba 18, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa uchepushaji maji ya mto Rufiji kwenye handaki ili kupisha ujenzi wa tuta kuu la bwawa la kufua umeme mkoani Pwani, leo Novemba 18, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha reli ya kisasa Morogoro, ambapo mpaka Novemba 15, 2020 ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro utakua umefikia asilimia 90, Mkoani Morogoro, leo Novemba 18, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa juu ya maendeleo ya ujenzi wa kituo cha reli ya kisasa, mkoani Morogoro, leo Novemba 18, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha reli ya kisasa, mkoani Morogoro ambapo aliwasisitiza umuhimu wa kutumia fursa ya ujenzi wa mradi huo ili waweze kujiletea maendeleo, leo Novemba 18, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nyumba wa Misri, Dkt. Abdelhamid Hafiz, mara baada ya kuzindua  uchepushaji wa maji ya mto Rufiji kwenye handaki ili kupisha ujenzi wa tuta kuu la bwawa la kufua umeme mkoani Pwani, leo Novemba 18, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2