SERIKALI NA WADAU KUENDELEA KUSHIRIKIANA KULINDA HAKI ZA WATOTO | Tarimo Blog

MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa rai kwa wadau wote wanaotekeleza shughuli za ulinzi na haki za Watoto kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kuhusu sheria, sera na miongozo mbalimbali inayolinda haki za Watoto nchini.

Nchimbi ametoa kauli hiyo katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Muhandisi Paskasi Muragila kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Haki ya Mtoto yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya shule ya Sekondari Mwenge, Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

Amesema kupitia elimu inayotolewa kwa makundi mbalimbali, mifumo iliyowekwa kuhusu ulinzi wa watoto sambamba na sheria zilizotungwa inawezesha Watoto kuwa salama hivyo ni jukumu la wadau wote ikiwemo wazazi, walezi Watoto wenyewe kushiriki kikamilifu katika ulinzi ili waweze kukua salama kwa maslahi mapana ya nchi.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa Watoto wanapata haki zao za msingi ikiwa ni Pamoja na kuwalinda dhidi ya ukatili wa ain azote” amesema.

Amesema jitihada zinazofanywa ni Pamoja na uanzishwaji wa Dawati la jinsia Watoto kupitia jeshi la Polisi nchini ambapo hadi sasa katika Mkoa wa Singida Halmashauri zote 7 zimeshaanzisha madawati hayo, pia kusimamia mifumo ya utoaji wa taarifa za ukatili dhidi ya Watoto na kujenga nyumba salama ili kuwapa hifadhi Watoto walioathiriwa na ukatili.

Ameongeza pia kuwa, Serikali inaendelea na zoezi la kuhamasisha uundwaji wa dawati la ulinzi wa Watoto shuleni kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili.

Wakitoa risala kwa niaba ya Watoto wa mkoa wa Singida Macmillan Marco na Caroline Joseph wameshukuru jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau kwa Pamoja katika kuhakikisha Watoto wanapata haki na ulinzi dhidi ya ukatili kwa kuwasaidia kupata elimu na mahitaji muhimu hasa Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Aidha wameomba Serikali iendelee kuchukua hatua kwa wote wanaohusika na ukatili wa Watoto ikiwemo kupigwa, kubakwa, kudhalilishwa kingono na kutelekezwa kwani vitendo hivyo bado vinaendelea katika jamii hasa ndani ya familia.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “Dunia salama kwa kila mtoto inawezekana; Chukua hatua” ambapo maadhimisho haya nchini yamefanyika katika ngazi ya Mikoa.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2