TBS YATEKETEZA VIPODOZI VYENYE VIAMBATA SUMU JIJINI ARUSHA | Tarimo Blog

Na Pamela Mollel Michuzi Tv,Arusha

Shirika la Viwango Nchini(TBS) limeteketeza vipodozi vyenye viambata sumu vya thamani ya shilingi milioni 125 baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa kushtukiza wenye maghala ya kuhifadhia vipodozi ambayo hayajasajiliwa katika jiji la Arusha

Vipodozi hivyo vilivyopigwa marufuku vimeteketezwa katika dampo kuu la jijini Arusha ambapo mkuu wa kitengo cha uhusiano wa TBS ameeleza gharama za kuteketeza ni shilingi milioni 3.5 ambazo zimelipwa na mmiliki wa vipodozi hivyo

Mkuu wa kitengo Cha Uhusiano kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS)Roida Andusamile alisema kuwa Sheria ya Fedha Na.8 ya mwaka 2019 iliipa mamlaka ya kusimamia usajili wa bidhaa za chakula,vipodozi,maghala ya kuhifadhia chakula na vipodozi pamoja na migahawa na mahoteli jukumu lililokuwa likifanywa hapo awali na iliyokuwa mamlaka ya Dawa Chakula na Vipodozi(TFDA)

Aliongeza kuwa utekelezaji Sheria hiyo ya fedha ulianza rasmi tangu Julai 2019 hivyo kuwalazimu wauzaji wazalishaji na wauzaji wa vipodozi kusajili bidhaa hizo pamoja na maghala ya kuhifadhia

Pia alisema kuwa Shirika linaendelea na ukaguzi huo kwa nchi mzima pamoja na kuwahimiza wazalishaji wa vipodozi kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu zilizopo kwa kusajili bidhaa hizo pamoja na maghala ili kuepuka usumbufu

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo Cha Uthibiti Ubora,Gervas Kaisi TBS  ameita jamii kuwa makini dhidi ya matumizi ya vipodozi  vyenye viambata sumu kwani madhara yake ni makubwa

Alitaja madhara hayo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)ya mwaka 2020 vikitumika kwa muda mrefu vitasababisha magonjwa ya figo ,mapafu,ngozi,macho,mfumo wa fahamu, mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na mfumo wa Kinga ya mwili na kwa upande wa matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ya hydroquinone husababisha magonjwa ya kansa ya ngozi

Picha ikionyesha namna uteketezaji ukiendelea eneo la dampo

Vipodozi vikishushwa kwenye gari mbili Aina ya fuso

Mkuu wa kitengo Cha Uhusiano kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS)Roida Andusamile akizungumza leo na waandishi wa habari katika eneo la dampo lililopo nje kidogo ya jiji la Arusha katika zoezi la kuteketeza vipodozi feki vyenye viambata vya sumu
Mkuu wa kitengo Cha Uthibiti Ubora,Gervas Kaisi TBS akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madhara yanayopatikana endapo vipodozi hivyo vitatumika



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2