Mkuu wa Idara ya Ajira na Kipato kutoka Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania Peter Sidler akielezea namna ambavyo wanafurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo wamekuwa wakiifadhili baada ya kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa misitu na mazingira katika kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Na Said Mwishehe,Iringa
SHIRIKA la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG)na wadau wake kwa kushirikiana na na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa limewezesha uandaaji wa mipango ya usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji na mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Pamoja na hayo Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo imetoa ombi kwa TFCG pamoja na wadau wake waendelee kuiwezesha halmashauri hiyo katika suala la uhifadhi wa misitu ya vijiji kwa kuitenga na kuhuwisha mipango ya usimamizi shirikishi ya vijiji iliyopitwana wakati.
Hayo yameelezwa leo na Mratibu wa Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara ya Mazao ya Misitu Tanzania(CoforEST)Aigen Mwilafi ambaye pia ni Ofisa Misitu Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Wakati akieleza hayo waliwepo wadau mbalimbali wakiwemo TFCG, Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania(MJUMITA),maofisa wanaosimamia mazingira kutoka serikalini, Maofisa wa Ubalozi wa Uswisi ambao ndio wafadhili na wadau wengine wa sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira nchini.
Aidha amesema kuna takribani misitu 11 haijatengwa kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji na kuna mipango ya usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji 45 imepitwa na wakati inahitaji kuhuhishwa.
Hivyo wangependa misitu yote katika vijiji vyao itengwe na kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji na iwe na mipango iliyohuwishwa na kupitishwa katika ngazi zote za kisheria."Tunaomba muendelee kushirkiana nasi katika kutekeleza hayo."
Ametumia nafasi hiyo kueleza TFCG imekuwa ikifanya kazi za uhifadhi kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Kololo tangu mwaka 2007 na kwamba TFCG na MJUMITA kwa kushirikiana na halmashauri iliunda mtandao mitandao ya jamii ya usimamizi wa misitu ya asili minne.
Ameongeza na kuanzisha mpango wa uvunaji wa mazao wa mazao ya misitu wa Wilaya.Pia kuanzisha mitandao mingine mipya katika kata za Mahenge na Nyanzwa na kwamba mwanzoni mwa Machi 2020 timu ya watalaam wa mradi kwa kushirikiana na halmashauri walitembelea vijiji vya Ikula, Mahenge, Mgowelo na Udekwa kwa lengo la kutembelea misitu na kuona kama inakidhi vigezo vya kutekelezwa mradi wa mkaa endelevu na kuzungumza na viongozi wa vijiji husika.
"TFCG na wadau wake kupitia mradi huu ,mpaka sasa imeweza kuwajengea uwezo watalaam 17 kutoka ngazi ya halmashauri na wanne kutoka ngazi ya kata kwa kutoa mafunzo mbalimbali.Kijiji cha Mahenge ambacho ndicho kinatekeleza mradi huu kumefanyika mikutano ya vitongoji kwa ajili ya kuutambulisha mradi.
"Pia kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi, mipango ya usimamizi shirikishi wa misitu ya kijiji na kupitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.Kuna mafunzo yanaendelea ya uzalishaji mkaa endelevu na uzalishaji wa mbao,kwa wazalishaji mkaa na wapasuaji mbao ambao walikuwa wanajishughulisha na shughuli hizo hapa kijijini bila kufuata taratibu,"amesema Mwalifi.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahima Njaidi amesema TFCG na MJUMITA wamedhamiria kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya misitu na mazingira nchini na wanaamini kwa ushirikiano uliopo kati yao na wadau wengine wakiwemo wananchi wa maeneo ambayo miradi inatekekelezwa mafanikio makubwa yatapatikana na kuleta tija kwa umma.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo Said Halfan Muhina amesema wameomba msaada wa kupatiwa mafunzo zaidi ambapo amefafanua licha ya kuelimishwa bado wanaomba waendelee kupatiwa elimu zaidi na kwamba wanamini kile ambacho kitapatikana kitasaidia kuleta maendeleo ya kijiji chao.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment