Wadau wa Sekta ya Uvuvi kutoka maeneo mbalimbali wamekutana kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu nchini.
Akiongea wakati akifungua kikao kazi cha kupitia mpango huo wa kitaifa kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 21, 2020, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi alisema sekta ya uvuvi inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wavuvi wadogo wapatao 202,053 na zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanategemea shughuli zinazohusiana na uvuvi ikiwemo uchakataji na biashara ya samaki na mazao mengine.
Aliongeza kuwa pamoja na hali hiyo bado wananchi wengi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi ni masikini huku akisema kuwa hali hiyo haikubaliki na ni kinyume na maelekezo ya sera na miongozo mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ya nchi yetu ikiwemo Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015.
Bulayi aliendelea kueleza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kutatua changamoto zinazowakabili wavuvi ikiwemo uandaaji wa mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu.
Alisema mwongozo huo umeibua na kutoa njia ambazo zikitumika kikamilifu hali ya kiuchumi na kijamii ya wavuvi wadogo itaboreka kwa kiasi kikubwa huku rasilimali za uvuvi zikiendelea kuvunwa kwa njia endelevu.
“Usimamizi thabiti wa mwongozo huu unaweza kupelekea kuongezeka kwa ajira, kipato, chakula na lishe na hivyo wavuvi wengi kujikwamua katika umasikini uliopitiliza,”alisema Bulayi
“Nichukue fursa hii kulishukuru sana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari na kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu katika muktadha wa chakula na kuondoa umasikini,” aliongez Bulayi
Aidha, alisema pamoja na mwongozo huo kuwa umepangiliwa vizuri, kama utekelezaji wake hautasimamiwa ipasavyo, hautaweza kutoa tija inayotarajiwa na kwa kutambua hilo Wizara iliunda Kikosi Kazi cha Kitaifa mwaka 2018 ili kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Oliver Mkumbo alisema umuhimu wa mpango kazi kwa nchi ya Tanzania uko wazi ukizingatia sekta ya uvuvi inategemewa na watu wengi kwa shughuli mbalimbali za kujipatia kipato na lishe.
“Tunatambua juhudu za Serikali, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazotekeleza mpango huu, tunaipongeza serikali na wadau kwa kuona umuhimu wa mpango huu na ni matumaini yangu utasaidia kuleta maendeleo kwa wavuvi na jamii kwa ujumla,” alisema Mkumbo
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kusimamia mazingira nchini (EMEDO), Elitrudith Lukanga aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa mpango huo na alitoa wito kwa mashirika mengine kuhakikisha wanashiriki vyema katika mchakato wa utekelezaji wa mpango huo.
“Sisi kama sehemu ya wadau wa utekelezaji wa mpango huu tutashiriki kikamilifu katika kuhamasisha wadau mbalimbali hususani Wanawake kuuelewa mpango huu ili uwe sehemu katika shughuli zao za kila siku,” alisema Lukanga.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Emmanuel Bulayi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau walioshiriki warsha ya kupitisha rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijini Dodoma Novemba 21, 2020. Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka TAMISEMI, Dismas Teti, wapili kutoka kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Nazael Madala na watatu kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Stephen Lukanga. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uvuvi, Merisia Sebastian, wapili kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa kikosi Kazi cha Kitaifa, Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu, Alhaj, Yahya Mgawe na watatu kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Oliver Mkumbo.
Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa, Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu, Alhaj, Yahya Mgawe akieleza jambo katika warsha ya kupitisha rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijiji Dodoma Novemba 21, 2020.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi akiongea na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) wakati akifungua warsha ya kupitisha rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijini Dodoma Novemba 21, 2020.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment