Na Tiganya Vincent
WAFANYABIASHARA wa saruji mkoani Tabora wameonywa kutotumia soko huria na uwepo wa upungufu wa bidhaa hiyo kuwaumiza wananchi wanyonge kwa kuongeza bei kwa lengo la kupata faida kubwa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati alifanya ziara ya kukagua maduka ya wauzaji wakubwa na wadogo wa saruji ili kujionea hali ilivyo ya upatikanaji wa saruji.
Alisema wafanyabiashara ni wadau muhimu katika kushirikiana na Serikali kwenye shughuli za maendeleo ni vema wakahakikisha saruji inauzwa kwa bei nafuu ambayo haiwaumizi wananchi na kuwafanya wajisichie Serikali yao.
“Kwa nadharia ya soko huria bidhaa zinapopungua sokoni bei zinapanda…nawataka wafanyabiashara wa sementi wasitumie mazingira hayo ya uhaba wa saruji kutaka kupata ‘super profit’ ambayo inawaumiza wananchi” alisisitiza
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwaonya pia wafanyabiashara wa saruji wa maduka ya rejareja ambao wanauza saruji kwa shilingi 23,000/= hadi 30,000/= kuacha mara moja na kuongeza Serikali itawachukulia hatua watakaokaidi.
Alisema haiwezekani wao wanunue kwa kiwango shilingi 19,000/= na kutaka kuuza kwa kiwango cha shilingi 23,000/= ambao wanaongeza shilingi elfu nne.
Dkt. Sengati alisema kiwango hicho ni kikubwa ukilingana na wauzaji wa jumla ambao wanapata faida ya shilingi 200 kwa mfuko na gharama za kusafirisha mzigo kutoka viwandani ni kubwa ukilinganisha na wao hapa mkoani Tabora.
“Tumebaini wafanyabiashara wa rejareja wanauza saruji kwa shilingi 23,000/= hadi 30,000/= wakati bidhaa hizo amechukulia hapa hapa Tabora na hana gharama kubwa za kusafirisha mizigo…kitendo hicho ni kutaka kutengeneza fedha nyingi kwa kuwaumiza wanyonge… hakikubaliki, serikali haiwezi kuvulimia ,tutawachukulia hatua” alisema.
Dkt. Sengati alisema wafanyabiashara wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuungana na maono na mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao unataka ubora na unafuu wa maisha kwa wananchi.
Mmiliki wa Kampuni ya Vimajo and Sons ambaye ni miongoni wa wanyabishara wakubwa wa Saruji Mkoani Victor Chami alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa yeye anauza mfuko wa kilo 50 kwa shilingi 19,000 baada ya kuwepo kwa uhaba wa saruji kutoka shilingi 18,500 kabla ya tatizo.
Alisema hivi saruji inapatikana kwa shida na wakati mwingine wanalazimika kununua kwa wafanyabiashara wenzao ambao wanaakiba na ndio maana ameongeza kiashi hicho kidogo.
Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa hivi sasa wameamua kununua saruji aina ya Camel baada ya waliyokuwa wakinunua kwa wingi Mkoani Tabora ya Dangote kutopatikana.
Alisema wananunua saruji hiyo kwa gharama ya shilingi 13, 340/= kiwandani Dar salaam na gharama za usafiri ni shilingi 5,000/= na vibarua wa kushusha wanawalipa shilingi 100/= na zinazobaki ndio faida yao.
Chami alisema kutoka na uhitaji mkubwa wa saruji hapa nchini kwa sababu ya miradi mikubwa inayojengwa na Serikali na mahitaji ya wananchi ni vema Seikali ikawabana Wazalishaji wa Saruji ili waongeza uzalishaji na waachane na kupeleka nje ya nchi.
Alisema pindi Serikali itakapokamilisha miradi yake ndio wazalishaji waruhusiwe kupeleka nje ya Tanzania.
Chami alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora kuwa amesikia kilio cha wananachi atauza saruji kwa bei ya awali ya shilingi 18,500/= kama ilivyokuwa kabla ya kuadimika kwa saruji mkoani humo.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuona uwezekano nao kushusha ili wananchi wasiumie.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment