Na.Ashura Mohamed -Longido.
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Pauline Gekul amewataka wafugaji haswa wa Kanda ya Kaskazini, kuhakikisha kuwa wanauza Mifugo yao katika kiwanda Cha Eliya food Overseas Ltd kilichopo wilayani longido mkoani Arusha.
Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea kiwanda hicho na kupokea changamoto kubwa kutoka kwa wawekezaji hao,kuwa wafugaji wengi bado wanapeleka mifugo yao nchi jirani ya kenya kwa madai ya bei kuwa juu kuliko hapa nchini.
Gekul alisema kuwa ni vema wafugaji wakawa wazalendo kwa kuuza mifugo yao kiwandani hapo, kwa kuwa uchakataji wa mazao hayo yanafanyika hapa nchini na faida nyingi zinakuwa kwaajili ya kunuafaisha taifa pamoja na kuingiza fedha za kigeni.
"Wafugaji ifike mahali sasa tuwe wazalendo kwa kuuza mifugo hapa nchini na ifike mahali tujisikie vibaya kunuifaisha watu wengine au Taifa lingine,Mifugo itoke Tanzania iende kunuafaisha Kenya,ichakatwe Kenya faida yote iende huko ndugu zangu hapa hatumuungi mkono, Maana kwa matendo haya kiwanda kinakosa malighafi."alisema Gekul
Aidha alisema changamoto ya wingi wa tozo amelichukua na kuahidi kuwa wizara yake chini ya waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki watakahakikisha kuwa wanaketi na wizara ya fedha kuweza kutengeneza mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji hao.
"Hili la Kodi nimelichukua tutakaa chini mapema sana na kuhakikisha tunatatua changamoto hii na niwaombe wafugaji kiwanda hiki kisikose Malighafi,tutakaa chini na waziri wa fedha na Kamati ya bajeti na kushauriana nao,ili mwekezaji huyu wa Elia Food Overseas Ltd atoe bei nzuri kwa wafugaji na wauze mazao hapa"alisema Gekul.
Naye mkuu wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe alisema kuwa kiwanda hicho Ni mkombozi kwa wafugaji wa mikoa ya Kaskazini na jirani hata kwa nchi kwa kuwa wafugaji wataweza kupata soko la uhakika na kuondokana na ufugaji wa mazao wa mifugo mingi ambayo haina tija.
"Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza tunashukuru serikali kwa kuweza kuwekeza hapa,na kwanza tumepata soko la kisasa la kimataifa la Mifugo lakini leo hii tunashuhudia kiwanda hiki kwa kweli Ni uwekezaji mkubwa Sana ila Sasa Serikali tunaomba iboreshe mazingira ya kibiashara na kuwezesha kiwanda hiki kushindana na nchi kama Kenya, Ethiopia na nyingine katika uzalishaji kwa kuondoa tozo hizi ambazo ni kikwazo kikubwa Sana "alisema Mwaisumbe.
Pia Mkurugenzi wa kiwanda Cha Elia Food Overseas ltd Irthan Virjee alisema kuwa kiwanda hicho kimeanza uzalishaji na Kuna uwezo wa kuchinja mbuzi 2000 kwa siku na ng'ombe 500.
Pia alisema wamejipanga kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri katika bara la Afrika kwa kuhakikisha kuwa wanasafirisha nyama kwa wingi zenye viwango na ubora wa kimataifa.
Dkt.Jumaa Mhina ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido alisema kuwa watumishi wa Serikali ya wilaya hiyo wamefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wawekezaji hao na kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinapatikana na wizara ilipokea jitihada hizo ambazo ni ukombozi mkubwa kwa wafugaji nchini.
"Tunaomba wizara hii iendele kutulea tunataka kufanya mabadiliko makubwa kwenye soko na kuhakikisha kuwa nchi yetu inafanya vizuri kwa mazao haya ya Mifugo haswa nyama,na kuweka nchi yetu katika ramani na kuhakikisha kuwa tunaitendea haki nchi yetu kwa wingi wa mifugo na usafirishaji wa nyama ambayo inazalishwa na kuchakatwa Tanzania."alisema Jumaa.
Ziara ya siku moja ya Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi wiliayani longido ni kutembelea kiwanda hicho kilichopo katika Kijiji cha Eurendeke na Soko la kimataifa la mifugo ambapo pia aliweza kuzungumza na Wafugaji.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment