KAGERA KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA- BYABATO | Tarimo Blog


Muonekano wa Transfoma Mbili zinazozalisha Umeme wa
Megawati 16, ambazo Serikali ipo katika mpango wa Kuzibadilisha na
kununua Transfoma Mbili kubwa ambazo zitakuwa na Uwezo wa Kuzalisha
Megawati 60 kila moja. (Picha Zote na Abdullatif Yunus)
Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato akimsikiliza
Msimamizi wa Kituo cha Kupoza Umeme Kibeta Ndg. Samson Kuboja, wakati
alipofika Kituoni hapo kufahamu utendaji kazi wake.
Naibu Waziri wa Nishati Adv. Stephen Byabato akipewa
ufafanuzi na Msimamizi wa Kituo cha Kupoza Umeme Kibeta Ndg. Samson
Kuboja, namna Kituo kinavyofanya kazi ya Kupokea na kusambaza Umeme
kwa Wateja.
Moja Kati ya Transfoma Mbili zinazozalisha Umeme wa
Megawati 16, ambazo zimefungwa Kituo cha Kibeta, Transfoma Kama hizo
zimefungwa pia Kituo Cha kupoza Umeme Kyaka.


SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati  inaendelea kuboresha Huduma ya
Umeme kwa kununua mitambo mipya zikiwemo Transfoma, pamoja na
kusimamia Ujenzi wa Miradi ya Kufua Umeme ya Rusumo na Kikagati, ili
kuondokana na adha ya kukatika kwa Umeme Mkoani Kagera, sambamba na
kuachana na Umeme wa kununua kutoka Nchi Jirani ya Uganda.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nishati Adv. Stephen Byabato
wakati wa ziara take ya kutembelea na Kukagua Vituo  viwili Vya kupoza
na kusambaza Umeme Vilivyopo Kibeta Manispaa ya Bukoba, na Kyaka
Wilayani Missenyi Mkoani Kagera na Kuridhishwa na Utendaji kazi wa
Vituo hivyo, mapema Desemba 23, 2020.

Akiwa katika Kituo cha kupoza umeme Kibeta, Naibu Waziri wa Nishati
ameshuhudia Mitambo mipya na Kisasa iliyojengwa eneo hilo, yenye uwezo
wa  kuzalisha  na kusambaza Umeme wa kiasi cha Megawati 16 huku
matumizi ya Umeme kwa Wananchi wa Mkoa Kagera kwa Ujumla Ni Megawati
10.2 mpaka 12 kwa Sasa.

Naibu Waziri Byabato amenukuliwa akisema  "..Nimeridhishwa na Utendaji
wa Kituo hiki Cha Kupoza Umeme, kazi yao Ni Nzuri ndio maana tunapata
Umeme wa Uhakika, ukiacha changamoto ndogo ndogo ambazo, husababishwa na Mambo mbalimbali ikiwemo Hali ya hewa." Amesema Byabato.

Aidha Naibu Waziri wa Nishati Adv. Stephen Byabato ameishukuru
Serikali kwa namna ambavyo imeboresha Miundo mbinu madhubuti na ya
Kisasa, ambayo imekuwa na mchango Mkubwa wa kuinua Uchumi wa Mkoa
Kagera kupitia Viwanda na mengineyo. Mhe. Byabato ameongeza kuwa kwa
Sasa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, ipo katika Mpango wa  kununua
Transfoma nyingine mbili kubwa zitakazokuwa na uwezo wa kuzalisha
Umeme  Megawati 60 kila moja, lengo likiwa Ni kwendana na kasi ya
Tanzania ya Viwanda, tunapoingia Uchumi wa Kati.

Naibu Waziri Byabato ameendelea kuwasihi Wananchi kulinda na kutunza
Miundo mbinu ya Umeme, kwa Kuzingatia umuhimu wa Nishati hiyo kwa
Matumizi ya kila siku, pamoja na kutojaribu kuhujumu Vifaa na Miundo
mbinu ya Kuzalisha Umeme kwa kile kinachoitwa kuuza vyuma chakavu,
Jambo ambalo husababisha hasara kubwa kwa Taifa.

Wakati huohuo Naibu Waziri Byabato, ametembelea kituo cha kupoza Umeme
cha Kyaka, ambacho hupokea Umeme huo kutokea Uganda na kuridhishwa na
Utendaji Kazi, na baadae akapata nafasi ya Kusikiliza Wananchi
waliojitokeza kuwasilisha Kero zao sugu, ambazo Baadhi zilipatiwa
majibu palepale na nyingine zikiendelea kutatuliwa.

Hayo yanajiri wakati jitihada za Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa
Rusumo - Ngara, wa Megawati 80 na ule wa Kikagati - Kyerwa Megawati 14
zikiendelea ili kuhakikisha Mkoa Kagera unapata Umeme wake na
kuunganishwa katika Gridi ya Taifa, ili kuondokana na Matumizi ya
Umeme kutoka Uganda kama ilivyo Sasa, ambapo Serikali imekuwa ikitumia
pesa Nyingi kununua Umeme huo kutoka Nchi Jirani.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2