KALEMANI APANIA KUVIWEKA VIJIJI VYOTE NCHINI NURUNI IFIKAPO DESEMBA 2022. | Tarimo Blog

 

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza wakati wa mkutano wake na watumishi  wa TANESCO Mkoa wa Geita na Wilaya zake tarehe 19 mwezi Desemba, 2020 mkoani Geita.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Bw. Raphael Nombo akitoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa , kwa Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani (kushoto kwake) wakati wa mkutano na Watumishi wa TANESCO wa Mkoa wa Geita.

*********************************************

Na Dorina Makaya, Geita,

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, amewataka Watumishi wa Shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) mkoa wa Geita na Wilaya zake pamoja na REA, kufanya kazi kwa kasi, kwa ubunifu na kwa usahihi ili kuhakikisha vijiji vyote nchini vimeunganishwa na umeme ifikapo mwezi Desemba mwaka 2022.

Waziri Kalemani ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa TANESCO Mkoa wa Geita na Wilaya zake tarehe 19 mwezi Desemba, 2020 mkoani Geita.

” Ni kauli mbiu ya Wizara ya Nishati, na ni kauli mbiu yangu kufanya kazi kwa kasi, kwa ubunifu na kwa usahihi na kila mtumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake anapaswa kuifahamu na kuitekeleza kauli mbiu hii” Amesema Dkt. Kalemani.

Waziri Kalemani ameeleza bayana kuwa, ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali yanatimia, kila mtumishi katika sekta ya Nishati, anapaswa kufanya kazi kwa ubunifu na kwa uadilifu mkubwa huku akizingatia huduma nzuri kwa wateja wakati wote wa utendaji kazi.

Waziri Kalemani amesema, ni wakati muafaka kuanzia sasa kwa watumishi wote kuzingatia utoaji wa huduma nzuri kwa wateja, huku ikizingatiwa lugha nzuri na ya ushawishi kwa wateja na kuwafanya watamani kuunganishiwa huduma ya umeme hata kwa wale wenye uwezo mdogo wa kifedha.

Amesisitiza kuwa, kuanzia sasa ni marufuku kwa mteja kulipia nguzo wala “transformer” ili kuunganishiwa umeme, kwani vifaa hivyo ni mali ya shirika la TANESCO. 

Dkt. Kalemani amehoji  kuhusu wateja wote walio ndani ya mita 30 wanaopaswa kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 na kuhoji kuwa, wananchi wa vijijini wanaoishi zaidi ya mita 30 watafikiwaje na huduma hiyo iwapo TANESCO hawatawapelekea nguzo ili na wao wawe ndani ya mita 30 na kustahili kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi elfu 27,000.

Waziri huyo wa Nishati aliyepania kuhakikisha kuwa, vijiji vyote nchini Tanzania vinaunganishiwa huduma ya umeme ifikapo mwezi Desemba mwaka 2022, ameutaka uongozi na watumishi wote wa TANESCO, kuhakikisha wanasogeza nguzo kwa wateja ili waweze kulipia huduma ya umeme kwa shilingi 27,000.

Waziri wa Nishati, Dkt. Kalemani ameelekeza kuwa, ukiondoa maeneo ya katikati ya mji, wateja wanapaswa kusogezewa nguzo hadi mita 30 ili wananchi hao wastahili kulipia umeme wa shilingi 27,000.

Dkt. Kalemani ameelezea kushangazwa kwake na ucheleweshwaji wa wateja kuunganishiwa umeme walio ndani ya mita 30, lakini bado wanacheleweshewa kuunganishiwa umeme kwa madai kwamba hadi wasubiri wapimaji waje wapime ndio wapatiwe namba ya kulipia  (control number ) waweze kulipia ili wapate kuunganishiwa huduma ya umeme. 

Dkt. Kalemani amekemea vikali uchelewashwaji huo na kuweka bayana kuwa, iwapo mteja yumo ndani ya mita 30 hakuna haja ya ucheleweshwaji wa wananchi kuunganishiwa huduma ya umeme kwani iko wazi ya kuwa mteja huyo yumo ndani ya mita 30 na gharama yake ni elfu 27,000 hivyo hakuna sababu ya kumchelewesha mteja huyo kupatiwa gharama za kulipia ili apatiwe huduma hiyo.

“Ni  wajibu wa TANESCO kusogeza nguzo kwa mteja mita 30 ili wateja waweze kulipia huduma ya umeme kwa shilingi 27,000/= “. Amesema Waziri Medard Kalemani.

Ukiondoa maeneo ya katikati ya mji, wateja wote walioko kwenye vijiji pamoja na mitaa, wanapaswa kusogezewa umeme hadi mita 30 ili wananchi hao wastahili kulipia umeme wa shilingi 27,000. 

Akizungumzia kuhusu wateja wote waliolipia kuunganishiwa huduma ya umeme wapatao 3911 katika mkoa wa Geita na wilaya zake, lakini bado hawajaunganishiwa huduma hiyo, Waziri Kalemani  ametoa maelekezo ya wateja hao kuunganishiwa umeme ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa na ifikapo tarehe 18 mwezi Januari wawe wamepatiwa huduma hiyo.

Waziri Kalemani ametoa maelekezo hayo, baada ya kuhakikishiwa na Kaimu Meneja Mwandamizi, TANESCO Kanda ya Ziwa, Ciprian Onyango ya kuwa, vifaa vyote kwa ajili ya kuwaunganishia wateja umeme, vipo na pia baada ya mameneja wa wilaya za Bukombe, Mbogwe, na Nyang’wale kumhakikishia Waziri Kalemani kuwa wakipatiwa vifaa hivyo kwa wakati, watahitaji si zaidi ya mwezi mmoja kukamilisha kazi hiyo ya kuwaunganishia umeme wateja wote ambao tayari wamelipia ili kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita Eng. Joachim Ruweta alimfahamisha Waziri Kalemani kuwa, hadi sasa vijiji ambavyo bado havijaunganishiwa huduma ya umeme katika mkoa wa Geita ni vijiji 112 tu. 

Dkt. Kalemani ameulekeza uongozi wa TANESCO mkoa wa Geita kwa kushirikiana na REA, kuhakikisha kuwa, vijiji hivyo viwe vimeunganishiwa huduma ya umeme ifikapo mwezi Desemba 2021.

Akizungumzia kuhusu suala la ucheleweshaji wa kuwafanyia wateja upimaji (survey), Waziri Kalemani amesema;” kuchelewa kuwafanyia “survey” wateja kunachangia katika kupoteza mapato kwa Serikali kwani kwa kushindwa kuwahudumia wateja mapema, kunapelekea kuchelewesha kupatikana kwa mapato yanayotokana na umeme, lakini pia wateja wakilipia umeme kutaongeza mapato kwa Serikali yanayotokana na kutumia umeme.” Amesema Dkt. Kalemani.

Ili kuondoa changamoto hiyo, Waziri Kalemani amewaelekeza Mameneja wote wa TANESCO kutumia rasilimali walizonazo kuwahudumia watanzania.

Ameelekeza kuwa, Mpimaji ( Surveyor) atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake achukuliwe hatua za kinidhamu.

” kote kwenye mitaa na kwenye vijiji gharama ya kuunganishiwa umeme ni shilingi 27,000 tu. Ni marufuku kwa wateja kulipia nguzo wala Transforma kwani vifaa hivyo ni mali ya shirika la TANESCO” amesisitiza Dkt. Kalemani.

Aidha, Waziri Kalemani, ameitaka idara inayohusika na Utoaji huduma kwa wateja ( Customer care department) kuweka mikakati itakayowezesha kuwafanya wapimaji wa maeneo yanayotakiwa kuunganishwa umeme (Surveyors), Watumishi wanaotakiwa kutoa namba ya malipo ( Employees responsible for provision of control numbers), na Watumishi waliojiriwa kwa mikataba ya vipindi vifupi ( Short Term Employee – STE ) na watumishi walioajiriwa kwa mikataba ya kuanzia miezi 6 (Temporary Employee -TE), kupata elimu ya huduma kwa wateja ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wateja, kwa kasi, kwa ubunifu na kwa usahihi kwani wao hukutana na wateja moja kwa moja, hivyo ni vema tukajenga mahusiano mazuri na wateja, kuwapa ari ya kutamani kupatiwa na kutumia huduma ya umeme, jambo litakalopelekea kuongeza mapato kwa Serikali kutokana na Sekta ya Nishati.

Vilevile, Dkt. Kalemani amekemea vitendo vya rushwa au kuomba pesa yoyote kwa mteja ili apatiwe huduma ya umeme.

” sitarajii kusikia mkiomba rushwa kwa wateja. Rushwa ni adui wa haki. Hakuna kuomba rushwa kwa wateja. Hakuna kuomba “lunch” wala chai kwa wateja wala nauli. Nitakayemsikia na kumthibitisha kufanya hivyo, huyo tutaachana nae na hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake. Ninawasihi watumishi wenzangu, msiombe, wala kupokea rushwa. Fanyeni kazi kwa kujituma na kwa uadilifu” amesema Dkt. Kalemani.

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato, Waziri Medard Kalemani, amewapongeza watumishi wa TANESCO mkoa wa Geita, kwa kuongoza katika ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba mwaka 2020 ambapo waliweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni 8.7.

Aidha, Dkt. Kalemani ameutaka uongozi wa TANESCO kuja na sera ya kuwapa motisha wafanyakazi watakaoongoza katika ukusanyaji wa mapato.

“Kila Wilaya ifunge mapato kwa kushindanishwa. Ifikapo mwisho wa mwaka watumishi watakaofanya vizuri katika kukusanya mapato. Kuhudumia wateja na kufanya kazi kwa uadilifu, wapewe zawadi” amesema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani amesisitiza sana juu ya umuhimu wa kila kiongozi kutambua umuhimu na mchango wa kila mtumishi katika kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake katika Sekta ya Nishati na  malengo mengine ya Kitaifa katika ujumla wake.

” Kila mtumishi anao mchango muhimu katika kufanikisha malengo tuliyojiwekea kiutendaji. Hivyo ni muhimu kutambua na kuheshimu mchango wa kila mtumishi kuanzia yule anayefanya usafi ofisini au katika eneo la kazi, anayeandaa chai, dereva hadi kiongozi wa ngazi ya juu ili kupata mafanikio mazuri katika kazi. Amesema Dkt. Kalemani.

Mkutano huo wa siku moja uliofanyika mkoani Geita, ulilenga kuwafahamu wafanyakazi, kujua changamoto walizonazo na kutoa maelekezo ya kazi. Umewakutanisha pamoja watumishi wa TANESCO mkoa wa Geita na wilaya zake pamoja na wawakilishi wa REA.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2