MO DEWJ NAJUA HUNIJUI KABISA ILA CHONDE CHONDE NISIKILIZE KUHUHU KOCHA | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MOHAMED Dewj 'Mo' najua wewe ndio Mwekezaji wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam. Ndio hivyo na kama sio kweli utaniambia.

Nimesahau hata kukusalimia, habari za leo Bro, natumai uko salama, na maisha yanakwenda. Baada ya salamu hizo naomba nizungumze nawe japo kidogo lakini pamoja na wana Simba wenzako.

Kwanza hongereni kwa kufanikisha ushindi katika mchezo wa awali dhidi ya timu ya Plateue United ya Nigeria na jana mkafanikiwa kulinda ushindi wenu kwa sare ya bila kufungana. Hongera Mo, hongera wana Simba, hongera kwa wachezaji.Hongera kwa kocha na benchi la ufundi kwa kazi nzuri.

Nikiri Mo wewe unifahamu na wala huna sababu ya kunifahamu. Ndio! Unashangaa nini? Yaani inawezekana vipi Bilionea akanijua fukara tena wa aina yangu. Niko choka mbaya, hohe hahe, chakula changu magimbi, mihogo wakati wewe Baga,unafanya mchezo.

Hatukutani sokoni, hatukutani kwenye vikao vikubwa vya matajiri, hata nikienda uwanjani kwenye mechi za timu yako ya Simba nakaa kule juani kwenye mzunguko wakati Bosi Kubwa Mo uko VIP ya wakubwa.Unagonga makofi kwa staili ya kibunge lakini ukiwa uwanjani unaangalia pira biriani la vijana wako.

Kilichonisukuma kuandika hiki ambacho nimeandika ni hivi,nisikilize na nisome kwa utaratibu kwa asilimia 100 nataka kukupongeza Mo kwa uwekezaji ambao umeufanya katika klabu ya Simba. Leo Simba imetulia, Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu mfululizo. Unastahili pongezi.

Umeandika historia pia ya kuipeleka Simba katika mabadiliko ya kimfumo katika kuendesha klabu. Sio kazi ndogo, natambua bado changamoto lakini dhamira yako njema na wana Simba wengine mtafikia mnakokwenda.

Najua mabadiliko ambayo yamefanyika Simba yamekuwa chachu kwa vilabu vingine vya soka. Sio vibaya kuiga jambo zuri, Yanga wameanza safari ya kuelekea kwenye mfumo kama ambao Simba wameufikia.

Naomba nikupongeze tena Mo kwa jinsi ambavyo umekuwa na mapenzi makubwa na Wana Simba wote, nathamini na kutambua jitihada zako katika kuhakikisha Simba tunaendelea kuwa na furaha. Hongera sana sana Mo tajiri kijana Afrika. Hongera Young Bilionea.

Nikupongeze pia kwa jinsi ambavyo umeendelea kuhakikisha Simba inaendelea kuwa bora ndani na nje ya uwanja. Umetumia mamilioni ya fedha kama sio mabilioni kununua wachezaji.

Kiwango cha Konde Boy, Luis Jose Miquissone tunakiona, sitaki kumzungumzia Clatous Chama, Joash Onyango, Jonas Mkude wala Kaka mkubwa John Raphael Bocco. Ndio sitawazungumzia akina Kapombe wala Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ sitamzumzia Saidi Hamis Ndemla wala Hassan Dilunga.

Sitaki kuwazungumzia maana kazi yao tunaiona. Hatuna mashaka na Pascal Wawa, hatuna shaka na Onyango wala Air Manula golini. Kifupi Simba imetimia. Kiwango cha wachezaji kimeenda kutengeneza msemo wa Simba na Pira biariani. Kazi kweli kweli, watangazaji wa Azam nao wana mambo kweli kweli.

Bada ya hayo yoooote hapo juu, Mo naomba nikueleze mambo mawili au matatu ya msingi na ya msingi kwa sababu ya mtazamo wangu. Ni mtazamo wangu mimi lakini naomba uuchukue na kuufanyia kazi.

Moja nakuomba Mo fanya yote Simba SC kwa sasa lakini msibadilishe Kocha, kuna watu wameanza kuleta maneno oooo Kocha  aondoke. Kisa kwanini hampangi Medie Kagere. Ukweli binafsi sioni kosa la Kocha Sven Vandenbroeck.Ni kweli najua uwezo na mchango wa Kagere ndani ya Simba lakini haiwi sababu ya kuanza kumkataa kocha.

Anajua anachokifanya, anaishi na kukaa na wachezaji muda mwingi kuliko sisi mashabiki, wengine tunawaona wachezaji kwa dakika 90 tu za mchezo, halafu anatokea mtu anasema fukuza kocha kisa Kagere amechelewa kuingia uwanjani. Hovyo kabisa. Nimesikia mashabiki wanavyoanza kunyooosha kidole kwa Kocha. Etiiii hooo aondoke, ooooo hatumtaki.

Binafsi natamani kuona Kocha anaachwa aendele na majukumu yake, asiingiliwe na uongozi, asiingiliwe na wanachama, asiingiliwe na mashabiki nikiwemo mimi shabiki magoli.

Magoli ni muhimu sana lakini unapocheza na nani! Mwalimu alikuwa anajua anataka kucheza mchezo wa aina gani kubaki kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele. Wanakuja mashabiki maneno lundooo Mo nakuamini sana, sikiliza kisha tupuuze.

Najua Kocha kuna makubaliano ambayo ameingia na Klabu ya Simba, apimwe kwa yale mliyokubaliana naye, haya ya mashabiki chondechonde tuachianieni huku huku mtaani, ziba macho, ziba masikio. Tunataka kusonga mbele tukiwa wamoja, Tuanze kwa kumlinda Kocha dhidi ya maneno ya mashabiki yenye nia ovu.

Mwisho kabisa kabisa Haji Manara anayo nafasi kubwa, anajua kujenga ushawishi pindi timu yake inapohitaji matokeo chanya. Nadhan aachwe afanye kazi yake ambayo hakika anaimudu vema, Juzi nilikuwa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, tulimuelewa vizuri sana kuliko Babra alivyomuelewa. ‘SIMBA NI KLABU KUBWA, MO NINA IMANI NA WEWE.’

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2