Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetakiwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa vitendo ikiwemo kuboresha mitaala yake ya ufundishaji ili kuwafanya wanafunzi wanaohitimu katika chuo hicho kujiajiri na kuajiri wengine.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Maulilio Kipanyula ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Tekinolojia Dkt. Reonald Akwilapo katika hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wahitimu SUA iliyofanyika Siku ya Alhamisi tarehe 17 Desemba 2020 kwenye ukumbi wa Multipurpose Kampasi ya Edward Moringe.
Prof. Kipanyula amesema kuwa muda muafaka umefika kwa chuo cha SUA kuangalia mitaala inayotumika kufundishia ili iweze kulenga zaidi kwenye kujiajiri.
“Ni wakati muafaka sasa kupunguza idadi ya wahitimu ambao wanamaliza na kuwaza kwenda kutafuta kazi duniani bali mitaala lazima iwawezeshe wahitimu waweze kujitegemea na kuzalisha ajira kujiajiri wenyewe na waaajiri watu wengine ” alisema Prof. Maulilio Kipanyula.
Prof. Kipanyula ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvisaidia vyuo vikuu nchini viweze kuendelea kuzalisha wataalamu ambao wataweza kulisaidia taifa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amesema wanafunzi waliofanya vizuri na kupewa zawadi ni 211 ambao wametoka katika Ndaki na vitivo mbalimbali chuoni hapo ikiwemo wanafunzi bora wa mwaka ambao ni 195 pamoja na Idara sita bora ambazo zimefanya vizuri kwa kuchapisha katika tovuti
Prof. Chibunda amesema Chuo kitaendelea kutoa zawadi kwa wanafunzi wahitimu waliofanya vizuri kila mwaka katika masomo ili kutambua jitihada wanazofanya nwanafunzi hao ikiwa ni motisha ili wengine nao wafanye vizuri zaidi.
Naye mwanafunzi Bw. Iddy Msangi wa mwaka wa pili katika masomo ya sayansi ya kilimo , ambaye alipata tuzo , alisema hiyo ni motisha kwake ya kuendelea kupambana zaidi katika kuongeza bidii kwenye masomo yake.
“Namshukuru mwenyezi Mungu masomo yalikuwa magumu ila ni kwa uwezo wake Mungu nimekuwa miongoni mwa wanafunzi bora wa mwaka niwashauri wanafunzi wenzangu tunapokuwa chuoni tusome kwa bidii zaidi” alisema Idi Msangi
Kwa upande wake mwanafunzi, Upendo Nzaligo, wa mwaka wa pili katika masomo ya Uandaaji na Uwasilishaji wa taarifa ambaye alipata tuzo ya Sh 100,000 , alisema ameipokea kwa mikono miwili na itampatia fursa nzuri kujitangaza na inatamwongezea kuongeza juhudi katika masomo yake.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment