*Wanaume wamekuwa wasiri kutoa taarifa wakati wakiwa wamefanyiwa ukatili
Na Chalila Kibuda, Michuzi TV
KAMANDA wa Polisi mkoa wa Ilala ACP Janeth Magomi amewataka wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoa taarifa kwenye madawati ya kijinsia ili kupatiwa msaada wa kisheria pamoja na hatua zingine za kimahakama kuchukuliwa katika kuweza kukomesha ukatili huo.
Magoni ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipokua akizundua mpango wa utoaji huduma wa msaada wa kisheria ambao unatolewa na Jeshi la Polisi mkoa wa Ilala kwa kushirikiana na Shirika la Friedrich Naumann Foundation for freedom.
Amesema kuwa, wanaume wapo wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili lakini wanashindwa kwenda kuripoti kutokana na mila na desturi zilizopo ndani ya jamii pamoja na mfumo dume ambao unanyima haki katika suala la ukatili wa kijinsia.
"Jeshi la Polisi tumejipanga na tumeweka madawati nchi nzima kwa ajili kupambana na vitendo vya ukaliti, hivyo tunaomba wananchi wanaofanyiwa vitendo vya kikatili wajitokeze kwani tunatenda haki"amesema ACP Magoni.
Amesema kuwa, mwitikio wa wanawake kujitokeza katika kuripoti matukio ya ukatili upo vizuri ila kwa wanaume bado ni changamoto hivyo elimu inahitajika zaidi.
Kwa upande Meneja Mradi wa Shirika hilo, Veni Swai amitaka, jamii kutoa taarifa kwa wakati wanapofanyiwa vitendo vya kikatili wa kijinsia na kuonesha ushirikiano ili wahusika wa vitendo hivyo waweze kuchukuliwa kisheria.
Amesema kuwa, ili kufanikisha katika mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili ni lazima ufanye kazi na ngazi za chini zaidi ili uweze kufikia malengo kwani matatizo au vitendo vingi vya kikatili vinaanzia huko.
Aidha, amesema asasi za kiraia zinazojishughulisha na ukatili wa kijinsia zinatakiwa kugusa ngazi zote endapo kama una muelimisha mtoto shuleni lazima uwaelimishe na wazazi kwani mtoto anaweza kudai haki yake na akaonekana ni jeuri zaidi na kuambulia kipigo.
Katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambapo kilele kilihitimishwa Dec 10, mwaka huu, lakini kwa mkoa wa kipolisi Ilala bado wanaendelea na kampeni hizo kwa kutoa elimu pamoja huduma za upimaji wa macho, kisukari na presha
Aidha zoezi hilo la kutoa huduma mbalimbali katika kukabiliana na kupinga ukatili wa kijinsia limeanza kata ya Chanika ambapo litaendelea kwa siku mbili na kulekea Pugu, Gongolamboto,Segerea, Vingunguti, Buguruni na kuhitimishia kiwalani.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment