UTOAJI CHANJO WAFANIKIWA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 90 | Tarimo Blog


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe akiongea na Waganga wakuu wa Mikoa na Waratibu wa huduma za chanjo nchini wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo nchini unaofanyika jijini Dodoma.

Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa chanjo nchini wakimsikiliza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ambao lengo lake ni kuangalia hatua zipi wamefikia katika kuwafikia watoto.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akiongea na viongozi na waratibu wa chanjo nchini.
Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo ambaye ni mwakilishi kutoka Shirika la Afya Dunia(WHO) Bw.Nasoro Mohamed akitoa salamu kwa niaba ya wadau wa chanjo nchini.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akiongea kwenye mkutano huo.

Na Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewapongeza viongozi na watumishi wa huduma za chanjo ngazi zote nchini kwa  utendaji bora wa utoaji wa chanjo kwa bidii na kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo Tanzania unaofanyika kwenye ukumbi wa Mt. Gasper jijini Dodoma.

"Niwapongeze kwa jitihada zenu na kuifanya nchi kufanikiwa katika utoaji wa huduma za chanjo kwa kuvuka kiwango cha asilimia 90 kilichowekwa kimataifa, hivyo nawataka mkubaliane na kupanga mbinu na mikakati ya kudumisha na kuboresha zaidi viwango vya chanjo nchini".

Hata hivyo katibu Mkuu huyo alisema licha cha kufanikiwa huko Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kudumisha  kiwango cha chanjo nchini na ana uhakika takwimu za mwaka 2020  zitakapotolewa na Shirika la Afya Duniani(WHO)  itafikia asilimia 98 au zaidi.

Licha ya pongezi hizo Prof. Mchembe  amewaagiza viongozi wa afya ngazi za Mikoa na wilaya  kuhakikisha kuwa huduma za chanjo zinapewa kipaumbele  ili usitokee tena mkoa utakaoshindwa kudumisha kiwango kilichofikiwa kwani ili watoto waendelee kuwa na afya njema hakuna budi kuwapa chanjo bora za kuwakinga dhidi ya maradhi.

"Nchi yetu imekuwa na utekelezaji wa mkakati wa Fikia kila Wilaya,Fikia kila mtoto apate chanjo,nawasisitiza waratibu wa huduma za chanjo kuhakikisha kuwa mikoa inayofanya vibaya inatumia mkakati huu ili  kuhakikisha kuwa watoto na walengwa wote wanafikiwa katika kupata haki yao ya msingi ya chanjo".

Aidha, Prof. Mchembe aliwashukuru wadau wote wa maendeleo kwa michango yao mbalimbali  katika kuhakikisha kwamba watoto  wanapatiwa chanjo bora  ambayo inaleta kinga dhidi ya maradhi ambayo yanaweza kusababisha ulemevu na vifo kwa watoto.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI  Dkt. Ntuli kapologwe amewapongeza Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na waratibu wa huduma za chanjo nchini kwa kuwa kinara wa utoaji wa chanjo na kuweza kuwafikia walengwa wote nchini na kuongoze kuwa TAMISEMI inaipa uzito mkubwa suala la chanjo kwani kinga ya mtoto inaanza na chanjo.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni  Mkurugenzi wa Idara ya kinga Kutoka Wizara ya afya, Dkt. leonard Subi amesisitiza kuwa wizara ya afya inasimamia ubora na usalama wa huduma wanazozitoa hasa upande wa chanjo ambao mara kadhaa umekua na mapokeo tofauti,hivyo amesisitiza kuwa wizara ipo makini zaidi na afya za wananchi

Wakati huo huo Mwakilishi wa wadau wa maendeleo ambaye anatoka WHO Nassoro Mohamed  ameipongeza Wizara ya afya pamoja na viongozi wa mikoa kwa kuhakikisha watoto wote nchini wanafikiwa  licha ya changamoto za hapa na pale hivyo kama wadau wanashiriki ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo waliyojiwekea katika kutoa huduma za chanjo.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2