*Awataka Watanzania wamuenzi kwa kuuishi utumishi wake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Baba Askofu Anthony Mathias Banzi kwa kuuishi utumishi wake uliogubikwa na upole na unyenyekevu aliowaonesha wakati wa kipindi cha uchungaji wake.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Desemba 29, 2020) kwenye mazishi ya
Askofu Banzi yaliyofanyika ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa
Padua, Jimbo Katoliki la Tanga. Waziri Mkuu ameshiriki mazishi hayo
kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Ibada ya mazishi
imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Askofu Titus
Mdoe.
Waziri Mkuu amesema katika maisha na utume wake wa kufundisha,
kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Askofu Banzi alitoa
kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kijamii zikiwemo za elimu,
afya na maji. Askofu Banzi alifariki dunia Jumapili, Desemba 20, 2020
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alikokuwa
akipatiwa matibabu.
“Leo hii tunapomsindikiza Baba Askofu Anthony Banzi tunajivunia
mchango wake mkubwa katika kupigania amani, maelewano na mtangamano wa jamii kwa lengo la kujenga umoja, upendo na mshikamano wa Kitanzania.
Sisi upande wa Serikali tutamkumbuka sana.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia, ndugu na
jamaa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na waamini wote wa
kikatoliki nchini. “Tumuombee kwa Mwenyezi Mungu azipokee kazi zake za
kiuchungaji alizozifanya katika kipindi cha uhai wake na ampumzishe
kwa amani.”
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,
Ummy Mwalimu amesema kuwa wanawake wa Mkoa wa Tanga wamempoteza baba mwema na mlezi ambaye alipenda kuwashauri na kuwaunganisha kama watoto wake kwa kutumia kaulimbiu yake ya hekima, umoja na amani
“Mimi ni mmoja wa wanufaika wa upendo, wema na hekima za baba Askofu,
licha ya kuwa mimi sio Mkatoliki lakini baba Askofu Banzi amekuwa
akinikaribisha nyumbani kwake na kunipa baraka zake na kuniombea kwa
sababu yeye anaamini watu wote ni wamoja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amesema Baba
askofu Banzi alikuwa ni kiongozi mnyenyekevu, muadilifu na mpenda
maendeleo aliyependa kuuona mkoa wa Tanga unapiga hatua.
Akisoma wasifu wa marehemu Askofu Banzi, Padri Richard Kimbwi alisema
alizaliwa Oktoba 28, 1946 katika Parokia ya Tawa, Jimbo Katoliki la
Morogoro, ambapo baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, Julai
29, 1973 alipewa daraja takatifu la upadre, Jimbo Katoliki la
Morogoro.
Alisema kuwa Mwaka 1976 aliteulia kuwa Msarifu wa Seminari kuu ya
Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na mwaka 1976 hadi mwaka 1981
alipelekwa nchini Austria kwa masomo ya juu na kufanikiwa kutunukiwa
Shahada ya Uzamivu katika Falsafa. Mwaka 1981 hadi mwaka 1982
aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mandera na mhudumu wa maisha
kiroho kwenye Hospitali ya Turiani, Jimbo Katoliki la Morogoro.
Aidha, mwaka 1981 hadi mwaka 1985 aliteuliwa kuwa Mhasibu wa Jimbo
Katoliki la Morogoro na kati ya Mwaka 1985 hadi mwaka 1987 alikuwa ni
Padre wa kiroho, Sekondari ya Masista Bigwa, Morogoro. Kati ya Mwaka
1988 hadi mwaka 1991 alikuwa mwalimu na mlezi, Seminari kuu ya
Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na baadaye akateuliwa kuwa Gambera.
Mwaka 1992 hadi mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Gambera wa Seminari kuu ya
Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi na ilipofika tarehe 10 Juni 1994,
Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki
Tanga na kuwekwa wakfu tarehe 15 Septemba 1994 na Kardinali Polycarp
Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Alisema Askofu Banzi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74 ya
kuzaliwa, miaka 47 ya Daraja Takatifu la Upadre na miaka 26 ya
Uaskofu, Utume ambao aliufanya kwa uaminifu mkubwa katika kuwaongoza,
kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo
Katoliki la Tanga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment