Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na wakazi wa Shirati
wilayani Rorya wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji wilayani
humo.
Wakazi wa Shirati wilayani Rorya wakimsikiliza Waziri wa Maji,
Jumaa Aweso (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya
maji wilayani humo.
Eneo la chanzo cha maji mradi wa Shirati ambao umesimama kutoa
maji tangu mwaka 2016
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga akizungumza mbele ya Waziri
wa Maji, Jumaa Aweso wakati wa ziara kwenye mradi wa maji wa Shirati.
Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege akimkaribisha Waziri wa
Maji, Jumaa Aweso kuzungumza na wakazi wa Shirati (hawapo pichani)
Na Mohamed Saif, Rorya
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ametoa siku 30 kwa Mamlaka ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuhakikisha wananchi wa Mji wa
Shirati wanapata huduma ya maji.
Ametoa maelekezo hayo Januari 6, 2021 Wilayani Rorya alipotembelea
mradi huo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege
na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga ili kujionea hali halisi
sambamba na kuzungumza na wanufaika.
Ilielezwa kwamba mradi ulisimama kutoa maji tangu mwaka 2016 baada ya
mtambo wa kusukuma maji kuharibika na kwamba hadi hivi sasa hakuna
hatua iliyochukuliwa.
Hata hivyo, Waziri Aweso alibainisha kwamba alikwishatoa maelekezo kwa
MUWASA kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika ili mradi wa Shirati
uanze kazi.
Alimpigia simu Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru mbele ya
msafara alioambatana nao ili kupata mrejesho wa tathmini ya gharama ya
uhuishaji wa mradi ambapo alielezwa kuwa kiasi cha shilingi milioni
247 kinahitajika ili uweze kutoa maji.
Mara baada ya kuzungumza na CPA Msiru, Waziri Aweso alihoji kiasi cha
fedha kilichopo kwenye akaunti ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa
Mazingira (RUWASA) Wilayani Rorya.
“RUWASA Rorya tueleze ulipokea shilingi ngapi kutekeleza miradi kwenye
eneo lako na hadi hivi sasa kuna kiasi gani kwenye akaunti,” alihoji
Waziri Aweso.
Akijibu swali hilo la Waziri Aweso, Meneja wa RUWASA wilayani Rorya,
Mhandisi Evaristo Mgaya alisema kwamba alipokea kiasi cha shilingi
bilioni 1.3 na kwamba hadi hivi sasa kiasi kilichopo kwenye akaunti ya
RUWASA Rorya ni shilingi milioni 290.
Suala hilo lilimshangaza na lilimkera Waziri Aweso na hivyo alielekeza
fedha hiyo badala ya kuendelea kukaa benki itumike kufanya ukarabati
wa mradi wa Shirati na kwamba fedha nyingine italetwa.
“Inashangaza sana unayo fedha kwenye akaunti halafu watoto wanalala
njaa hii haijakaa sawa hata kidogo; wananchi hapa kipindi chote hiki
wanateseka hawana maji halafu fedha ipo tu benki imekaa haitumiki kama
ilivyokusudiwa,” alisema Waziri Aweso.
Aliongeza, “hili eneo lipo chini yako wananchi hapa wana shida ya maji
lakini wewe unakaa na fedha na haitumiki kwa shughuli iliyokusudiwa
maana yake ni kwamba majukumu haya uliyopewa yamekushinda,” Waziri
Aweso alimueleza Mhandisi Mgaya.
Mara baada ya mahojiano na Mhandisi Mgaya, Waziri Aweso akiwa hapohapo
kwenye eneo la mradi alimpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga na kumuelekeza fedha zilizopo kwenye akaunti ya
RUWASA Rorya zitumike kutekeleza mradi wa Shirati.
“Wape maelekezo kwamba hizo fedha milioni 290 zitumike na kama kuna
maeneo mengine ambayo inahitajika fedha utawaletea lakini hizi
zisiendelee kukaa kwenye akaunti huku wananchi wakiendelea kuteseka;
kwahiyo waelekeze MUWASA waje kufanya kazi hii kesho,” Waziri Aweso
alimuelekeza Katibu Mkuu Sanga.
Waziri Aweso aliisisitiza MUWASA kukamilisha mradi kwa kipindi
walichokubaliana na alisema hatokubali kisingizio chochote hasa
ikizingatiwa fedha yote inayohitajika inatoka leo hii yaani Januari 6,
2020.
Aliwakumbusha watendaji kwenye Sekta ya Maji kuepuka kuzoea shida za
wananchi badala yake wajikite kuwatatulia kero ya maji na alibainisha
kwamba kutokana na changamoto alizozishuhudia wilayani humo
amejiridhisha kwamba Meneja wa RUWASA Rorya hana uwezo wa kutosha
kutatua changamoto zilizopo.
Waziri Aweso alielekeza meneja huyo apatiwe majukumu mengine na kwamba
apelekwe mtaalam mwingine atakayekuwa na uwezo wa kutatua changamoto
zilizopo wilayani hapo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment