Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ushauri ya wilaya ya Mbinga wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Kosmas Nshenye jana(hayupo pichani)wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri cha wilaya ambapo amewanyooshea kidole watendaji wa Shirika la Umeme Tanesco kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Picha na Mpiga Picha Wetu
********************************************
Na Mwandishi wetu,
Mbinga
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Kosmas Nshenye,amewataka wafanyakazi wa shirika la umeme Tanesco wilayani humo, kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wajielekeze katika kutatua kero na kuboresha huduma zao kwa wateja ikiwemo kumaliza tatizo sugu la kukatika umeme mara kwa mara.
Nshenye ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya(DCC) kilichofanyika katik ukumbi wa kanisa katoriki jimbo la Mbinga.
Alisema, shirika hilo linaonekana limeshindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na huduma mbovu inayotoa kwa wananchi ikiwemo kushindwa kuwaunganishia umeme wananchi licha ya kulipa gharama mbalimbali zinazotakiwa.
Alisema, serikali kupitia idara na taasisi zake ndiyo yenye jukumu la kutoa huduma bora kwa wananchi,kwa hiyo kama watumishi wa shirika hilo wameshindwa kufanya, hivyo ni vyema wakaondoka katika wilaya ya Mbinga ili waje watu wengine ambao wako tayari kuhudumia wananchi.
“kuna malalamiko mengi ofisini kwangu juu ya tabia yenu mbaya ya kuchukua fedha za watu lakini mnashindwa kuwapatia huduma,mimi nimechoka kusikia malalamiko dhidi yenu, kuanzia sasa nataka kila mwezi mlete taarifa ya utendaji wenu ofisini kwengu maana nyinyi wenyewe mmeshindwa kujisimamia”alisema Mkuu wa wilaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga Beda Hyera alisema,Tanesco ndiyo taasisi inayoongoza kuwatesa wananchi wa Mbinga kama Tanesco kutokana na tatizo la kukatika umeme mara kwa mara ambapo kwa siku unaweza kukatika kati ya mara kumi na tano na ishirini.
Alisema, kama shirika hilo halitabadilika kiutendaji kuna hatari wananchi wakakosa imani na kuichukia serikali yao ya Chama cha Mapinduzi kutokana na uzembe wa watendaji wa shirika hilo.
Ameitaka Tanesco kuhakikisha kinawafuatilia wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme kupitia miradi ya Rea kwani wanakiuka makubaliano ya mkataba kwa kuuza nguzo kwa wananchi,licha ya nguzo hizo kutolewa bure pamoja na kuwachukulia fedha kwa ahadi ya kuwaunganishia umeme majumbani.
Hyera alisema, jambo la kusikitisha baada ya kuchukua fedha hawaonekani eneo la mradi jambo lililoleta malalamiko mengi na kuna wananchi wenye lisiti zinazoonyesha wamelipia gharama lakini hadi sasa bado hawajapa huduma.
Aidha,amelalamikia kitendo cha wakandarasi wa Rea kupeleka umeme katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa barabara kuu na kuviacha vijiji vya pembezoni.
Mwenyekiti huyo wa Chama tawala, amemtaka meneja wa shirika hilo na timu yake kuwafuatilia mara kwa mara wakandarasi wa Rea wanaofanya kazi ya kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya utapeli kwa wananchi.
Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda, amezitaka taasisi za Serikali ikiwemo Tanesco kutoa huduma bora kwa wananchi, na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani tabia hiyo inarudisha nyuma mipango mizuri ya serikali ya awamu ya tano.
Amemtaka meneja wa Tanesco wilaya ya Mbinga kuwasimamia watumishi walio chini yake ili waweze kutoa huduma bora na kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo Rushwa ambavyo imekithiri sana kwa wafanyakazi wa shirika hilo.
Kaimu meneja wa Tanesco wilaya humo Fani Mwenda alisema, Tanesco haijapata malalamiko kuhusiana na mkandarasi kuuza nguzo hata hivyo amehadi kuanzia sasa watakuwa bega kwa bega na mkandarasi kufuatilia maeneo yaliyolalamikiwa ili wananchi wapate huduma
“sisi kama Tanesco tutamfuata meneja wa Rea ili twende maeneo yote yaliyolalamikiwa ili kufahamu changamoto zilizopo na kuzimaliza,sisi kama shirika la umma kazi yetu ni kutoa huduma bora bila upendeleo kwani ni wajibu wetu kufanya hivyo”alisema Mwenda.
Hata hivyo, amekiri baadhi ya maeneo kutofikiwa na mradi wa Rea na kuwataka wananchi wa maeneo hao kuwa wavumilivu wakati serikali iko katika hatua ya mwisho kutekeleza mradi wa Rea awamu ya tatu ambao utafika kila kijiji.Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment