Jane Edward, Michuzi TV- Arusha
MKUU wa Wilaya ya Hai Lengai ole sabaya amepongeza bunifu zilizofanywa na chuo cha Ufundi Arusha(Arusha technical College) kwa matumizi ya teknolojia zinazotumia dhana rafiki
Sabaya aliyasema hayo wakati akizindua umoja wa wanafunzi waliosoma katika chuo cha ufundi Arusha wenye lengo la kuendeleza ugunduzi walioufanya pamoja na kusaidia wanafunzi waliopo kujifunza juu ya teknolojia za kisasa na baadaye kusaidia jamii inayowazunguka.
"zipo mamlaka ndani ya serikali zinashindwa kuwapa nafasi wanachuo wanaoonyesha bunifu zao ,hali ambayo inasababisha nchi kutokuwa na vijana wazawa wenye uwezo wa kulitumikia Taifa." alisema Sabaya.
Alioongeza kuwa, ni kazi ya serikali kubeba vijana bunifu wanaoonyesha moyo na utayari katika mambo ya msingi ikiwemo vifaa ambavyo vimebuniwa na vijana wa chuo hicho cha ufundi ambavyo vinawezesha kutatua changamoto mbalimbali.
Sabaya alisema kuwa,ni vyema Nacte na TCU wakakaa pamoja na kuunda bodi moja itakayosaidia vijana wabunifu kufanikisha ugunduzi wao na sio kila mmoja kuwa na vigezo vyake kwani jambo hilo linawarudisha nyuma na kuwakatisha tamaa na kufanya jamii kuendelea kuamini teknolojia za nje.
Mkurugenzi wa elimu ya ufundi kutoka wizara ya elimu, Dokta Noel Mbonde alisema kuwa,ni vyema wanafunzi wanapohitimu chuo wakaendeleza kwa vitendo kile alichokipata kutoka chuoni hapo ili kuonyesha umuhimu wa uwepo wao.
"kitendo cha kuondoka huna chochote ulichokipata chuoni hautakuwa na msaada katika Taifa hili, hivyo natoa rai kujiendeleza na mwishowe kufikia nafasi za juu za uongozi kwani sisi tunapita hivyo mjitahidi nakuacha kujidharau nyie wenyewe kwani serikali hii inajali vijana,"alisema Dkt Noel.
Aliongeza kuwa, ni vyema vijana wasitegemee kuajiriwa bali wajiandae kujiajiri na kwa kufanya hivyo ni lazima wahakikishe wanaigeuza elimu walioipata kuwa ya vitendo zaidi.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho cha Ufundi,Issa Suleiman alisema kupitia umoja huo wanafunzi waliomaliza kwenye chuo hicho utasaidia kubadilishana uzoefu na ubunifu mbalimbali walionao lakini changamoto wanayopata ni upatikanaji wa fedha ili kuendeleza taaluma yao.
"Kilichopelekea kuzindua jumuiya hii ambayo itasaidia kupata fedha na kuangalia mpangilio wa fedha utakao enda kuendeleza ubunifu unaofanywa na baadhi ya wanafunzi ili kuachana na dhana ya kuuza wazo bali waweze kutengeneza bidhaa zao kamili,"alisema rais huyo.
Uzinduzi wa jumuiya hiyo ya wanafunzi waliomaliza chuo cha Ufundi Arusha, unatajwa kuwa na manufaa ya kuwafanya wahitimu hao kurudi chuoni na kutatua changamoto zinazoikabili chuo hicho katika nyanja mbalimbali.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment